Tafuta

Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani, WMO limeratibu taarifa za kisayansi za Mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2020. Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani, WMO limeratibu taarifa za kisayansi za Mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2020. 

UN: Taarifa ya Kisayansi Kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi 2020

Taarifa ya mwaka 2020 imepembua kuhusu: Hali ya kiwango cha Maji duniani, Bahari, Kiwango cha maji yaliyoganda kwenye uso wa dunia, hali halisi ya ardhi duniani, kiwango cha maji ya Bahari pamoja na usafi na usalama wa hali ya hewa duniani. Bwana Antònio Guterres anasema, maeneo yote haya ni muhimu ili kuweza kutoa taarifa kamili ya uelewa wa mabadiliko ya tabianchi kisayansi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa yametoa taarifa ya kisayansi kuhusu mabadiliko ya tabianchi kwa mwaka 2020 “The United in Science 2020 Report” na Karibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana António Guterres kuandika dibaji yake. Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani, WMO, limeratibu taarifa za Mashirika ya: Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, UNESCO-IOC, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP, Global Carbon Project, GCP, Intergorrmental Panel On Climate Change, IPCC. Kila Shirika liliweza kutoa taarifa yake ya kisayansi na zote kwa pamoja zikahaririwa na Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani, WMO. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana António Guterres katika dibaji ya taarifa hii anasema kwamba, janga la homa kali ya mapafu inayosabishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limeleta madhara makubwa katika maisha ya watu sehemu mbalimbali za dunia.

Wakati huo huo, kumekuwepo na ongezeko kubwa la nyuzi joto duniani hali ambayo imepelekea athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi. Majanga ya moto yameongezeka maradufu, kumekuwepo na ongezeko la kina cha bahari, mafuriko na kwa upande mwingine kumekuwepo na ukame wa kutisha. Barafu inaendelea kuyeyuka kwa kasi kubwa kiasi cha kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi. Haya yote yamekuwa ni madhara makubwa kwa watu na mali zao. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la uzalishaji mkubwa wa hewa ya ukaa, hali inayotishia Jumuiya ya Kimataifa kutoweza kufikia lengo lake la kudhibiti ongezeko la nyuzi joto duniani hadi kufikia nyuzi joto 1.5.C., kama njia ya kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya Mkutano wa 21 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 uliofanyika mjini Paris, nchini Ufaransa, kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2015. Kutokana na watu kuwekwa karantini, kumekuwepo na maboresho kwa kiasi fulani katika mazingira nyumba ya wote. Ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19 iwe ni fursa ya kuweza kujikita katika maboresho ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Ili kuweza kufikia lengo hili mahususi, viongozi wa Serikali mbalimbali duniani wanapaswa kujifunga kibwebwe, ili waweze kushirikiana kwa ukaribu zaidi na wanasayansi, ili kuibua sera na mikakati endelevu na hatimaye, waweze kufanya maamuzi magumu katika maisha yao, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo. Taarifa ya kisayansi kuhusu mabadiliko ya tabianchi huchapishwa mara moja kwa mwaka, kwa kuonesha maboresho yaliyofanyika katika kipindi cha mwaka mmoja. Kwa mara ya kwanza taarifa hii ilitolewa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa uliofanyika kunako mwaka 2019. Taarifa hii inachapishwa ili kuonesha mwenendo wa mabadiliko ya tabianchi duniani kwa mwaka 2020. Taarifa hii imapembua kwa kina na mapana kuhusu: hali ya kiwango cha Maji duniani, Bahari, Kiwango cha maji yaliyoganda kwenye uso wa dunia kama inavyojulikana kitaalam “Cryosphere”, hali halisi ya ardhi duniani, kiwango cha maji ya Bahari pamoja na usafi na usalama wa hali ya hewa duniani.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana António Guterres anasema, maeneo yote haya ni muhimu ili kuweza kutoa taarifa kamili ya uelewa wa mabadiliko ya tabianchi kisayansi. Jumuiya ya Kimataifa inahitaji sayansi na mshikamano wa dhati, ili kupambana na changamoto mamboleo za ugonjwa wa Virusi vya COVID-19 pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ni matumaini ya Bwana António Guterres kwamba, Serikali na viongozi mbalimbali wa Jumuiya ya Kimataifa wataweza kutumia tafiti hizi za kisayansi, ili kuweza kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, ili kujenga mazingira salama sanjari na kuendelea kujikita katika maendeleo fungamani ya binadamu kwa ajili ya mafao ya wengi.

Un Mazingira
11 September 2020, 14:42