Tafuta

Washiriki wa Mkutano huko Tunis kwa ajili ya masuala ya mgogoro wa Kanda ya Libia Washiriki wa Mkutano huko Tunis kwa ajili ya masuala ya mgogoro wa Kanda ya Libia 

Libia inafanya mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa

Mkutano wa Mazungumzo ya kutafuta muafaka kwa sehemu zote zinazokumbwa na gmgogoro wa Libia unaendelea jijini Tunis,kwa kuongozwa na Umoja wa Mataifa.Katika ujumbe kwa njia ya Video kwa washiriki hao Katibu Mkuu wa umoja wa Mataifa amesema "wakati ujao wa Libia huko mikononi mwenu".

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Umoja wa Mataifa umeanzisha  mazungumzo huko Libia yanayolenga kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na kuandaa uchaguzi ambao utaleta amani baada ya muongo mmoja wa machafuko katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini. Jumapili wakati wa sala ya Malaika wa Bwana, Papa Francisko aliombea mkutano huo uweze kuleta mwafaka wa kusitisha uwagaji damu kwa watu wasio na hatia.

Wajumbe 75, waliochaguliwa na Umoja wa Mataifa kuyawakilisha mashirika ya serikali na makundi ya kisiasa na kijamii nchini Libya, walikutana nchini Tunisia baada ya miezi kadhaa ya utulivu na mpango muhimu wa kuweka chini silaha uliofikiwa Oktoba. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliwaambia wajumbe hao kwa njia ya video katika hafla ya ufunguzi kuwa wana fursa ya ya kumaliza mzozo huo uliosababisha maafa na sasa ni zamu yao kuutengeneza mustakabali wa nchi yao. “Mnaweza kuutegemea Umoja wa Mataifa katika kuunga mkono juhudi zenu. Na jumuia ya kimataifa kutoa msaada wake mkubwa pia, ikiwemo kuhakikisha kikamilifu marufuku ya silaha. Mustakabali wa Libia na watu wake ni mkubwa kuliko tofauti zozote za mtu binafsi au vyama. Mustakabali wa Libia sasa uko mikononi mwenu”,amesema Bwana Guterres.

Kaimu mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Stephanie Williams alizngumzia matumaini ya nadra akisema kuwa baada ya miaka mingi ya mgogoro, anaamini hatimaye kuna mwanga mdogo wa matumaini. Mazungumzo hayo ya siku sita yanafanyika katika hoteli moja ya kifahari katika mji wa Mediterenia wa Gammarth, nje kidogo ya Mji Mkuu wa Tunisia, Tunis. Hata hivyo mkutano huo jijini Tunis unatokana na utulivu wa miezi kadhaa uliojitokeza nchini Libia na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosainiwa mwezi Oktoba kati ya kambi mbili kuu katika mzozo huo wa muda mrefu. Makubaliano ya kusitisha mapigano ya mwezi Oktoba yameruhusu  hata kuanza tena kwa uchimbaji wa mafuta na hatua iliyopigwa katika juhudi za kuumaliza vizingiti vya  kisiasa uliodumu kwa miaka kadhaa, lengo likiwa kuiunganisha nchi hiyo chini ya utawala mmoja na kufungua njia ya uchaguzi wa kitaifa.

10 November 2020, 16:05