Tafuta

Tarehe 5 Juni ni Siku ya Mazingira duniani.Shughuli za mwanadamu zinachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu na uchafuzi wa mazingira. Tarehe 5 Juni ni Siku ya Mazingira duniani.Shughuli za mwanadamu zinachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu na uchafuzi wa mazingira. 

Siku ya Mazingira duniani.Guterres asema kuwa tunaharibu mazingira yetu wenyewe!

Moto,mafuriko,ukame na vimbunga vikubwa kupita kiasi vinatokea mara kwa mara na vinasababisha uharibifu mkubwa.Mazingira yanatoa ujumbe kwetu ulio wazi kwamba tunaharibu mazingira yetu ya asili hasa yaliyo yetu wenyewe.Ni maneno ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kilele cha Siku ya Mazingira duniani,5 Juni 2020,inayoangazwa na bayonuai.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku ya mazingira duniani inayoadhimishwa tarehe 5 Juni yak ila mwaka kwa kuongozwa na kauli mbiu juu ya bayonuai, amesema kuwa uharibifu wa mazingira na bayonuai unafanyika kwa kasi kubwa huku tabianchi nayo inazidi kusambaratika kila kunapokucha. “Mazingira yanatoa ujumbe kwetu ulio wazi kwamba tunaharibu mazingira yetu ya asili  hasa yaliyo  yetu wenyewe”, amaanza na maneno hayo Katibu Mkuu.

Bwana Guterres amesema kuwa “moto, mafuriko, ukame na vimbunga vikubwa kupita kiasi vinatokea mara kwa mara na vinasababisha uharibifu mkubwa. Kiwango cha joto na aside baharini kinaongezeka na wakati huo vikiharibu mifumo anuai ya matumbawe. Na sasa virusi vipya vya Corona vinaharibu tena afya na mbinu za kipato.” Kwa maana hiyo ameshauri Bwana Guterres a kuwa, kutunza ubinadamu ni lazima kutunza mazingira na “tunahitaji jamii nzima ya kimataifa kubadili mwelekeo. Na kwa kuonya  amesema “Hebu tufikirie upya kile tununuacho na  tutumiavyo.”

Katika kuelekeza zaidi Bwana Guterres amesema kuwa, “tufuate mbinu endelevu kitabia, kwenye kilimo na kwenye biashara, tulinde maeneo yaliyobaki ya wanyapori na tuahidi mustakabali usioharibu mazingira na wenye matumaini”. Bwana Guterres anasema kuwa wakati huu jamii ya kimataifa inafanya kazi kurejesha hali bora, “hebu na turejeshe mazingira katika hali yake, katika kitovu cha hatua zetu za kupitisha maamuzi. Na katika siku ya mazingira duniani hii leo ni wakati wa mazingira.”

Ikumbukwe kuwa Siku ya mazingira ulimwenguni ilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 15 Desemba 1972 kupitia azimio namba A/2994 (XXVII). Mwaka huu maadhimisho yanafanyika pakiwepo na matukio ya kutia hofu kama vile moto katika misitu nchini Brazil, Marekani na Australia na baa la nzige katika Mashariki mwa nchi za  Afrika na sasa janga la COVID-19, hali ambayo Umoja wa Mataifa unasema kuwa inaonesha uhusiano mkubwa kati ya binadamu na mazingira.

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP ni mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika utunzaji wa mazingira kwa njia ya kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo. UNEP hufanya kazi pamoja na serikali, sekta ya kibinafsi, mashirika ya uraia na taasisi zinginezo za Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa ulimwenguni kote.

Katika hili kwa mfano kuna makubaliano mapya kuhusu Maendeleo Ulaya  hasa jinsi Umoja wa Ulaya EU unavyoshughulikia Ajenda 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ambayo inalenga kuleta mabadiliko kwa kiasi kikubwa kwa kusisitiza uwepo wa sera za maendeleo jumuishi kama vile nishati endelevu, hatua za kushughulikia mazingira zinazojumuisha uwekezaji na biashara, ajira, usawa wa kijinsia, vijana, uongozi mzuri, demokrasia, uzingatiaji wa sheria na wa haki za binadamu, uhamiaji na uhamaji.

Kwa kupitia program zake nyingi katika mataifa mbali mbali UNEP inasisitiza kuwa ni muhimu kutumia elimu na maarifa kutoka nchi mbalimbali  ili kubuni sera zinazoweza kutumiwa kwa wingi ili kuhakikisha matokeo chanya na utekelezaji kikamilifu katika ngazi zote za kikanda, kitaifa na kimataifa. Uharibifu wa  mazingira ni dhana ambayo thamani ya uhai wa mazingira inaathiriwa na moja au zaidi ya muunganiko wa njia zinazosababishwa na binadamu katika ardhi.

05 June 2020, 10:21