Tafuta

Vatican News
Tamko Kuhusu Hija ya Rais Donald Trump kwenye Madhabahu ya Mtakatifu Yohane Paulo II Kitaifa nchini Marekani: Kila Mtu anayo haki ya kutembelea mahali hapa pasi na ubaguzi! Tamko Kuhusu Hija ya Rais Donald Trump kwenye Madhabahu ya Mtakatifu Yohane Paulo II Kitaifa nchini Marekani: Kila Mtu anayo haki ya kutembelea mahali hapa pasi na ubaguzi!  (AFP or licensors)

Tamko Kuhusu Rais Trump kwenye Madhabahu ya Yohane Paulo II!

Lengo la hija hii kwa Rais Trump, lilikuwa ni kuweka sahihi kwenye Hati inayohusu Uhuru wa Kidini Kimataifa. Hapa ni mahali muafaka kwa kuzingatia kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni kiongozi aliyejipambanua kwa kusimamia haki msingi za binadamu, utu, heshima na uhuru wa kuabudu. Haya ni mambo msingi yalijionesha wakati wa uongozi wa Mtakatifu Yohane Paulo II.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rais Donald Trump wa Marekani pamoja na mkewe, Jumanne, tarehe 2 Juni 2020 amefanya hija ya kiroho kwenye Madhabahu ya Mtakatifu Yohane Paulo II Kitaifa yaliyoko Jimbo kuu la Washington DC., nchini Marekani yaliyoanzishwa kunako mwaka 2014. Hapa pamekuwa ni mahali pa sala na tafakari ya kina; mahali pa maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na mahali pa kuwakutanisha watu wa dini na madhehebu mbali mbali wanaotaka kujichotea utajiri na urithi mkubwa wa tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu kutoka kwa Mtakatifu Yohane Paulo II. Hija ya Rais Donald Trump kwenye Madhabahu haya wakati, Marekani imegubikwa na machafuko ya kijamii, imezua kinzani kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Kanisa na watu wa Mungu nchini Marekani katika ujumla wao. Ni katika muktadha huu, Madhabahu ya Mtakatifu Yohane Paulo II Kitaifa nchini Marekani yametoa tamko kuhusu hija hii iliyofanywa na Rais Trump kwa kusema kwamba, hija hii ilikuwa imepangwa mapema na Ikulu la Marekani hata kabla ya kuibuka kwa machafuko ya kijamii ambayo yamesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Lengo la hija hii kwa Rais Trump, lilikuwa ni kuweka sahihi kwenye Hati inayohusu Uhuru wa Kidini Kimataifa. Hapa ni mahali muafaka kwa kuzingatia kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni kiongozi aliyejipambanua kwa kusimamia haki msingi za binadamu, utu, heshima na uhuru wa kuabudu. Haya ni mambo msingi yalijionesha wakati wa uongozi wa Mtakatifu Yohane Paulo II kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Rais Trump anataka kuunga mkono jitihada za kukuza na kudumisha uhuru wa kidini ili kuondokana na nyanyaso na dhuluma wanazofanyiwa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Ikumbukwe kwamba, Madhabahu ya Mtakatifu Yohane Paulo II Kitaifa ni mahali pa sala na majiundo endelevu kwa watu wote wanaopenda kujichotea amana na utajiri kutoka kwa Mtakatifu Yohane Paulo II.

Tamko Kuhusu Rais Trump
03 June 2020, 13:58