Tafuta

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 5 Oktoba inaadhimisha Siku ya Walimu Duniani. Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 5 Oktoba inaadhimisha Siku ya Walimu Duniani. 

Siku ya Walimu Duniani 5 Oktoba 2020: Walimu Wanaongoza!

Maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani kwa Mwaka 2020 yanaongozwa na kauli mbiu: “Walimu: Wanaongoza katika kipeo, kwa kuunganisha na ya mbeleni”. Hii ni fursa makini ya kusherehekea wito wa walimu kurithisha ujuzi, elimu na maarifa kwa vijana wa kizazi kipya. Bila walimu bora, wenye sifa na ujuzi unaotakiwa, si rahisi sana kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 5 Oktoba, inaadhimisha Siku ya Walimu Duniani iliyoanzishwa kunako mwaka 1994, kama sehemu ya kumbukumbu endelevu ya Mapendekezo ya Mwaka 1966 yaliyotolewa na Shirika la Kazi Duniani, ILO, kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, kuhusu: haki na wajibu wa walimu; kiwango chao za elimu, majiundo yao, ajira pamoja na mafunzo kazini. Mapendekezo haya yaliboreshwa tena kunako mwaka 1997 kwa kuwaingiza pia walimu kutoka katika taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu. Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030 ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani. Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora, kwa kuzingatia usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira pamoja na kudumisha amani duniani!

Jumuiya ya Kimataifa katika kutekeleza Lengo la Nne kuhusu Elimu bora, inatambua na kuthamini mchango wa walimu katika mchakato wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030. Maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani kwa Mwaka 2020 yanaongozwa na kauli mbiu: “Walimu: Wanaongoza katika kipeo, kwa kuunganisha na ya mbeleni”. Hii ni fursa makini ya kusherehekea wito wa walimu kurithisha ujuzi, elimu na maarifa kwa vijana wa kizazi kipya. Bila walimu bora, wenye sifa na ujuzi unaotakiwa, si rahisi sana kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu na bila kumwacha mtu awaye yote nyuma! Ni wakati wa kuwekeza zaidi katika usalama, maboresho ya mazingira ya kufundishia pamoja na kujikita katika utekelezaji wa elimu shirikishi. Walimu wamekuwa mstari wa mbele wakati wa janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 lilipopamba moto, shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vilifungwa. Inakadiriwa kwamba, zaidi ya wanafunzi bilioni 1.6 sawa na asilimia 90% ya wanafunzi wote walioandikishwa katika masomo waliathirika.

Walimu milioni 63 wameathirika pia. Mashirika ya Umoja wa Mataifa katika taarifa yao ya pamoja yanasema, kuna haja ya kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu, ili kujibu kwa haraka zaidi vipeo mbalimbali vinavyoweza kujitokeza. Hii ina maana ya kulinda elimu kifedha, kuwekeza zaidi katika ubora wa mafunzo kwa walimu pamoja na kuendeleza nguvu kazi katika sekta ya elimu kwa kutoa mafunzo kazini. Hii ina maana kwamba, walimu wanapaswa kufundishwa elimu ya computer na serikali mbalimbali zianze kuwekeza katika miundombinu ya kidigitali, ili kuwaunganisha wanafunzi mahali popote pale walipo! Hii ni changamoto pevu kwa nchi nyingi duniani. Serikali hazina budi kuhakikisha kwamba, zinawekeza katika ulinzi, usalama na afya ya walimu pamoja na fursa zao za ajira. Haki, wajibu na mafao ya walimu yanapaswa kuboreshwa zaidi, pamoja na kuwahusisha walimu katika kikosi kazi cha kupambana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19.

Katika maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani kwa Mwaka 2020, Jumuiya ya Kimataifa inawashukuru na kuwapongeza walimu kwa mchango wao katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Ni wakati wa kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu, ili kujenga jamii shirikishi hata baada ya janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushirikiana na kushikamana kwa dhati kabisa na walimu ili kuhakikisha kwamba, haki ya wanafunzi kupata elimu bora inatekelezwa. Hata katika kipeo cha Corona, COVID-19, walimu wameendelea kufundisha, kutoa msaada kwa waathirika na sasa shule, taasisi za elimu na vyuo vikuu vimeanza tena kufunguliwa, changamoto ni kuhakikisha kwamba, pengo la elimu lililosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 lina rekebishwa na kusawazishwa. Walimu wanapaswa kushirikishwa kikamilifu ili kuibua mbinu mkakati wa maboresho ya elimu kwa siku za usoni, kwa kuendelea kujikita katika kufundisha kwa weledi!

Elimu Duniani 2020

 

 

05 October 2020, 15:13