Tafuta

Tarehe 12 Juni 2020 Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira za Watoto Wadogo: Janga la Corona, COVID-19 limeacha madhara makubwa katika sekta ya uchumi! Tarehe 12 Juni 2020 Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira za Watoto Wadogo: Janga la Corona, COVID-19 limeacha madhara makubwa katika sekta ya uchumi! 

Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira za Watoto Wadogo Mwaka 2020

Tarehe 12 Juni ya kila Mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira za Watoto Wadogo. Shirika la Kazi Duniani, ILO, linasema, kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya mwanadamu, watoto katika kipindi hiki cha janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 wanapaswa kulindwa sana. Janga hili limesababisha madhara makubwa katika sekta ya uchumi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utumwa mamboleo ni mambo ambayo yanafumbatwa katika: Kazi za suluba, ukahaba, biashara ya binadamu na viungo vyake. Kuna masuala ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na uhalifu wa magenge. Matendo yote haya ni uhalifu mkubwa dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu na yanapaswa kutambulika hivi na viongozi wa kidini, kisiasa na kijamii kama yanavyobainishwa na sheria za kitaifa na kimataifa bila kupindishwa pindishwa au kufumbiwa macho! Tarehe 12 Juni ya kila Mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira za Watoto Wadogo. Shirika la Kazi Duniani, ILO, linasema, kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya mwanadamu, watoto katika kipindi hiki cha janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 wanapaswa kulindwa sana.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, janga la Corona, COVID-19 limesababisha madhara makubwa katika sekta ya uchumi na kuna uhaba mkubwa wa nguvu kazi kutokana na watu wengi kufariki dunia kutokana na Virusi vya Corona-COVID-19. Kipeo hiki cha uchumi, kinaweza kuwatumbukiza watoto wengi katika ajira za watoto wadogo. Hadi sasa inakadiriwa kwamba, kuna zaidi ya watoto milioni 152 waliotumbukizwa kwenye ajira za watoto sehemu mbali mbali za dunia. Kati yao kuna watoto milioni 72 wanaoishi na kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi. Kumbe, Shirika la Kazi Duniani, ILO kwa kushirikiana na, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, yanapenda kuwaalika wadau mbali mbali kushirikiana na kushikamana ili kupambana dhidi ya ajira ya watoto wadogo duniani, ili kuwajengea leo na kesho yenye matumaini zaidi. Ikumbukwe kwamba, asilimia kubwa ya ajira za watoto iko kwenye nchi changa zaidi duniani. Hali hii inaathiri ukuaji na ukomavu wa watoto kiafya na kimaendeleo

Ulinzi wa utu na heshima ya binadamu ni dhamana na wajibu wa kisiasa na kijamii na Kanisa linatambua haki hizi msingi katika maisha na utume wake. Hizi ni haki ambazo zimebainishwa kwenye “Tamko la Haki ya Mtoto la Mwaka 1959” na kama haki hizi zinavyofafanuliwa kwenye Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuwawezesha watoto kukua na kukomaa katika mazingira salama katika maisha na utu wao. Hawa ni watoto walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, walipewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Yesu. Unyenyekevu wa watoto ni mfano bora wa kuigwa kwa wale wanaotaka kuingia kwenye Ufalme wa Mungu. Lakini, Yesu anaonya kwamba, Ole wake atakayemkwaza mtoto mdogo, itabidi afungiwe jiwe la kusagia shingoni na kuzamishwa baharini!

Kanisa linataka pia kuungana na Jumuiya ya Kimataifa kukomesha nyanyaso, biashara ya binadamu, utumwa mamboleo na mifumo yake; vita na ghasia; mambo yanayofafanuliwa kwa kina na mapana na Umoja wa Mataifa katika Mikakati ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ifikapo mwaka 2030. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ameshuhudia mateso na mahangaiko ya watoto hawa sehemu mbali mbali za dunia, changomoto na mwaliko kwa kuwawezesha tena watoto kuwa na furaha, amani na utulivu wa ndani kwa kuwajengea mazingira bora ya malezi na makuzi. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuunganisha nguvu kwa kujikita katika: haki, ujasiri na furaha ya kuwaangalia watoto machoni pao pasi ya kuona aibu! Ikumbukwe kwamba, utu na heshima ya binadamu vinafumbatwa katika kazi yake halali! Kumbe, kazi isiwe ni mahali pa kunyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu! Kazi ni jina, heshima na utumilifu wa utu wa binadamu! Kila mtu ajisikie kuwa nawajibika kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu dhidi ya biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo!

Ajira Kwa Watoto Wadogo

 

11 June 2020, 13:13