Tafuta

Vatican News
Siku ya Bahari Duniani Inaadhimishwa Kila Mwaka Mwishoni mwa Mwezi Septemba na kwa mwaka huu inaadhimishwa tarehe 24 Septemba 2020: Maendeleo endelevu kwa ajili ya sayari dunia. Siku ya Bahari Duniani Inaadhimishwa Kila Mwaka Mwishoni mwa Mwezi Septemba na kwa mwaka huu inaadhimishwa tarehe 24 Septemba 2020: Maendeleo endelevu kwa ajili ya sayari dunia. 

Siku Ya Bahari Duniani 2020: Usafiri Endelevu Baharini

Bwana Kitack Lim Katibu mkuu wa Shirika la Bahari Duniani, IMO, katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani tarehe 24 Septemba 2020 inayoongozwa na kauli mbiu “maendeleo fungamani kwa ajili ya maendeleo fungamani ya sayari dunia anasema janga la Virusi vya COVID-19 limesababisha athari kubwa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 6 Machi 1948  huko Geneva nchini Uswiss katika mkutano ulioitishwa na Umoja wa Mataifa ulipopitisha Mkataba wa Kimataifa wa kuanzisha Shirika la Bahari Duniani. Na tarehe 17 Machi 1958, lilianza kutekeleza dhamana na wajibu wake. Shirika hili limekuwa likijelekeza zaidi katika mambo yafuatayo: Kutoa utaratibu wa ushirikiano katika nyanja ya udhibiti wa vitendo vya kiharamia; Ushirikiano wa masuala ya kiufundi yanayoathiri usafiri wa biashara wa kimataifa. Kuhimiza na kuhamasisha kiwango cha juu katika usalama baharini, utunzaji wa mazingira na ufanisi katika usafiri wa majini. Kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazohusiana na malengo ya kuanzishwa kwa Shirika hili. Kwa mara ya kwanza katika historia, Siku ya Bahari Duniani, iliadhimishwa kunako mwaka 1978 kama kumbukumbu ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Bahari Duniani, IMO (International Maritime Organization, IMO), kunako mwaka 1958. Maadhimisho haya yanalenga kuragibisha umuhimu wa usafirishaji wa abiria na mizigo; usalama wa mabaharia na bidhaa sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Binadamu Ifikapo mwaka 2030.

Bwana Kitack Lim Katibu mkuu wa Shirika la Bahari Duniani, IMO, katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani tarehe 24 Septemba 2020 inayoongozwa na kauli mbiu “maendeleo fungamani kwa ajili ya maendeleo fungamani ya sayari dunia anasema kwamba,  janga la Virusi vya Corona, COVID-19 limesababisha athari kubwa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Shirika la Bahari Duniani limejitahidi kukabiliana na changamoto ambazo zimekua na athari kubwa hasa katika suala zima la usafiri baharini, ulinzi na usalama wa mabaharia, ili kuwawezesha kufikisha bidhaa na huduma kwa walengwa, ili kukabiliana na changamoto za Virusi vya Corona, COVID-19. Jumuiya ya Kimataifa inategemea asilimia 80% ya usafiri wa bahari kwa ajili ya biashara ya kitaifa na kimataifa na kama kikolezo muhimu sana cha ukuaji wa uchumi. Usafiri wa bahari unatarajiwa kuwa ni nguzo muhimu katika mchakato wa kufufua na hatimaye, kuimarisha uchumi kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu.

Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030 ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani. Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora, kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira pamoja na kudumisha amani duniani! IMO inasema, malengo haya yanaweza kufikiwa ikiwa kama kutakuwepo na uhakika na usalama wa usafiri baharini, kwa kuzingatia usalama, afya bora pamoja na kuzingatia baianuai (biodiversity) ya bahari.

Ili kufikia malengo haya adhimu, IMO inalenga kuendelea kusimama kidete kulinda usalama wa meli na mabaharia sanjari na kuingiza mfumo wa kidigitali; kwa kukazia weledi, ujuzi na maarifa pamoja na uboreshaji wa mazingira ya kazi. IMO inapania kulinda na kutunza mazingira, kuendelea kushirikiana na mamlaka za bandari duniani pamoja na kukuza ushirikiano wa kiufundi,  ili kuzijengea nchi changa zaidi duniani uwezo wa kukabiliana na changamoto mamboleo mintarafu usafiri baharini. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na mchakato wa kudumisha usawa wa kijinsia katika Jumuiya ya Mabaharia. IMO, itaendelea kujizatiti katika kudumisha usalama baharini pamoja na kulinda mazingira ya bahari. Jumuiya ya Kimataifa inawajibika kuhakikisha kwamba, juhudi zote hizi zinafanikiwa, ili Malengo ya Maendeleo ya Kimataifa yaweze kufikiwa.

Bwana Kitack Lim Katibu mkuu wa Shirika la Bahari Duniani, IMO, katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani kwa Mwaka 2020 anaendelea kusema kwamba, janga la Virusi vya Corona, COVID-19 limesababisha madhara makubwa, lakini pia kumekuwepo na umoja, mshikamano na ushirikiano katika ulimwengu wa Mabaharia pamoja na wadau mbalimbali. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza zaidi katika sera za umoja, ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, kwa kuunga mkono juhudi za usafri baharini na mabaharia, ili hatimaye, sekta hii nyeti iweze kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara!

Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba zake mbalimbali mintarafu utunzaji Bora wa mazingira nyumba ya woye, anasema, Jumuiya ya Kimataifa ina haki na wajibu wa kutumia na kutunza bahari, maziwa na vyanzo mbali mbali vya maji kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu. Kanuni ya pili ni ekolojia fungamani ya maendeleo ya binadamu inayogusa medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu kama vile: masuala ya kiuchumi, ekolojia ya kijamii, ekolojia ya kitamaduni na  ekolojia ya maisha ya kila siku inayoongozwa na kanuni ya ustawi, mafao ya wengi na haki kati ya vizazi mbali mbali. Kumbe, uchafuzi wa mazingira una athari kubwa katika maisha ya binadamu na maendeleo yake. Haki jamii ni kati ya masuala tete yanayopaswa kuingizwa katika majadiliano ya juu ya utunzaji bora wa mazingira ili kuweza kusikiliza kilio cha Dunia Mama pamoja na kilio cha maskini duniani. Sera na mikakati hii ilenge pia kuboresha hali ya maisha ya wavuvi baharini pamoja na familia zao, sanjari na kuboresha mazingira ya kazi na haki zao msingi.

Changamoto na matatizo mbali mbali yanayojitokeza katika uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote yanapaswa kushughulikiwa kwa pamoja kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema; katika umoja na mshikamano kwa kuwaambata na kuwakumbatia watu wote. Kanuni ya nne ni elimu ya utunzaji bora wa mazingira inayopaswa kumwilishwa katika malezi na makuzi ya watoto hadi watu wazima. Elimu ya utunzaji bora wa mazingira ni muhimu sana kwa vijana wa kizazi kipya. Kanuni ya tano inakita ujumbe wake kwa kuwataka watu wa Mungu kuhakikisha kwamba, wanajadiliana na kushirikisha mamuzi na utekelezaji wake katika ngazi mbali mbali. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na tafuiti makini ili ziweze kufanyiwa kazi. Kuhusu utunzaji bora wa mazingira, jambo la msingi ni ushirikiano na wala hakuna sababu za malumbano yasiyokuwa na tija wala mvuto, kwa sababu athari za mabadiliko ya tabianchi hazibagui wala hazichagui, wote wanaathirika, lakini maskini wanaathirika zaidi.

Siku ya Bahari Duniani

 

24 September 2020, 15:22