Tafuta

Watanzania wanahamasishwa kushirikiana na kushikamana wakati huu walimwengu wanapoendelea kupambana na magonjwa mbalimbali ya maambukizi! Wametakiwa kupambana kikamilifu! Watanzania wanahamasishwa kushirikiana na kushikamana wakati huu walimwengu wanapoendelea kupambana na magonjwa mbalimbali ya maambukizi! Wametakiwa kupambana kikamilifu! 

Watanzania Jengeni Umoja na Mshikamano! Hiki Ni Kipindi Tete!

Watanzania wametakiwa kuendelea kuungana na kushikamana katika kipindi hiki ambacho dunia ina mahangaiko makubwa na magonjwa mbalimbali ya maambukizi. ”Tuendelee kumtegemea Mwenyezi Mungu kama Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alivyotusisistiza na tuendelee kuiamini Serikali na jitihada za viongozi wake tutapata amani na utulivu wa ndani! Yataka Moyo

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, Lindi na Tanga, Tanzania

Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kuendelea kushikamana katika kipindi hiki ambacho dunia ina mahangaiko makubwa na magonjwa mbalimbali ya maambukizi. ”Tuendelee kumtegemea Mwenyezi Mungu kama Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alivyotusisistiza na tuendelee kuiamini Serikali na jitihada za viongozi wake tutapata utulivu. Waziri Mkuu ameyasema hayo Jumatatu, Februari 22, 2021 wakati aliposhiriki mazishi ya mfanyabiashara maarufu katika mikoa ya Lindi na Mtwara Ally Nalaga yaliyofanyika Mnazimmoja Lindi. Amesema magonjwa hayo yameleta tafsiri tofauti na wakati mwingine kutokuwa na utulivu kwani watu wanatishana sana na hali ambayo inawafanya wasiwe na amani na kuwajengea hofu. Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kufuatilia mwenendo wa aina zote za magonjwa ambayo yanawakabili wananchi katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania na kuyatafutia tiba.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewasisitiza wananchi waendelee kuchukua tahadhari ya kila ugonjwa. ”Ukisikia ukimwi kuna tahadhari zake, ukisikia kipindupindu kina tahadhari zake.” Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini zote nchini Tanzania waendelee kuliombea Taifa na viongozi wake ili liendelee kuwa na amani na kimbilio kwa walipoteza amani na matumaini. Akimzungumzia  Marehemu Nalaga, Waziri Mkuu amesema alikuwa mcheshi na mwenye upendo kwa kila mtu na alijitoa sana katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii. ”Tumepoteza mtu muhimu kwenye jamii yetu ya Wana Lindi na Mtwara. Bwana Nalaga ametuachia mambo mengi hivyo tumuombea kwa Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema.” Waziri Mkuu amewaasa wananchi wayaenzi mambo yote mema aliyoyafanya enzi za uhai wake ikiwa ni pamoja na kujitoa katika shughuli za maendeleo ya jamii.

Wakati huo huo, Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema barakoa husaidia kujikinga na maambukizi ya magonjwa mbalimbali, hasa watu wanapokuwa wamekaa karibu. Ametoa kauli hiyo Jumamosi Februari 20, 2021 alipokuwa akitoa salamu za Serikali katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa Katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi wilayani Korogwe Mkoani Tanga. Amesema: “Pamoja na maombi, Watanzania tunapaswa tuendelee kufuata maelekezo ya Serikali bila kuwa na hofu. Serikali kupitia maabara na vituo vya kutoa huduma, inaendelea kuhakikisha huduma zinapatikana. Akimzungumzia Marehemu Balozi Kijazi, Waziri Mkuu aliwapa pole wafiwa na wanafamilia kutokana na msiba huo mkubwa na akamwelezea kwamba, alikuwa kiongozi mwenye mapenzi mema na Taifa lake lakini pia alikuwa na uwezo wa kutoa ushauri ambao ulikuwa na manufaa kwa Taifa. “Tunalo jukumu la kumuenzi kwa kuendeleza na kutenda mema yote aliyotuachia.”

Ibada ya kumwombea Marehemu Balozi Kijazi ilifanyika katika Kanisa la Mtakatifu Agustino, eneo la Manundu, mjini Korogwe, mkoani Tanga na iliongozwa na Askofu Mstaafu Telesphory Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro. Mapema, akizungumza katika mazishi hayo, Mkuu wa Majeshi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo alisema wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama walikuwa karibu naye kwa sababu Balozi Kijazi alikuwa ni Katibu wa Baraza la Usalama la Taifa. “Alikuwa ni mahiri, mpole na mwenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja ambazo zilieleweka na kukubalika katika vikao vyao,” alisema. Naye, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bw. Martine Shigela alisema Balozi Kijazi alikuwa ni Baba, kiongozi na mwalimu na wakati wote alikuwa ni kielelezo cha uchapakazi na uadilifu kwa watu wa mkoa wa Tanga. “Na kwa sababu hiyo, mkoa umeamua kuwa stendi ya mabasi ya mji wa Korogwe itaitwa jina la Balozi John Kijazi kwa heshima yake na ili kutunza kumbukumbu yake,” aliongeza. Mazishi hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wabunge wa mkoa wa Tanga. Mhandisi Balozi Kijazi alizaliwa mkoani Mwanza akiwa ni mtoto wa pili kwenye familia ya watoto 10. Ameacha mke, watoto watatu pamoja na wajukuu wawili.

23 February 2021, 15:02