Tafuta

Rais wa Mali  Ibrahim Boubacar Keita akiambatana na Rais wa Niger Mahamadou Issoufou huko Bamako Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita akiambatana na Rais wa Niger Mahamadou Issoufou huko Bamako 

ULIMWENGU:Rais wa Mali kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita ametangaza kuanzisha mchakato wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong amesema hakutakuwa tena na vita kwa sababu silaha zake za nyuklia zitahakikisha ulinzi na hatma ya taifa hilo.Maambukizi mapya ya COVID-19 yarekodiwa nchini China.Miji imeonekana kuwa kitovu cha janga la virusi vya corona.

Na Sr. Angela Rwezaula-Vatican

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita ametangaza kuanzisha mchakato wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa katika nchi hiyo inayoandamwa na machafuko baada ya kupata shinikizo kutoka viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi. Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Mali imesema ili kukidhi matakwa ya jumuiya ya kikanda ya ECOWAS, rais Keita ameamua kuunda ujumbe wa mawaziri wachache watakaopewa jukumu la kufanya majadiliano na upande wa upinzani kwa lengo kuunda serikali ya pamoja. Waandamanaji wamekuwa mitaani kwa wiki kadhaa sasa kushinikiza kujiuzulu kwa rais Keita ambaye uongozi wake unaandamwa na kitisho cha makundi ya itakadi kali na uchumi unaodorora kabisa. Hapo kabla viongozi wakuu wa nchi 15 za jumuiya ya maendeleo ya nchi za magharibi ya Afrika, ECOWAS, walisema wanamuunga mkono rais Keita lakini wakatoa wito wa kuundwa serikali ya pamoja itakayojumuisha upande wa upinzani.

Korea-Kim: Silaha za nyuklia zitazuia vita nyingine

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amesema hakutakuwa tena na vita kwa sababu silaha zake za nyuklia zitahakikisha ulinzi na hatma ya taifa hilo licha ya mbinyo na vitisho vya kijeshi kutoka nje. Kim ametoa matamshi hayo wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 67 tangu kumalizika kwa vita ya Korea ya mwaka 1950 hadi 1953 zililofanyika jana kwa halfa maalum iliyowajumuisha maveterani. Kiongozi huyo amesema hivi sasa Korea Kaskazini inao uwezo wa kujilinda dhidi ya vitisho vya kigeni na kwamba silaha za nyuklia zilizopo zitaweka kizingiti cha kuzuka mzozo mwingine wa kijeshi. Hotuba ya Kim imetolewa katika wakati ambapo mazungumzo na Marekani juu ya kuuongokoa mfumo wake wa nyuklia na miradi mingine ya makombora ya masafa marefu yamekwama licha ya ahadi ya kuondolewa vikwazo vya kiuchumi.

Maambukizi mapya 68 ya COVID-19 yarekodiwa nchini China

Maafisa wa afya nchini China wametangaza leo kuwa wamerikodi visa vipya 68 vya virusi vya corona ambavyo 64 kati yake ni maambukizi ya ndani ya nchi hiyo. Takwimu mpya kutoka tume ya afya ya taifa imeonesha jimbo la magharibi ya China la Xinjiang, ambalo limekuwa kitovu cha mripuko wa virusi wa hivi karibuni limeshuhudia maambukizi mapya 57. Katika jimbo lingine la kaskazini mashariki la Lianoning ambako visa kadhaa ya maambukizi vilizuka kwenye kiwanda cha vyakula vya baharini katika mji wa Dalian kumeripotiwa maambukizi mapya sita. Mamia ya safari za ndege za ndege kwenda na kutoka mji wa Dalian zilifutwa jana Jumatatu kwa lengo la kuzuia kusambaa kwa virusi. Miji ya Shanghai, Beijing na Yunnan imerikodi maambukzii ya virusi vya corona ambayo sehemu kubwa ya watu kutoka nje ya China.

Miji ni kitovu cha COVID-19 kwa kuwa asilimia ya wagonjwa wote wa janga wamethibitika humo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kupitia ujumbe wake wa uzinduzi wa tamko la kisera kuhusu janga la virusi vya corona katika miji, tarehe 28 Julai 2020 ametoa wito kwa viongozi wote  duniani kufikiria upya na kurekebisha miji katika kipindi hiki ambacho dunia inapona kutokana na janga la COVID-19 kwani miji imeonekana kuwa kitovu cha janga hilo. Miji ni kitovu cha COVID-19 kwa kuwa asilimia ya wagonjwa wote wa janga wamethibitika kuwa wa mijini ameeleza hayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Gueterres. Katibu Mkuu Guterres amesema miji imejaa shida, mingi ikiwa na mifumo ya afya iliyoelemewa, huduma duni za maji na usafi pamoja na changamoto nyingine,“hii iko hususani katika maeneo maskini ambapo hali hii imefunua ukosefu wa usawa uliokita mizizi.”

Usawa katika jamii

Pamoja na hayo, Bwana Guterres ameeleza kuwa kwa upande mwingine, miji pia ni maeneo ambayo yameonesha mshikamano wa ajabu na ushujaa akisema kuwa dunia imeshuhudia, “watu wasiofahamiana wakisaidiana, mitaa ikiwashangilia kwa kuwaunga mkono wafanyakazi muhimu, wafanyabiashara wakitoa misaada ya kuokoa maisha.”  Katibu Mkuu Guterres pia amesema tunapopambana na janga hili la COVID-19 na kuelekea katika kupona, miji inapaswa kuangaliwa kama kitovu cha jamii, uvumbuzi wa mwanadamu na ustadi.  Bwana Guterres ametoa mapendekezo matatu likiwemo mosi kuhakikisha awamu zote za mapambano dhidi ya COVID-19 yanapambana pia na kukosekana kwa usawa katika jamii kwa kuwapa kipaumbele wale walioko hatarini ikiwemo kuwahakikishia malazi, pili kuimarisha uwezo wa serikali za mitaa na tatu kutafuta uchumi wa kijani, imara na jumuishi.

28 July 2020, 14:00