Tafuta

Majangwa yanazidi kuongezeka kwa miaka 20 iliyopita Majangwa yanazidi kuongezeka kwa miaka 20 iliyopita 

Ipo gharama kubwa ya binadamu kutokana na majanga kuzidi kiasi!

Katika kuelekea siku ya kudhibiti majanga tarehe 13 Oktoba,Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza madhara ya majanga,(UNDRR)imetoa ripoti ikibainisha kuwa kati ya mwaka 2000 na 2019 kulikuwepo na matukio 7348 ya majanga yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya milioni 1.2 huku wengine bilioni 4.2 maisha yao yakiathiriwa na majanga hayo.Ripoti imepewa jina Gharama ya binadamu kutokana na majanga.

Majanga ya asili yameongezeka mara dufu miaka 20 iliyopita kwa mujibu wa Ripoti  iliyotolewa tarehe 12 Oktoba 2020  mjini Geneva, Uswisi na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza madhara ya majanga, (UNDRR).Ripoti hii inabainisha kwamba kati ya mwaka 2000 na 2019 kulikuwepo na matukio 7348 ya majanga yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya milioni 1.2 huku wengine bilioni 4.2 maisha yao yakiathiriwa na majanga hayo. 

Gharama za majanga hayo ni dola trilioni 2.9 ambapo ofisi hiyo imesema kiwango hicho cha hasara na vifo ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na matukio ya miaka 20 iliyopita ambapo kulikuwepo na matukio 4,212. Tofauti hiyo kubwa imetajwa kusababishwa na ongezeko la majanga yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi. Kwa mfano matukio ya mafuriko kati ya mwaka 1980 na 1999 yalikuwa ni 1389 ikilinganishwa na 3254 kati ya mwaka 2000 na 2019. 

Ripoti iliyopewa  jina, “Gharama ya binadamu kutokana na majanga”, imemulika pia ukame, mioto ya nyika na viwango vya juu zaidi ya joto. Matetemeko pia ya ardhi, tsunami nayo pia vyote vimejumuishwa huku vikitajwa kusababisha vifo zaidi vya binadamu kuliko majanga mengine ya asili. Naye Mami Mizutori Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya upunguzaji wa athari za majanga, amesema, “sisi tunajaribu wenyewe kwa utashi wetu. Hili ni hitimisho ambalo mtu anaweza kusema baada ya kutathmini matukio ya majanga katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Covid-19 ni uthibitisho mpya zaidi  kuwa viongozi wa kisiasa na biashara bado hawajachukua hatua.” 

Akisisitiza zaidi Mizutori amesema iwapo viwango vya juu vya joto vitaendelea kama sasa kwa kipindi cha miaka 20, basi  mustakabali wa binadamu uko mashakani.  Mkuu huyo wa UNDRR amekumbusha kuwa usimamizi bora wa majanga unategemea uongozi wa kisiasa na utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kupitia mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi na mkataba wa Sendai wa kupunguza athari za majanga uliopitishwa miaka mitano iliyopita.  Kwa mujibu wa ripoti hiyo, bara la Asia ndipo lilikumbwa zaidi na majanga ya asili, ikifuatiwa na Amerika na baadaye Afrika. Hata hivyo tukio kubwa zaidi kusababisha vifo vingi ni tsunami kwenye bahari ya Hindi mwaka 2004 ambayo ilisababisha vifo vya watu 226,400.  Ripoti hii imetolewa kuelekea siku ya kudhibiti majanga tarehe 13 Oktoba.

12 October 2020, 16:32