Tafuta

15 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya wanawake vijijini.Umoja wa Mataifa unataka uwekezaji wa maeneo ya vijijini unaojali jinsia na ndiyo lengo la kuangazia  siku hii kwa  mwaka huu 2020. 15 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya wanawake vijijini.Umoja wa Mataifa unataka uwekezaji wa maeneo ya vijijini unaojali jinsia na ndiyo lengo la kuangazia siku hii kwa mwaka huu 2020.  

Siku ya Kimataifa ya wanawake vijijini:Changamoto ni nyingi hasa wakati wa covid-19!

Tarehe 15 Oktoba ni siku ya kimataifa ya wanawake wa vijijini ikiangazia umuhimu wa kujenga mstakabali wa kundi hilo wakati huu ambapo dunia imekumbwa na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au covid-19.Maadhimisho haya uangukia katika wiki ambayo Umoja wa Mataifa unaadhimisha Siku ya Chakula Duniani ambayo ni tarehe 16 Oktoba na Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Umaskini tarehe 17 Oktoba.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Siku ya Kimataifa ya Wanawake Vijijini ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia Azimio 62/136 la tarehe 18 Desemba 2007, kwa lengo la kutambua jukumu muhimu la wanawake wa vijijini katika kukuza maendeleo ya vijijini na kilimo, kuchangia usalama wa chakula na kutokomeza umaskini vijijini. Umoja wa Mataifa kupitia ukurasa wake maalum wa siku ya Kimataifa ya wanawake wa vijijini, tarehe 15 Oktoba 2020 unasema kuwa wanawake na wasichana wako upande wa changamoto zaidi wakati huu wa janga, changamoto ambayo inaongezwa zaidi ukizingatia mazingira wanamoishi ya vijijini. Wanawake wa vijijini, wakiwa na jukumu la msingi kwenye kilimo, uhakika wa chakula na lishe, wanakabiliwa na changamoto katika maisha yao ya kila siku.  Kwa sasa, tangu kuanza kwa janga la COVID-19 na mahitaji yao ya kipekee ya kiafya huko maeneo ya ndani zaidi, wako na fursa finyu zaidi kupata huduma bora za afya, matibabu na chanjo. Changamoto nyingine ni kukosa taarifa, teknolojia za kisasa kuboresha kazi zao na maisha yao sambamba na kuendelea na jukumu kubwa la malezi bila ujira wowote.

Maadhimisho haya uangukia katika wiki ambayo Umoja wa Mataifa unaadhimisha Siku ya Chakula Duniani ambayo ni tarehe 16 Oktoba ya kila mwaka  na Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Umaskini tarehe 17 Oktoba. Malengo haya, yaliyounganishwa kila mmoja, yamekuwa kipaumbele cha kimkakati cha ulimwengu na kutiwa saini kwa Ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu (SDGs); Uhakika wa usalama wa chakula, usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake, uzalishaji endelevu wa kilimo na vita dhidi ya umaskini ni mambo muhimu katika malengo n. 17 ya Maendeleo Endelevu yaliyothibitishwa na Ajenda.

Ni kwa kuzingatia hilo, Umoja wa Mataifa unataka uwekezaji maeneo ya vijijini unaojali jinsia na ndiyo maana ya kusisistiza siku hiii kwa  mwaka huu 2020 katika kujenga mstakabali wa wanawake wa vijiini wakati wa  janga la COVID-19 na kuhamasisha juu ya machungu ya wanawake, mahitaji yao na dhima muhimu na ya msingi wanayobeba katika jamii zao. Kwa mfano nchini Sierra Leone, kwa msaada wa mfuko wa maendeleo ya kilimo wa Umoja wa Mataifa, IFAD, mwaka 2013, mwaka mmoja kabla ya Ebola kutikisa taifa hilo, ilianziishwa  benki za vijijini ambazo ziliwezesha wakulima wadogo kuendelea kupata mikopo. Benki hizo zilikuwa wazi na wakulima wanawake kwa wanaume waliweza kukopa fedha wakati wa janga hilo, baada na hata sasa wakati wa janga la COVID-19.  Benki ya jamii iliyoanzishwa na IFAD ikageuka mkombozi kwa kaya zaidi ya 200,000 wakati wa Ebola na hata wakati wa sasa wa janga la COVID-19 kwa kuwa uwezo wao wa kukopa fedha umesaidia kuendeleza biashara zao.

