Tafuta

Vatican News
Tarehe 13 Juni ya Kila mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Unyanyapaa Dhidi ya Walemavu wa Ngozi. Tarehe 13 Juni ya Kila mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Unyanyapaa Dhidi ya Walemavu wa Ngozi. 

Siku ya Kimataifa ya Walemavu wa Ngozi 13 Juni 2020

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako tarehe 18 Desemba 2014 lilitangaza kwamba, kuanzia tarehe 13 Juni 2015, Jumuiya ya Kimataifa itakuwa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Unyanyapaa Dhidi ya Walemavu wa ngozi: “Albino”. Tangu wakati huo, Jumuiya ya Kimataifa imeweza kuadhimisha umoja katika utofauti, ili kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na ushirikishwaji wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yalianza kupamba moto kunako miaka 2000 kutokana na kushamiri kwa imani potofu na za kishirikina. Walemavu wa ngozi ni kundi la watu wanaobaguliwa, kunyanyaswa, kuteswa na hata kuuwawa kikatili. Ni watu wanaokabiliwa na changamoto ya kupata matibabu muafaka, elimu makini na wakati mwingine, wanapotea katika mazingira ya kutatanisha. Mambo yote haya yanachangiwa pia na elimu duni, umaskini na kumong’onyoka kwa tunu msingi za kiutu na kimaadili. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, haki zao msingi zinasimamiwa na kudumishwa na wote. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako tarehe 18 Desemba 2014 lilipitisha Azimio namba 69/170 lililotangaza kwamba, kuanzia tarehe 13 Juni 2015, Jumuiya ya Kimataifa itakuwa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Unyanyapaa Dhidi ya Walemavu wa ngozi: “Albino”.

Tangu wakati huo, Jumuiya ya Kimataifa imeweza kuadhimisha umoja katika utofauti, ili kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na ushirikishwaji wa watu ili kulinda haki zao msingi. Maendeleo na matumaini yaliyopyaishwa na hatimaye, ni mng’ao wa maisha ya walemavu wa ngozi duniani. Umoja wa Mataifa unasema kwamba, licha ya maendeleo makubwa ya sayansi, teknolojia na tiba ya binadamu, lakini bado kuna watu wana amini kwamba, baadhi ya viungo vya walemavu wa ngozi vinaweza kutibu magonjwa na hata wakati mwingine kuleta utajiri wa chapuchapu! Matokeo yake, kumekuwepo na wimbi kubwa la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, “Albino”. Wanasiasa hasa nyakati za kampeni za kuwania uongozi pamoja na wafanyabiashara ni kati ya watu wanaotuhumiwa kujihusisha sana na utekaji na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Walemavu wa ngozi,  wanakabiliwa na wimbi la umaskini ambapo wengi wao hawajapata elimu na hivyo kuwa na maisha magumu lakini pia kutojua mbinu za kujiinua kiuchumi kutokana na jamii kuwaona kana kwamba hawana uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali. Hii ni dhana potofu ambayo imepitwa na wakati! Walemavu wa ngozi wanapaswa kulindwa, kuwezeshwa kielemu pamoja na kujengewa uwezo wa kiuchumi na kiafya ili kupambana na hali na mazingira yao kikamilifu. Serikali mbali mbali duniani hazina budi kuibua mpango mkakati na wenye tija kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi, vingine, maadhimisho haya hayatakuwa na mafao yoyote kwa walemavu wa ngozi.

Walemavu wa Ngozi
12 June 2020, 12:35