Tafuta

Umoja wa Mataifa unatafuta dola bilioni 3.6 za ziada kwa ajili ya Mpango wake wa Masuala ya Kibinaadamu Ulimwenguni ili kupambana na janga virusi vya corona Umoja wa Mataifa unatafuta dola bilioni 3.6 za ziada kwa ajili ya Mpango wake wa Masuala ya Kibinaadamu Ulimwenguni ili kupambana na janga virusi vya corona 

Umoja wa Mataifa unatafuta dola bilioni 3,6 zaidi kupambana na Covid-19!

Umoja wa Mataifa watoa onyo kwa nchi zilizoendelea kuwa zitajuta ikiwa hawatawapatia msaada nchi maskini na wakati huo huo Umoja huo huko katika harakati za kutafuta dola bilioni 3.6 zaidi kwa ajili ya masuala yake ya kibinamu hasa katika kupambana na janga la Covid-19.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Umoja wa Mataifa unatafuta dola bilioni 3.6 za ziada kwa ajili ya Mpango wake wa Masuala ya Kibinaadamu Ulimwenguni ili kupambana na janga la COVID-19. Na wakati huo huo imeonya nchi zilizoendelea kuwa zitajuta kwa kutochukua hatua kama mataifa maskini hayatapata msaada. Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Bwana Mark Lowcock amewaambia waandishi wa habari kuwa kuna kitisho kikubwa cha kutokea njaa kubwa baadaye mwaka huu na mapema mwaka ujao kwa hivyo ni bora kuwekeza na kuzuia hilo. Mbali na Somalia, Sudan Kusini, Yemen na Nigeria, ambazo tayari zimekumbwa na uhaba wa chakula, alielezea wasiwasi unaoongezeka kuhusu Sudan, Zimbabwe na Haiti. Pamoja na kupambana na baa la njaa linaloongezeka kutokana na mgogoro wa kiuchumi unaosababishwa na janga la corona, fedha za ziada zitatumika katika ununuzi wa vifaa vya matibabu, kufanya kampeni za habari na operesheni za angani za kusambaza misaada ya kibinadamu Afrika, Asia na Amerika Kusini.

Mikakati ya kimataifa kukabiliana na covid-19

Mwanzoni mwa mwaka huu taarifa hiyo imesema wahudumu wa misaada ya kibinadamu waliwalenga watu milioni 110 lakini kwa taarifa iliyotolewa tarehe 17 Julai 2020  wanahitakji kuwafikia watu milioni 250 na msaada wa kibinadamu katika nchi 63.  Watu wengi zaidi wamejikuta katika hali mbaya na wanahitaji msaada wakiwemo watu masikini mijini, wanawake wasiojiweza na wasichana ambao wako hatarini kutokana na ukatili wa kijinsia, watu wenye ulemavu na matatizo ya afya ya akili, wazee, watu wenye njaa, watoto na vijana barubaru.

Umuhimu wa msaada wa fedha

Kwa mujibu wa OCHA mwezi Machi mwaka huu lilizinduliwa ombi la kimataifa kwa ajili ya hatua za kibinadamu za kupambana na COVID-19 ambapo dola bilioni 2 ziliombwa. Lakini kutokana na ongezeko la mahitaji mwezi Mei ombi hilo liliongezeka na kufikia dola bilioni 6.7 na baada ya kuendelea kutathimini mahitaji na ongezeko la idadi ya watu wanaohitaji msaada sasa ombi hilo limeongezeka na kufikia dola bilioni 10.3 Mashirika ya Umoja wa Mataifa  yamesema mipango ya ombi hili jipya ni ya kushughulikia  mahitaji ya msingi ya huduma za afya ikiwemo kujumuisha chanjo, huduma ya mama na mtoto  na mengineyo. Lakini yamesema asilimia kubwa ya fedha hizo zitaelekezwa katika msaada ambao si wa afya hususani katika uhakika wa chakula, maji na usafi, kujikimu kimaisha, malazi na ulinzi ambao pia unajumuisha dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Kuna ongezeko la watu wenye njaa

Kwa mujibu wa taarifa ya mashirika hayo hivi sasa linashuhudiwa ongezeko kubwa la watu wanaokabiliwa na njaa duniani ambao idadi yao inaweza kufikia milioni 270 ifikapo mwisho wa mwaka huu. Hivyo ombi hilo la leo linajumuisha dola milioni 500 za kuzuia baa la njaa. Tangu kutolewa kwa ombi la kwanza la fedha OCHA inasema kufikia sasa ni dola bilioni 1.7 pekee zilizokwisha kusanywa ambazo hazitoshi hata kufikia mahitaji ya ombi la awali la dola bilioni 2 lililotolewa mwezi Machi. Hata hivyo taarifa yao inatambua kwamba nchi zote zinaathirika kiuchumi na wahisani kwa ujumla wamejitolea zaidi katika kukabiliana na masuala ya kibinadamu kwenye nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2020 kuliko walivyofanya miaka ya nyuma ambapo mpaka sasa wameshatoa jumla ya dola bilioni 8.8 kwa ajili ya kukabiliana na masuala ya kibinadamu na COVID-19.

Nchi tajiri zinalinda uchumi zake na watu wake kwa misaada bila kuwekeza

Taarifa yao imesisitiza kuwa katika  kuchukulia hali halisi  kama mazoea katika mazingira haya itakuwa ni hatari kubwa . Nchi tajiri zinalinda chumi wake na watu wake kwa misaada ya kuwapunguzia athari  lakini ni hatari kutowekeza katika kuwalinda walio hatarini zaidi duniani pia. Na isipofanyika hivyo basi taarifa imeonya kwamba kuna hatari ya kuwa na majanga mapya yaliyochochewa na COVID-19. Vile vile wamesisitiza kuwa hakuna mtu katika dunia hii ambaye atakuwa salama dhidi ya virusi vya COVID-19 mpaka pale ambapo kila mtu atakuwa salama hivyo wametoa wito kwa dunia kuwa wakarimu siyo tu kwa sababu ni jambo la kiutu kufanya lakini ni kwa sababu ni suala la maslahi yao wote.

18 July 2020, 14:07