Kwa kutambua changamoto za wanawake wa vijijini ambazo zinaongezeka zaidi hivi sasa za wakati wa COVID-19, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake wa siku hii ya kimataifa   amesema, “kwa pamoja ni lazima tuwekeze kwa wanawake wa vijijini ili wawe na fursa ya huduma ya afya, ulinzi wa kijamii na taarifa kuhusu kilimo. Lazima tupunguze pengo la teknolojia na kuwapatia huduma muhimu ili wakabiliane na kivuli cha janga la ukatili dhidi ya wanawake. Pia tuondoe sheria za kibaguzi za umiliki wa ardhi na urithi na mambo yanayofanya wanawake wa vijijini kuwa hatarini zaidi kupoteza vipato vyao.” Katibu Mkuu amesema katika siku ya leo hebu kila mtu arejelee ahadi yake kwa wanawake wa vijijini kwa kutambua  utofauti wao, “kuongeza jitihada zetu za kuwasaidia wakati huu wa janga la Corona na kufanya nao kazi ili kujenga mnepo dhidi ya majanga yajayo.”

Hata hivyo wanawake wa vijijini, robo ya idadi ya watu wote duniani wanafanya kazi ya kilimo, na wanapata kipato na ni wajasiriamali. Nusu ya asilimia 20 ya wamiliki wa ardhi duniani ni wanawake. Katika maeneo ya vijijini, pengo la ujira kijinsia kati ya mwanamke na mwanaume ni asilimia 40. Kwa kupunguza kiwango cha pengo la ujira duniani kwa asilimia 25 kati ya mwanamke na mwanaume, kunaweza kuongeza pato la ndani la taifa kwa asilimia 3.9 ifikapo mwaka 2025. Iwapo wanawake wa vijijini wanapata sawa na wanaume pembejeo za kilimo, elimu na masoko, uzalishaji kwenye sekta ya kilimo unaweza kuongezeka na idadi ya watu wenye duniani inaweza kupungua kwa kati ya milioni 100 hadi milioni 150.

Ikumbukwe Siku ya Kimataifa ya Wanawake Vijijini ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia Azimio 62/136 la tarehe 18 Desemba 2007, kwa lengo la kutambua jukumu muhimu la wanawake wa vijijini katika kukuza maendeleo ya vijijini na kilimo, kuchangia usalama wa chakula na kutokomeza umaskini vijijini. Wanawake wa vijijini, ambao wengi wao hutegemea maliasili na kilimo kwa maisha yao, wanawakilisha zaidi ya robo ya idadi ya watu duniani. Wao ni wahusika wakuu wa maendeleo endelevu ya uchumi, kijamii na mazingira ya sayari nzima. Katika nchi zinazoendelea, wanawake wa vijijini hufanya karibu asilimia 43 ya nguvu ya wafanyakazi na hutoa chakula kingi kinachopatikana, na hivyo kuchukua jukumu kubwa katika usalama wa chakula. Pamoja na hayo, wengi wao wanaishi bila kuwa na  usalama na wanakabiliwa na ubaguzi mkali na vurugu, ambazo zinasababishwa na athari zinazozalishwa na umaskini, mgogoro wa uchumi, shida ya chakula na mabadiliko ya tabianchi. Wengi wao wananyimwa upatikanaji wa huduma za afya, elimu, udhibiti wa ardhi na michakato ya uamuzi katika kufafanua sera zinazowahusu. Kwa kuongezea, kwa sababu ya umbali mrefu za usafiri  kusafirisha maji na zana za kazi, hali ya maisha ya wanawake vijijini ni mbaya sana, na kusababisha kiwango cha juu cha vifo vya akina mama na watoto wachanga.

15 October 2020, 14:39