Tafuta

Vatican News
Unicef, na Save the Children katika harakati za kusaidia watoto Unicef, na Save the Children katika harakati za kusaidia watoto  (ANSA)

UNICEF:Janga la covid-19 limeongeza madhara makubwa kwa watoto!

Idadi ya watoto wanaoishi katika umaskini wa namna mbalimbali imeongezeka hadi takriban bilioni 1.2 kutokana na janga la COVID-19. Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na shirika la Save the Children uliochapishwa hii leo mjini New York Marekani na London Uingereza.

Uchambuzi huo umeeleza kuwa  hili ni ongezeko la asilimia 15 ya idadi ya watoto wanaoishi katika hali duni katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, au watoto zaidi ya milioni 150 tangu janga hilo la covid-19 lilipotokea mapema mwaka huu.  Uchambuzi wa umaskini unaotazama pande mbalimbali umetumia takwimu kutoka katika nchi 70 kuhusu ufikiaji wa elimu, afya, nyumba, lishe, usafi na maji. Umebainisha kwamba karibu asilimia 45 ya watoto walinyimwa angalau moja ya mahitaji haya muhimu katika nchi hizo zilizochambuliwa, kabla ya janga la virusi vya corona.  Ingawa uchambuzi tayari umeonesha hali mbaya, UNICEF inaonya kuwa hali hiyo inaweza kuwa mbaya zaidi katika miezi ijayo. Shirika la Save the Children na UNICEF wamejitolea kuendelea kufuatilia hali hii inayoendelea na kushirikiana na serikali na asasi za kiraia kukabiliana nayo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Bi Henrietha Fore anasema, “COVID-19 na hatua za kufunga mipaka zilizowekwa kuzuia kusambaa kwake, vimewasukuma mamilioni ya watoto ndani zaidi katika umaskini. Familia ambazo zilikuwa katika kilele cha kuutoroka umaskini zimerejeshwa nyuma katika umaskini wakati wengine wanakabiliwa na viwango vya uminywaji ambao hawajawahi kuuona hapo awali. Zaidi, tuko karibu na mwanzo wa shida hii kuliko mwisho wake.”

Wakati huo huo Mkuu wa Save the Children Inger Ashing amesema, “Janga hili tayari limesababisha dharura kubwa ya elimu kimataifa katika historia ya ulimwengu na ongezeko katika umaskini litafanya hata kuwa vigumu zaidi kwa watoto wengi walioko katika mazingira hatarishi na familia zao kurejea katika hali nzuri. Watoto ambao watapoteza nafasi ya masomo wana uwezekano mkubwa wa kulazimishwa kuingia katika ajira za utotoni au ndoa za mapema na kuingia katika mtego wa mzunguko wa umaskini katika miaka ijayo. Hatuwezi kumudu kukiacha kizazi chote kuwa waathirika wa janga hili la corona. Serikali za kitaifa na jumuiya ya kimataifa zinatakiwa kuchukua hatua kupunguza makali.” 

Katika ripoti aidha inaeleza kuwa si tu kuwa hivi sasa kuna ongezeko la watoto wengi zaidi wanaokabiliana na umaskini kuliko mwanzo, bali pia hata watoto waliokuwa maskini wanazidi kuwa maskini zaidi. Kwa mujibu wa wao wanasema “Lazima tuchukue hatua sasa kuzuia watoto zaidi wasinyimwe mahitaji ya kimsingi kama shule, dawa, chakula, maji na malazi,” amesema Bi Fore, Mkuu wa UNICEF akiongeza kuwa , “serikali lazima ziwape kipaumbele watoto waliotengwa zaidi na familia zao kupitia upanuzi wa haraka wa mifumo ya ulinzi wa jamii ikiwa ni pamoja na uhamishaji wa pesa na mafao ya watoto, fursa za kujifunza vijijini, huduma za afya na chakula shuleni. Kufanya uwekezaji huu muhimu sasa kunaweza kuzisaidia nchi kujiandaa kwa majanga ya siku za usoni.

18 September 2020, 12:23