Tafuta

WAKIMBIZI KUTOKA TIGRAY KWENDA SUDAN WAKIMBIZI KUTOKA TIGRAY KWENDA SUDAN 

Waziri Mkuu wa Ethiopia ahimiza vikosi vya waasi vya Tigray kujisalimisha

Waziri Mkuu Abiy Ahmed ametaka vikosi vya waasi vya Tigray kujisalimisha wakati Waziri mpya wa Mambo ya nje wa Ethiopia awahakikishia wanadiplomasia kwamba vita hivi karibuni vitaisha.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amezungumza kwa njia ya video ya dakika tano kwa lugha ya Kitigrigna akiwapa washiriki wa Kikosi Maalum cha Tigray uamuzi wa kujisalimisha kwa siku mbili hadi tatu. Na Waziri mpya wa Mambo ya nchi za nje wa Ethiopia, Demeke Mekonnen, amewahakikishia wanadiplomasia nchini Ethiopia kwamba serikali ilikuwa na nia ya kutimiza malengo yake na kumaliza mapigano katika eneo la Tigray.  Msemaji amethibisha kuwa taarifa hizo zilitolewa na Waziri mpya wa Mambo ya nchi za nje siku ya Ijumaa na kwamba Waziri, Mekonnen alisema kuwa  lengo kuu lilikuwa ni kurudisha utawala wa sheria katika mkoa wa Tigray na kuwafikisha katika haki za kisheria wahusika wa vita  kwa kipindi cha muda mfupi sana.

UN yaomba ufikiaji wa ukanda kwa ajili ya msaada wa kibinadamu

Kwa mujibu wa ripoti kwa waandishi, Mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ethiopia, Catherine Sozi, ameomba serikali ya Ethiopia kufungua njia za kuweza kufikisha msaada wa kibinadamu  ili utolewe kwa watu wanaohitaji msaada sasa. Ameomba pia kufunguliwa kwa miundombinu kama vile barabara, upatikanaji wa maji, mawasiliano ya simu na benki. “Ingawa zaidi ya wafanyakazi wa msaada wa kibinadamu 800 wanaishi katika eneo la Tigray, imekuwa ni vigumu kuwasiliana na kutoa msaada wa kibinadamu unaohitajika katika maeneo yenye mizozo”, amesema  Catherine Sozi. Maelfu ya wakimbizi wa Ethiopia wanaendelea kukimbia mapigano huko Tigray na wengi wamevuka hadi nchini Sudan.

Huduma ya Kijesuit kwa ajili ya wakimbizi wanaomba njia zifunguliwe

Dhamana ya upatikanaji wa misaada ya kibinadamu katika mkoa wa Tigray wa Ethiopia, ambayo imekuwa ikikabiliwa na mzozo mkali kati ya vikosi vya Serikali ya Shirikisho na Chama cha Ukombozi cha Watu wa Tigray (Tplf) kwa siku kumi na moja, ndiyo pia ombi kutoka  kwa kikosi cha Huduma ya Wakimbizi cha Kijesuit (JRS) cha  Afrika Mashariki, kupitia mkurugenzi mkuu wake, Andre Atsu. “Kama shirika la kibinadamu ameeleza mhusika huyo aliyenukuliwa na Shirika la habari za Kanisa Afrika (ACI)  kuwa  tunazindua wito ili kuhakikisha msaada wa kibinadamu, na watu walioathiriwa na mzozo wafikiwe vifaa muhimu”. Aidha amesema Mapigano ya silaha, kiukweli, yalilazimisha kufungwa kwa benki, maduka na njia za ufikiaji kwa miji kuu; Kwa maana  hiyo kuna hatari ya kweli kwamba ikiwa mapigano yataendelea, wafanyakazi wa kibinadamu, wakimbizi na watu wa jamuiya mbali mbali  watajikuta bila chakula na mahitaji mengine ya msingi”.

Wakimbizi wa Eritrea huko Tigray

Wakati huo huo, Padre wa Eritrea, Abba Mussie Zerai, kuhani wa Kanisa kuu la Asmara ametoa wito kwa ajili ya ulinzi wa wakimbizi wa Eritrea ambao wako katika mkoa wa Tigray. “Katika Tigray, kuna maelfu ya Waeritrea ambao mara nyingi wana njaa na wanakabiliwa na aina zote za unyonyaji na unyanyasaji. Hali hii ya sasa inaongezea kukata tamaa kwa watu hawa na inawaingiza mikononi mwa wafanya biashara haramu wa binadamu.

Maneno ya Papa Francisko Jumapili tarehe 8 Novemba

Jumapili iliyopita tarehe 8 Novemba, mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Papa Francisko alikuwa ameelezea  maskitiko yake na kufuatia na  habari zinazotoka nchini Ethiopia. Aliwashauri kupinga vishawishi  vya mapigano ya kisilaha na kuwaalika watu wote wasali na kuheshimiana kidugu, kwa njia ya mazungumzo na kutafuta amani dhidi ya kutokelewana. Vile vile hata Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki (Amecea) walioomba sehemu zote mbili kutafuta zababu na suluhisho la amani ili wasihatarishe vita vya wenyewe kwa wenyewe.

15 November 2020, 15:02