Tafuta

Harakati za Unicef katika maandalizi ya usafirishaji wa chanjo dhidi ya covid-19 Harakati za Unicef katika maandalizi ya usafirishaji wa chanjo dhidi ya covid-19 

UNICEF yawashirikisha wadau 350 katika mipango ya kusambaza chanjo ya Covid-19!

Wakati kazi ya kutengeneza chanjo ikiendelea,UNICEF inaongeza juhudi ikishirikiana na mashirika ya ndege,makampuni ya kusafirisha mizigo kwa ndege na kwa meli na jumuiya za masuala ya kiufundi ili kufikisha chanjo za kuokoa maisha haraka iwezekanavyo na kwa usalama.Ni kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Unicef wa masuala ya usambazaji ambapo wamewashirikisha makampuni ya Ndege mipango ya kusambaza chanjo ya COVID-19.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limeanza majadiliano hivi karibuni na mashirika zaidi ya 350 duniani kote  ili kupanga mipango ya kusambaza chanjo dhidi ya corona au COVID-19 pindi zitakapokuwa tayari. Kwa mujibu wa UNICEF wadau hao ni makampuni makubwa ya safari za ndege na makampuni ya kusafirisha mizigo kwa njia ya bahari  kwa lengo la kuandaa juhudi za pamoja za kufikisha chanjo ya COVID-19 kwa zaidi ya nchi 92 kote duniani pindi tu chanjo hiyo itakapokuwa tayari.

Katika kuanza maandalizi  ya mchakato huo UNICEF ikishirikiana na shirika la afya kwa nchi za Amerika PAHO na jumuiya ya kimataifa ya usafiri wa anga (IATA) waliyaeleza mashirika makubwa ya usafiri wa ndege duniani juma lililopita kuhusu uwezekano wa safari za ndege unaohitajika na kujadili njia za kusafirisha dozi karibu bilioni 2 za chanjo ya COVID-19 mwaka 2021. Dozi hizo ni mabomba ya sindano bilioni 1 ambayo yanatarajiwa kusafirisha kwa njia ya bahari na meli za mizigo.  Mkutano wa Jumatatu tarehe 23 Novemba ni wa kwanza wa aina hiyo kufanywa na UNICEF kwa njia ya mtandao kujadili usafirishaji wa chanjo ya COVID-19 ukiwaleta pamoja wadau zaidi ya 350 yakiwemo mashirika ya safari za mizigo za ndege, makampuni ya usafirishaji mizigo kwa meli na jumuiya za kimataifa za masuala ya kiufundi.

Naye Etleva Kadili mkurugenzi wa UNICEF wa masuala ya usambazaji amesema “Wakati kazi ya kutengeneza chanjo hizo ikiendelea, UNICEF inaongeza juhudi ikishirikiana na mashirika ya ndege, makampuni ya kusafirisha mizigo kwa ndege na kwa meli na jumuiya za masuala ya kiufundi ili kufikisha chanjo za kuokoa maisha haraka iwezekanavyo na kwa usalama. Ushirika huu wenye thamani kubwa utakwenda mbali kuhakikisha kwamba kuna uwezo unaohitajika wa usafirishaji kwa ajili ya operesheni hii ya kihistria, tunahitaji kila muhusika kujituma wakati huu wa maandalizi ya kusafirisha dozi za dawa, mabomba ya sindano na vifaa zaidi vya kujikinga ili kuwalinda wahudumu walio msitari wa mbele kupambana na janga hili kote duniani. Kwa kuwalinda wahudumu hawa bila shaka tunawalinda mamilioni ya Watoto ambao wanawategemea wahudumua hawa.”  Ameongeza kuwa uungaji mkono kutoka kwa serikali, washirika, na sekta binafsi utakuwa muhimu sana katika kusafirisha chanjo hizo za COVID-19 kama ilivyo kwa chanjo za magonjwa mengine kama yanayokatili maisha ikiwemo surua, kifaduro na pepopunda.

24 November 2020, 16:29