Tafuta

Vatican News
Jumuiya ya Kimataifa mwaka 2020 inaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 75 tangu Miji ya Hiroshima na Nagasaki iliposhambuliwa kwa mabomu ya atomiki. Changamoto na kutokomeza silaha za nyuklia duniani. Jumuiya ya Kimataifa mwaka 2020 inaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 75 tangu Miji ya Hiroshima na Nagasaki iliposhambuliwa kwa mabomu ya atomiki. Changamoto na kutokomeza silaha za nyuklia duniani.  (©kae4b - stock.adobe.com)

UN: Miaka 75 ya Mashambulizi ya Atomiki Hiroshima na Nagasaki

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anabainisha kwamba, miaka 75 iliiyopita, silaha moja ya nyuklia ilisababisha maafa makubwa kwa watu na madhara yake bado yanaendelea kuonekana hadi leo hii. Miji ya Hiroshima na Nagasaki iwe ni kielelezo cha matumaini mapya, majadiliano na maridhiano ili dunia iweze kuwa huru pasi na vistisho vya mahangamizi ya silaha za nyuklia. Amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Imekwisha gota miaka 75 tangu Marekani idondoshe bomu la atomiki mjini Hiroshima nchini Japan, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema njia pekee ya kuondokana na tishio la nyuklia ni kutokomeza silaha za nyuklia. Katika ujumbe wake kwa maadhimisho hay alioutoa huko Hiroshima nchini Japan kwa njia ya video, Katibu Mkuu amesema amezingatia ukweli kwamba miaka 75 iliyopita, silaha moja ya nyuklia ilisababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao na madhara yake bado yanaendelea kuonekana hadi leo hii. Miji ya Hiroshima na Nagasaki iwe ni kielelezo cha matumaini mapya, majadiliano na maridhiano ili dunia iweze kuwa huru pasi na vistisho vya mahangamizi ya silaha za nyuklia.

Wahanga wa mashambulizi ya silaha za nyuklia nchini Japan, “Hibakusha”, ni kielelezo na ushuhuda wa watu wanaotaka ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kuona kwamba, dunia inakuwa huru dhidi ya vitisho vya mashambulizi ya kinyuklia. Katibu Mkuu amekumbusha kwamba, tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1945, Umoja wa Mataifa ulianza kujizatiti katika mchakato wa kutokomeza silaha za nyuklia duniani kwani ni katika kipindi hiki miji ya Hiroshima na Nagasaki ilikuwa imeshambuliwa kwa mabomu ya Nyuklia na athari zake kuonekana bayana. Inasikitisha kuona kwamba, katika kipindi cha Miaka 75 iliyopita, Jumuiya ya Kimataifa imeshindwa kufikia maamuzi mazito ya kusitisha utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha za nyuklia, kwani madhara yake ni makubwa sana kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Vita baridi inayoendelea kati ya mataifa inaochochea mashindano ya utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha za nyuklia duniani, mambo yanayotishia mustakabali wa amani na maendeleo kwa Jumuiya ya Kimataifa. Katibu Mkuu amesema kuwa nchi zinazomiliki silaha za nyuklia zinazidi kuimarisha makombora yao na hatari ya nyuklia kutumiwa kwa makusudi au kwa bahati mbaya ni kubwa kwa mienendo hiyo kuendelea. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa Jumuiya ya KImataifa kurejea katika majadiliano yanayosimikwa katika misingi ya ukweli na uwazi, ili kuweza kufikia muafaka wa kusitisha mchakato wa kutengeneza na kulimbikiza silaha za nyuklia.

Nchi zinazomiliki silaha za nyuklia zina wajibu wa kipekee, kila mara zimejizatiti kutokomeza silaha za nyuklia lakini bila ya mafanikio yanayotarajiwa. Sasa ni wakati wa mazungumzo, kuweka mikakati ya kujengeana imani, kupunguza ukubwa wa silaha zao za nyuklia na zaidi ya yote kujizuia kuzitumia. Ametaka pia kulinda na kudumisha mifumo ya kimataifa ya kuendeleza matumizi bora ya nishati ya nyuklia akisema kuwa mwaka 2021 serikali zitakuwa na fursa hiyo wakati wa mkutano wa mapitio ya mkataba wa kuzuia kuenea kwa silaha nyuklia. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekumbusha kwamba kila mtu analo jukumu katika kutokomeza silaha za nyuklia akisema, vijana na mashirika ya kiraia wamethibitisha nguvu yao mara kwa mara, katika kuunga mkono juhudi za Jumuiya ya Kimataifa kutokomeza silaha za nyuklia. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kusikiliza mawazo ya watu mbali mbali na kuwapatia fursa ili sauti zao zisikike. Umoja wa Mataifa utaendelea kufanya kazi na wale wote wanaotaka kusimama kidete ili kufanikisha lengo moja la Jumuiya ya Kimataifa la kuwa na dunia bila silaha za nyuklia.

Umoja wa Mataifa 75

 

10 August 2020, 07:22