Tafuta

Mwaka 1995, mjini Beijing walikuwepo wanawake 12 wakuu wa nchi na serikali na leo hii tuna wanawake 22 wakuu wa nchi na serikali katika mataifa 193. Mwaka 1995, mjini Beijing walikuwepo wanawake 12 wakuu wa nchi na serikali na leo hii tuna wanawake 22 wakuu wa nchi na serikali katika mataifa 193. 

UN-Women-Bi.Mongela:Yapo mafanikio ya miaka 25 baada ya Beijing,licha ya changamoto!

Getrude Mongela,alikuwa ni Katibu Mkuu wa mkutano wa 4 wa kimataifa wa wawanake uliofanyika Beijing,China mwaka 1995.Baada ya miaka 25 tangu mkutano huo ufanyike anaona hatua zilizopigwa kwa kiasi fulani na zaidi katika suala elimu ambapo mataifa mengi yamekubaliana kutekeleza usawa kati ya mtoto wa kike na wa kiume.

Tarehe Mosi Oktoba 2020  katika mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, (UNGA75) kikao chake cha  ngazi ya juu kimehusu kuchagiza utekelezaji wa usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake na mtoto wa kike, sambamba na maadhimisho ya miaka 25 tangu mkutano wa 4 wa kimataifa kuhusu wanawake ufanyika Beijing nchini China manmo mwaka 1995. Katika mkutano huo wa Beijing, washiriki kutoka nchi maskini na tajiri walipitisha mwongozo wa utekelezaji wa Beijing wenye kurasa 129 na vipengele 12 vya kuzingatia. Mambo hayo ni umaskini, elimu na mafunzo, afya, ghasia, mizozo ya kivita, uchumi, madaraka na upitishaji maamuzi, mifumo ya kitaasisi, haki za binadamu, vyombo vya habari, mazingira na mtoto wa kike. Katibu Mkuu wa mkutano huo wa Beijing wa wakati ule alikuwa ni Bi Getrude Mongela na ambaye amehojiwa na katika kituo cha habari wa Umoja wa Mataifa (UNIC) nchini Tanzania kwa kutaka kujua nini kimeendelea mara baada ya miaka hii 25 ya mkutano huo

Akijibu swali hili Bi Mongela amesema, “miaka 25 sasa imepita tumeangalia yote tuliyokubaliana Beijing, tumeona tumepiga hatua kiasi gani. Inapokuja kwenye suala kama elimu, mataifa mengi yamekubaliana kutekeleza usawa kati ya mtoto wa kike na wa kiume. Na Tanzania anafikiri wamefanya kazi nzuri zaidi, na jambo ambalo limemffurahisha zaidi rais na serikali yake ya awamu ya 5, ambao wamechukua uamuzi wa kuhakikisha watoto wote wa shule hawalipi karo tangu wanapoanza shule hadi anapomaliza kidato cha 4. Watu wengi labda hawajui, hayo ni mapinduzi makubwa. Akikimbuka enzi zake amesema “Tuliposoma sisi, tatizo lilikuwa moja asomeshwe mtoto wa kike au wa kiume.”

Je kwa upande wa nchi nyingine za Afrika?, Bi Mngela ameema  “wenzetu kama vile wa nchi za Afrika magharibi wengi wamejiimarisha katika uchumi. Mwanamke ana uchumi na ana uwezo. Kwa mfano wenzetu huko Nigeria unakuta mwanaume ameoa wanawake wanne, na si kwamba awatunze, wamtunze yeye. Kwa hiyo kuna mabadiliko mengine si mazuri sana lakini inaonesha uwezo wa mwanamke kiuchumi na haya yamefanyika kwenye maeneo mengi.” Aidha Bi Mingela amesema  kuwa “tulikuwa na matatizo, tulipoenda Beijing, ilikuwa malipo ya mwanamke wanafanya kazi ile ile, ni mwalimu kama mwalimu wa kiume lakini mwalimu wa kiume atalipwa zaidi kuliko mwalimu wa kike, au daktari wa kiume atalipwa zaidi kuliko daktari wa kike. Hayo nayo yamesawazishwa. Tumekuwa na hatua mbalimbali kila sehemu lakini bado tuna changamoto”.

