Tafuta

Watanzania wanahamasishwa kujiandaa kutumia fursa ya reli ya kisasa na Bandari Kavu ya Isaka ili kujiletea maendeleo fungamani. Watanzania wanahamasishwa kujiandaa kutumia fursa ya reli ya kisasa na Bandari Kavu ya Isaka ili kujiletea maendeleo fungamani. 

Uchaguzi Mkuu Tanzania 2020: 28 Oktoba! Reli Na Bandari Kavu

Watanzania wanaendelea kuhamasishwa ili waweze kujiandaa tayari kutumia fursa ya ujenzi wa reli ya kisasa na ujenzi wa bandari kavu ili kuweza kujiletea maendeleo fungamani katika maisha yao. Tanzania inahitaji kiongozi mahiri, atakayesimamia na kuratibu rasilimali za nchi kwa ajili ya mafao ya watanzania wote; kiongozi mwenye hofu na mchaji wa Mungu na mpenda watu wake!

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Shinyanga, Tanzania

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewakata wakazi wa Isaka, wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga wawe tayari kutumia fursa ya ujenzi wa reli ya kisasa na ujenzi wa bandari kavu ili kujiletea maendeleo. Ametoa wito huo Ijumaa, Oktoba 2, 2020 wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa kata za Kagongwa na Isaka akiwa njiani kuelekea kata ya Kakole katika jimbo la Msalala. Amesema Isaka ni kitovu kikubwa cha biashara kwa sababu kuna miradi mikubwa miwili ambayo itatekelezwa. “Kwanza kutakuwa na bandari kavu ambayo itakuwa inapokea mizigo kutoka nchi tofauti zinazotuzunguka. Kwa hiyo wana Kagongwa, tumieni fursa hii kufanya biashara. Wana Isaka tumieni fursa hii kujenga nyumba za kulala wageni na mahoteli ya kuuza vyakula.” “Pili ni reli ya kisasa ambayo tunapanga kuijenga itapita hapa Isaka. Reli hii ikikamilika, mtu atakuwa anatumia saa nne kwenda Dar es Salaam badala ya saa 14 ambazo zinatumika hivi sasa kwa usafiri wa mabasi.” Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Shinyanga kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli alitumia fursa hiyo kuwanadi wagombea udiwani wa jimbo la Msalala. Mgombea ubunge wa jimbo la Msalala, Bw. Iddi Kassim Iddi amepita bila kupingwa.

Wakati huo huo, akizungumza na wakazi wa Kata za Segese na Kakola, Mheshimiwa Majaliwa amesema barabara ya kutoka Geita kupitia Kagongo hadi Kahama yenye urefu wa km. 106 itajengwa kwa kiwango cha lami. "Barabara hii ilikuwemo kwenye ilani inayomalizika sasa uk.66 na ilipangiwa kufanyiwa upembuzi yakinifu lakini katika ilani yetu ya sasa, inatakiwa kukamilishwa ili wananchi muanze kufanya biashara kwa urahisi." Katika hatua nyingine, akimwombea kura Rais Magufuli kwenye mikutano huo, mgombea ubunge wa jimbo la Shinyanga Mjini, Bw. Patrobas Katambi amesema wakazi hao wana kila sababu ya kukichagua Chama cha Mapinduzi kwa vile kina sera za kuwaendeleza watu wa makundi tofauti wakiwemo vijana na wanawake.  "Ndugu zangu msidanganywe, tarehe 28 twendeni tukamchangue Dkt. Magufuli, mbunge na madiwani wa CCM kwa sababu watatuletea maendeleo. Usipoteze muda, kwa mjomba hakuna urithi. Rudi nyumbani kumenoga," amesema. Aliwataka wakazi hao wajihadhari wasiwachague wagombea wa upinzani kwani wameahidi kuweka rehani madini ya Tanzania ili wapate fedha endapo watachaguliwa kuongoza nchi. "Wamesema wataweka madini yetu rehani ili wapate fedha, sasa tukiwapa nchi, si watatuweka na sisi rehani?" Alihoji.

