Tafuta

Serikali ya Tanzania inapania kufufua vyuo na vituo vya utafiti wa kilimo sanjari na kuendelea kuimarisha usafiri wa majini ili kuboresha zaidi mchakato wa usafirishaji wa bidhaa na abiria. Serikali ya Tanzania inapania kufufua vyuo na vituo vya utafiti wa kilimo sanjari na kuendelea kuimarisha usafiri wa majini ili kuboresha zaidi mchakato wa usafirishaji wa bidhaa na abiria. 

Tanzania Kuimarisha Usafiri wa Majini na Vituo vya Utafiti wa Kilimo

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema: Malengo ya Serikali ya Tanzania ni kuruhusu mataifa ya nje yafanye biashara na Tanzania na kuruhusu Watanzania wasafiri kwenda hukohuko kuona na kujifunza ili warudi nchini mwao na taaluma mpya. Utaratibu huo pia utawezesha kutengeneza mzunguko mzuri wa kifedha kwa wananchi. Tanzania itafufua pia vituo vya utafiti wa kilimo!

Na Ofisi ya Waziri Mkuu – Mtwara, Tanzania.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema malengo ya Serikali ni kuimarisha usafiri kwenye maziwa yote na bahari ili kuwawezesha Watanzania wafanye biashara na mataifa ya nje. “Malengo yetu ni kuruhusu mataifa ya nje yafanye biashara na Tanzania na kuruhusu Watanzania wasafiri kwenda hukohuko kuona na kujifunza ili warudi hapa na taaluma mpya. Utaratibu huo pia utawezesha kutengeneza mzunguko mzuri wa kifedha kwa wananchi,” amesema. Akizungumza na wananchi katika viwanja vya Klabu ya Bandari mjini Mtwara Jumanne, Julai 7, 2020) Waziri Mkuu amesema kabla ya kukagua ujenzi wa gati namba 2 katika bandari ya Mtwara juzi alitembelea miradi ya ujenzi wa bandari za Karema (Katavi), Kabwe na Kasanga (Rukwa) katika mwambao wa Ziwa Tanganyika. “Nimetoka Ziwa Tanganyika ambako tunapakana na Burundi, Rwanda, Zambia na Congo DRC na Serikali kwenye mkakati huu tumeingiza fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa bandari zetu. Tumeimarisha bandari ya Kigoma pale Kibirizi, kazi imekamilika na sasa tunajenga eneo la kuweka makontena.”

Amesema katika Ziwa Victoria kuna meli iliyokuwa inakarabatiwa “New MV Victoria” na imeanza majaribio ya kwenda Kagera na nyingine inaendelea kujengwa ili kuruhusu wafanyabiashara wa Kanda ya Ziwa wafanye biashara zao kwa urahisi. Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka vijana wanaopata ajira kwenye miradi mikubwa inayogharimiwa na Serikali watumie fursa hiyo kupata utaalamu utakaowawezesha kuajiriwa maeneo mengine hata baada ya miradi ya sasa kukamilika Akizungumza na vijana wa Kitanzania wanaofanya kazi kwenye mradi wa gati jipya katika bandari ya Mtwara, Waziri Mkuu amewataka vijana wote wanaofanya kazi kwenye miradi mbalimbali nchini hasa ile mikubwa na ya kimkakati wawe waaminifu ili kujenga taswira nzuri ya nguvukazi ya vijana wa Kitanzania wanapohitaji kuajiriwa hasa na makampuni ya nje ya nchi. “Kuweni mabalozi wazuri wa vijana wenzenu kwa kufanya kazi kwa bidii na uaminifu wa hali ya juu ili mkimaliza miradi ya sasa, mpate ajira tena kwenye miradi mingine. Bado Serikali yetu inakusudia kuanzisha miradi mingine mingi na matarajio ni kuwa vijana wa Kitanzania watanufaika kwa kupata ajira katika miradi hiyo.”

Awali, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Mhandisi Juma Kijavara alimweleza Waziri Mkuu kuwa kazi ya ujenzi wa gati namba 2 katika bandari ya Mtwara unafanywa na kampuni ya MS China Railway Construction Enginereering Group Company Limited (CRMBEG) kwa gharama ya sh. 157,801,598,519.92.00. Amesema ujenzi wa mradi huo ulianza rasmi Mei 27, 2017 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Julai, 2020 ukisimamiwa na Mhandisi Mwelekezi, Inros Lackner kutoka Ujerumani. Mhandisi Kijavara alisema kuwa mradi huo umefikia asilimia 75 ya utekelezaji wake na jumla ya sh. bilioni 74.84 zimelipwa kwa mkandarasi sawa na asilimia 48. Akizungumzia ushiriki wa wazawa katika ujenzi wa mradi huo, Mhandisi Kijava alisema kuwa mkandarasi huyo ameajiri wazawa 308 sawa na asilimia 87.5 ya wafanyakazi wote. Alisema wafanyakazi hao wameajiriwa katika kada mbalimbali. Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu alifuatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Kapteni Mstaafu, George Mkuchika, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa na baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Mtwara.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli itahakikisha kwamba vyuo na vituo vyote vya utafiti wa kilimo nchini vinafufuliwa, hivyo Wizara ya Kilimo inatakiwa kutenga fedha za kutosha katika bajeti yake kila mwaka. “Nataka niwahakikishie Serikali yenu imedhamiria kuimarisha kilimo pamoja na utafiti wake. Mwezi mmoja uliopita nilikuwa Mlingano mkoani Tanga kuona shughuli za utafiti wa zao la mkonge lakini miezi miwili iliyopita nilikuwa kwenye chuo kipya tulichokianzisha kule Kigoma cha utafiti cha Kihinga na nimeona kazi yake na tutapata mafanikio makubwa.” Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo Julai 07, 2020 alipotembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele iliyoko mkoani Mtwara kwa lengo la kujionea shughuli za utafiti wa mazao mbalimbali ya kilimo zinazoendelea kituoni hapo. Alisema Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefurahishwa na kazi nzuri za utafiti wa mazao mbalimbali zinazofanywa na vituo vya utafiti na matokeo mazuri ya utafiti huo kwa wakulima wa Watanzania.

Waziri Mkuu alisema “Azma ya kusimamia na kuona vyuo vya utafiti vinafanya kazi yake vizuri ni pamoja na maboresho haya kwanza wizara husika lazima itambue kuwa vyuo vya utafiti vinamchango mkubwa, wizara kwenye bajeti zake ipeleke fedha nyingi kwenye utafiti na tuone utafiti unagundua mambo na yale yanayogunduliwa yaende yakafanyiwe kazi.” Vilevile, Waziri Mkuu alisema idadi ya udahili wa wanafunzi katika vyuo vya kilimo itaongezwa ili wapatikane wataalamu na watafiti wengi ambao wanahitajika sana katika kufanikisha mapinduzi ya kilimo nchini. Taasisi ya hiyo ya Kilimo ya Naliendele ni miongoni mwa vituo vya utafiti wa kilimo nchini ambavyo vimewawezesha wakulima wengi kujiongezea tija na kujikwamua kiuchumi baada ya kutumia mbegu bora zinazozalishwa kituoni hapo kama za korosho, ufuta na muhogo.

09 July 2020, 09:03