Tafuta

Bwana Joe Biden ni rais mteule wa Marekani. Bwana Joe Biden ni rais mteule wa Marekani. 

Pongezi kutoka sehemu nyingi za dunia kwa rais mteule Joe Biden

Viongozi ulimwenguni kuanzia Afrika,Ulaya,Asia na Amerika zote wamemtumia salaam za pongezi rais mteule wa Marekani Bwana Joe Biden.Kwa walio wengi wanaonesha tumaini la umoja na ushirikiano ambao wanadai kusubiri kwa matarajio makubwa.

Salaam za pongezi zimetoka katika miji mikuu ya dunia, barani Ulaya, Asia, Afrika kwa ajili ya rais mteule Bwana Joe Biden na zaidi wakionesha matumaini ya kuweza kurudisha uhusiano ambao wanadai ulikuwa umeanza kuyumba na zaidi katika mawasiliano ya mataifa ya kanda ya Atlantiki na mengine. Kutoka nchini Italia, Rais wa Jamhuri Bwana Sergio Mattarella na Waziri Mkuu wa Italia, Bwana Conte wametoa pongezi zao kwa Rais mteule Joe Biden na kumtakia kazi njema na kwamba wanataongeza nguvu ya uhusiano kati ya Italia na Marekani kwenye ujumbe wa Twitter.  Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron  katika ujumbe wa Twitter amesema kwamba, Wamarekani wamemchagua rais wao. “Hongera Biden na Kamala Harris. Tuna mengi ya kufanya kushughulikia changamoto za sasa. Tushirikiane pamoja". Naye Kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel amempongeza Biden na Bi Harris kamala, katika taarifa yake na kwamba ni matazamio ya kushirikiana pamoja na viongozi hao wateule wote.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson pia amepongeza Rais mteule Biden na Bi Kamala, na kusema Marekani ndiyo mshirika muhimu zaidi wa Uingereza na anatazamia kufanya kazi kwa karibu zaidi juu ya vipaumbele vyao vya pamoja, kuanzia mabadiliko ya tabianchi, hadi biashara na usalama. Naye Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, mshirika wa karibu wa rais Trump, amemtaja Biden kuwa rafiki mkubwa wa Israeli, na kumpongeza yeye pamoja na Harris juu ya ushindi wao. Amesema hayo  katika ujumbe wa twitter: “Natazamia kufanya kazi pamoja na nyote wawili kuimarisha zaidi ushirikiano maalumu kati ya Marekani na Israeli”.

Mfalme wa Jordan, Abdullah II, pia ametumia ujumbe wake katika mtandao wa Twitter kuwapongeza washindi hao wawili akisema, “natazamia kushirikiana nanyi kuendeleza ushirkiano imara kati ya Jordan na Marekani, katika kuendeleza malengo yetu ya pamoja ya amani, utulivu na ustawi.” Waziri mkuu wa Canada Justion Treduea, amesema pia anatazamia kushirikiana na rais mteule Bwana Biden na makamu wake Bi Harris, utawala wao na bunge la Marekani wakati wakishughulikia changamoto kubwa zaidi za dunia.

Kutoka Afrika:Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, ameto wito wa ushirikishwaji zaidi wa bara la Afrika. Amesema kuwa anatazamia ushirikiano zaidi kati ya Nigeria na Marekani, hasa katika ngazi za uchumi, diplomasia na siasa, ikiwemo kuhusu vita dhidi ya ugaidi. Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, amesema hayo naye kupitia Twitter kwamba serikali yake inatazamia kufanyakazi pamoja na viongozi hao wateule, kuimairisha urafiki na ushirikiano.

Kutoka Amerika ya Kusini: Rais wa Mexico Manuel Lopez Obrador yeye amesema  hata hivyo amesema ni mapema mno kumpongeza Biden na kwamba atasubiri hadi masuala yote ya kisheria kuhusu uchaguzi huo yatatuliwe. Na kwa upande wake, katibu mkuu wa jumuiya ya kujihami NATO, Jens Stoltenberg, ameeleza Bwana Biden kama muungaji mkono thabiti wa muungano huo, na kwa maana hiyo amethibitisha marajio ya kushirikina na Biden.

08 November 2020, 15:01