Tafuta

2020.20.11: Siku ya Mtoto duniani 2020.20.11: Siku ya Mtoto duniani 

Siku ya Mtoto kimataifa:Kila mtoto akaribishwe,atetewe,asaidiwe na ulinzi!

Katika siku ya Mtoto duniani tarehe 20 Novemba,Papa Francisko ametoa ujumbe wake kwa njia ya mtandao kuwa kila mtoto anahitaji kukaribishwa na kutetewa,kusaidiwa na kulindwa tangu tumboni mwa mama yake.Katika muktadha huo Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa UNICEF inaonesha kuwepo kwa ongezeko kubwa la madhara ya janga la ugonjwa wa Corona kwa watoto wakati bado linaendelea kusalia ulimwenguni.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Katika siku ya Mtoto duniani tarehe 20 Novemba, Papa Francisko ametoa ujumbe wake kwa njia ya mtandao akisema kuwa kila mtoto anahitaji kupokelewa na kutetewa, kusaidiwa na kulinda tangu aiwa tumboni mwa mama yake. Hata hivyo kuhusiania na mantiki ya siku hiyi, tarehe 19 Novemba 2020 imetolewa Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF ikionesha kuwepo kwa ongezeko kubwa la madhara ya janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 kwa watoto wakati huu ambapo janga hilo linaelekea kuingia mwaka wa pili. Ni katika taarifa ya ripoti hiyo iliyotolewa jijini New York, Marekani kuelekea siku ya mtoto duniani tambayo uadhimishwa kila ifikapo Novemba 20.

Ripoti hiyo iliyopewa jina “Kukwepa kupoteza kizazi cha COVID-19”, ni ya kwanza kuangalia kwa kina madhara ya janga hilo kwa watoto. Inaonesha kuwa ingawa dalili za Corona kwa watoto si dhahiri sana, maambukizi yanaongezeka, na athari za muda mrefu katika elimu, lishe na ustawi katika kizazi kizima na vijana zinaweza kuwa nao katika maisha yao yote.  Bi Henrietta Fore, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF amenukuliwa akisema, kuwa: “wakati wote wa janga la COVID-19, kumekuwepo na fikra potofu ya kwamba watoto hawaathiriwi na janga hilo. Ilhali watoto watoto wanaweza kuugua na kusambaza Corona, hilo ni jambo dogo sana. Kuvurugwa kwa huduma muhimu na kuongezeka kwa umaskini ni tishio kubwa zaidi kwa watoto. Kadri janga hili linavyoendelea kuwepo, madhara yake kwa watoto yanaongezeka hasa kwenye elimu, afya, lishe na ustawi. Mustakabali wa kizazi kizima uko hatarini.”

Ripoti imebaini kuwa hadi tarehe 3 mwezi huu wa Novemba, katika nchi 87 zilizokuwa zina takwimu zilizochambuliwa, watoto na vijana wajoli wenye umri chini ya miaka 20 walikuwa wagonjwa 1 kati ya 9 walioripotiwa kuambukizwa virusi vya Corona.  Kiwango hicho kinamaanisha asilimia 11 ya watu milioni 25.7 waliopata Corona kwenye mataifa hayo.  Ripoti pia inasema kuwa wakati watoto wanaweza kuambukizana virusi hivyo wao wenyewe na hata kwa watu wazima, kuna ushahidi wa kutosha kuwa iwapo kuna mikakati thabiti ya usalama, faida ya kufungua shule ni kubwa zaidi kuliko gharama za kufunga shule hizo., Shule si kichocheo kikuu cha maambukizi ya Corona, na watoto wanaweza zaidi kuambukizwa virusi hivyo wakiwa nje ya shule,” imesema ripoti hiyo.

Ripoti kadhalika inabainisha kuwa katika theluthi moja ya nchi zilizoshiriki kwenye utafiti, kulikuwepo na anguko la asilimia 10 la utoaji wa huduma za afya kama vile chanjo, huduma za mama na mtoto na zile za tiba za magonjwa ya maambukizi. Halikadhalika, huduma za lishe kwa wanawake na watoto zimepungua kwa asilimia 40 kwenye nchi 135.  Hadi mwezi uliopita wa Oktoba, watoto milioni 265 hawakuweko shuleni na hivyo kukosa huduma ya mlo bora. Zaidi ya watoto milioni 250 wenye umri wa chini ya miaka mitano wanakosa huduma za kuokoa maisha ikiwemo matone ya vitamini na vyakula vyenye virutibisho.  Zaidi ya yote, nchi 65 zilieleza kuwa wahudumu wa kijamii hivi sasa hawatembelei majumbani kutoa huduma ikilinganishwa na mwaka jana. Kwa upande wa elimu, hadi mwezi huu wa Novemba, watoto milioni 572 wameathiriwa kutokana na shule kufungwa katika nchi 30. 

Kwa upande wa UNICEF ina mapendekezo 6 kwa serikali na wadau wake ambapo mosi inataka wahakikshe watoto wote wanajifunza ikiwemo kupunguza pengo la kupata huduma za teknolojia.  Pili, huduma za lishe, afya na chanjo zipatikane kwa watoto wote bila kujali uwezo wa wazazi, tatu kusaidia na kulinda afya ya akili kwa watoto na vijana na kuepusha unyanyasaji, ukatili wa kingono na kutelekeza watoto.  Pendekezo la nne ni kuongeza upatikanaji wa huduma za maji safi, kujisafi na uhifadhi wa mazingira na kukabili mabadiliko ya tabianchi.  Tano kubadili mwelekeo wa sasa wa watoto kuwa maskini na kuhakikisha kila mtu anakwamuka kutoka COVID-19 na sita ni kuongeza maradufu juhudi za kulinda na kusaidia watoto na familia zao zilizoko kwenye majanga, ukimbizi na vita.  Bi. Fore amekumbusha kuwa wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto duniani, “tunaomba serikali na wadau wake na sekta binafsi wasikilize watoto na wapatie kipaumbele masuala yao. Tunapofikiria upya mustakabali wa watoto, na kuangalia dunia baada ya Corona, watoto lazima wawe kipaumbele.” 

20 November 2020, 17:30