Mkutano wa kwanza wa kimataifa wa wanawake ulifanyika Mexico City nchini Mexico mwaka 1975, wa pili ulifanyika Copenhagen, Denmark mwaka 1980 na kisha Nairobi Kenya mwaka 1985 na miaka 20 baadaye Beijing China mwaka 1985.  Hata hivyo Azimio la Beijing na Jukwaa la kuchukua hatua vimefungua zama mpya ya kusaka usawa wa kijinsia, kwa mujibu wa Bi  Phumzile Mlambo-Ngcuka katika hotuba yake aliyotoa tarehe Mosi Oktoba 2020  kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani wakati wa miaka 25 ya maadhimisho ya mkutano wa kimataifa wa wanawake, FWCW uliofanyika Beijing, China. Bi. Ngcuka ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN-Women amesema, azimio hilo, “limeleta mabadiliko chanya makubwa ikiwemo marekebisho ya kisheria 274 katika mataifa 131. Wanawake zaidi hivi sasa wanashiriki kwenye michakato ya amani. Uhalifu wa kijinsia kwenye mizozo sasa unatambuliwa chini ya sheria za kimataifa na wahusika wanafunguliwa mashtaka. Maisha ya watoto wa kike na wanawake yamenufaika na ongezeko la kuandikishwa shuleni sambamba na huduma za uzazi.”

Akamulika pia wanawake kwenye uongozi wa juu akisema, “mwaka 1995, mjini Beijing walikuwepo wanawake 12 wakuu wa nchi na serikali na leo hii tuna wanawake 22 wakuu wa nchi na serikali katika mataifa 193.” Hata hivyo amesema licha ya mafanikio hayo bado kuna changamoto ikiwemo kuwa mafanikio hayatoshelezi na pia kasi ni ndogo sana. Kwa kuto mfano Amesema uongozi wa wanawake, ikiwemo wasichana ni muhimu sana wakati huu wa dharura ya kujenga upya jamii baada ya janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, “wanawake na wakazi wa dunia wanataka mabadiliko haya.” Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UN-Women amesema katika muongo wa hatua uliobakia kuelekea ukomo wa 2030, hakuna tena kisingizio chochote katika ukosefu huo wa mizania kwenye uongozi. Amesema ushirikiano wa kimataifa na Umoja wa Mataifa ni vitu muhimu, wanawake wanaamini kwenye hilo na hivyo ni lazima iwe jumuishi, “Wanawake hivi sasa wanataka kasi ya haraka zaidi kuelekea uwakilishi wa asilimia 50 kwa 50 katika nyanja zote kuanzia mabaraza ya mawaziri, bodi za mashirika kwenye uchumi ambako pia wanawake wajumuishwe kama wanufaika wa mipango ya kuchechemua uchumi baada ya COVID-19.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Bi. Ngcuka amesema  kuwa ameonesha utashi wa kisiasa na uamuzi thabiti kuanzia ngazi za juu za uongozi kwenye chombo hicho. Hivyo amesema, tuko "katika njiapanda. Mustakabali unategemea ushiriki wa vizazi vyote, watu wa rangi zote na watu wenye uwezo mbalimbali ili kila pahali duniani, mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 10 mwaka 2020 aweze kuwa na ustawi bora kama msichana ifikapo mwaka 2030.” Ameshukuru wale wote walioungana katika jukwaa la wadau mbalimbali la Kizazi cha Usawa, zikiwemo serikali, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na wanaume na wavulana, viongozi na wenyeviti wenza wa jukwaa hilo ambao ni Ufaransa na Mexico. Amekumbusha kuwa wanawake duniani wanaamini kwenye Umoja wa Mataifa na mashikamano na mataifa wanachama akisema wanaamini sote kwa pamoja “tunaweza kubadili mustakabali wetu ambao uko mikononi mwetu.”

02 October 2020, 15:22