“TANZANIA ni nchi kubwa inazidi kilometa za mraba 947,000. Ina makabila zaidi ya 120 na wakazi wake wanakaribia milioni 60. Inahitaji kiongozi mahiri na mwenye hofu na uchaji wa Mungu.” Hiyo ni kauli ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa aliyoitoa hivi karibuni wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Ngara Mjini, kwenye mkutano uliofanyika katika viwanja vya Posta, wilayani Ngara, mkoani Kagera. Mheshimiwa Majaliwa ambaye alikuwa mkoani Kagera kwa nia ya kumwombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Ngara, Bw. Ndayisaba George Ruhoro na mgombea udiwani wa CCM wa kata ya Ngara Mjini, Bw. Stanford Kennedy. Akifafanua sifa za kiongozi anayetakiwa kuiongoza Tanzania, Mheshimiwa Majaliwa alisema: “Tunataka tupate kiongozi mwenye hofu ya Mungu. Tanzania inahitaji kiongozi mahiri, mzalendo, mwadilifu na mwaminifu ambaye ni lazima tujiridhishe kuwa ataweza kuongoza nchi.” “Nimeangalia katika wote wanaotaka kupewa Urais, hakuna kiongozi mwenye hizo sifa zaidi ya Dkt. John Pombe Magufuli.

Tulimpa miaka mitano ya kuongoza nchi, amefanya mambo makubwa na nyote mmeona ama kusikia yaliyofanyika kupitia vyombo vya habari.”  Alisema Chama cha Mapinduzi ndicho chama pekee kinachoweza kuwatumikia Watanzania mpaka wale wanyonge, na akawaomba wakazi hao wawapigie kura wagombea wa CCM ili wawatumikie. “Dkt. Magufuli ni kiongozi ambaye anaweza kuiongoza nchi, ndiye kiongozi anaweza kuunda Serikali na kuisimamia ili iende ikawatumikie Watanzania mpaka wa chini kabisa kwa sababu ya uchapakazi wake. Ikifika tarehe 28 Oktoba, nendeni mkamchague kwa kura nyingi ili aendelee kuongoza,” alisisitiza. Alisema Dkt. Magufuli ni kiongozi mwenye hofu ya Mungu aliyemtanguliza Mungu mbele katika kuleta mafanikio ya Taifa hili. “Kwa hiyo tunahitaji kiongozi mwenye hofu ya Mungu na ndiyo maana tulifanikiwa pia kupambana na vitu vingine vyote baada ya kumtanguliza Mungu. Kwani Corona, COVID-19 bado ipo?” alihoji na kujibiwa hakuna. “Hii ni kwa sababu ya kumwamini Mungu.

Alitusihi Watanzania tufunge kwa siku tatu na tuombe kila mmoja kwa imani yake. Je, hatujafanikiwa?” alihoji na kujibiwa tumefanikiwa. Akielezea uboreshaji wa miundombinu ya barabara, Mheshimiwa Majaliwa alisema baada ya kukamilisha usanifu na upembuzi yakinifu, Ilani ya CCM ya 2020-2025 inatamka bayana kuwa barabara zinazounganisha wilaya hiyo na mji Bukoba kupitia Karagwe zitajengwa kwa kiwango cha lami. “Barabara ya Lusahunga - Rusumo (km 92), Nyakanazi - Kobelo (km.60), Bugene -Kasulo (km.124) na Murugarama - Rulenge - Nyakahura (km 85) ziko kwenye mpango mahsusi ambao ni Ilani ya Uchaguzi ya CCM,” alisema. Kuhusu maji, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa CCM itaendelea kuimarisha huduma za maji katika maeneo yote nchini lengo ni kuhakikisha kaulimbiu ya kumtua ndoo mama kichwani inatimia. Mheshimiwa Majaliwa alisema katika wilaya ya Ngara, sh. bilioni 6.38 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya vijijini vikiwemo vijiji vya Makubu, Mbuba, Murugarama, Rwinyana, Kanazi na Kabelenzi, Murunyagira, Rusumo, Mshikamano, Kasharazi, Kasulo, Rwakaremela na Mugoma. Alisema fedha hizo pia ziliwezesha ujenzi wa visima 23 kwa vijiji vya Kasulo, Kasharazi, Bukiriro, Rwakaremela, Nyakariba, Mwivuza, Mukubu, Kashinga, Kazingati, Bulengo, Chivu, Keza, Mbuma, Mukubu, Kashinga, Kigina, Nyamahwa, Nyamiyaga, Kanyinya, Murubanga, Kazingati, Nyarurama na Nyamahwa. Alisema mradi uliosaidia wilaya ya Ngara kupata maji ni ujenzi wa miradi ya maji kutokana na fedha za mchango kwa jamii (CSR) kupitia mradi wa umeme wa Rusumo ambapo sh.  bilioni 11.5 zilitumika katika vijiji vya Kasulo, Rwakalemela, Mshikamano na Kasharazi.

05 October 2020, 14:54