Tafuta

Vatican News
Rais Lazarus Chakwera wa Malawi amesema, kati ya vipaumbele vyake ni ujenzi wa umoja wa kitaifa, mapambano dhidi ya umaskini, magonjwa na njaa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rais Lazarus Chakwera wa Malawi amesema, kati ya vipaumbele vyake ni ujenzi wa umoja wa kitaifa, mapambano dhidi ya umaskini, magonjwa na njaa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.  (AFP or licensors)

Rais L. Chakwera: Vipaumbele: Umoja, Ustawi na Maendeleo!

Rais Lazarus Chakwera wa Malawi alizaliwa tarehe 5 Aprili 1955 huko Lilongwe, nchini Malawi. Amejiendeleza zaidi katika masomo ya falsafa na taalimungu nchini Malawi, Afrika ya Kusini na Marekani. Ni Mchungaji, Jaalim na Mwandishi mbobezi wa vitabu kadhaa. Huu ni ushindi wa demokrasia na haki; ni kielelezo cha kiu ya wananchi wa Malawi, wanaotaka kushuhudia mageuzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi linaipongeza Tume ya Uchaguzi nchini Malawi kwa kuendesha mchakato mzima wa uchaguzi kwa kuzingatia: sheria, kanuni na taratibu za nchi, jambo ambalo limeiwezesha Malawi kurudia tena uchaguzi mkuu hapo tarehe 23 Juni 2020 na hatimaye, mshindi kupatikana. Tume ya Uchaguzi nchini Malawi, ikamtangaza Bwana Lazarus Chakwera kuwa Rais na hatimaye, kuapishwa rasmi, Jumapili tarehe 28 Juni 2020, huko Lilongwe, nchini Malawi. Takwimu zinaonesha kwamba, Rais Lazarus Chakwera kutoka Chama cha Malawi Congress Party alipata asilimia 58.57% ya kura zote halali zilizopigwa na wananchi wa Malawi katika uchaguzi wa marudio na kumbwaga Peter Mutharika, mwenye umri wa miaka 79. Rais Lazarus Chakwera wa Malawi alizaliwa tarehe 5 Aprili 1955 huko Lilongwe, nchini Malawi. Amejiendeleza zaidi katika masomo ya falsafa na taalimungu nchini Malawi, Afrika ya Kusini na Marekani. Ni Mchungaji, Jaalim na Mwandishi mbobezi wa vitabu kadhaa.

Rais Lazarus Chakwera wa Malawi anasema, huu ni ushindi wa demokrasia na haki kwa wananchi wa Malawi wapatao milioni 18. Hiki ni kielelezo cha kiu ya wananchi wa Malawi, wanaotaka kushuhudia mageuzi makubwa katika medani mbali mbali za maisha yao. Hii ni heshima kubwa kwa wananchi wa Malawi, kutoa fursa ya uongozi kwa Chama cha Upinzani. Serikali mpya kwa sasa ina jukumu la kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa kuondokana na ndago ya ukabila, kikwazo kikubwa cha maendeleo, ustawi na mafao ya wengi. Huu ni wakati wa kupambana na umaskini, ujinga na njaa, ili kuwajengea wananchi uwezo wa kutimiza ndoto zao za maisha. Hii ni Serikali inayopaswa kuongoza; kwa kusikiliza na kujibu matamanio halali ya wananchi wa Malawi.

Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi lilisikitishwa na vitendo vya ghasia na uvunjifu wa sheria vilivyojitokeza wakati wa maandamano kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2019. Huu ni wakati kwa Serikali kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Umaskini nchini Malawi ni kati ya mambo yanayoendelea kudhalilisha utu na heshima ya watu wa Mungu. Ni wakati wa kukuza na kudumisha utawala wa bora unaozingatia misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi.

Itakumbukwa kwamba, Mahakama ya Katiba nchini Malawi, tarehe 3 Februari 2020 iliamuru kuwa uchaguzi urudiwe, kwa kuwa matokeo ya uchaguzi wa mwanzo yalibatilishwa kwa sababu ya ushahidi mkubwa wa mapungufu pamoja na kughushi kura katika uchaguzi uliofanyika Mei 2019. Katika uchaguzi huo wa mwezi Mei mwaka 2019, Peter Mutharika alitangazwa kuwa mshindi akiwa na asilimia 38% ya kura zote zilizopigwa, Lazarus Chakwera alikuwa mshindi wa pili kwa kupata asilimia 35% na Bwana Saulos Chilima alikuwa mshindi wa tatu kwa kujipatia asilimia 20% ya kura zote halali zilizopigwa. Chakwera na Chilima waliwasilisha kesi dhidi ya uchaguzi wa Peter Mutharika na kuwataka viongozi wa Tume ya Uchaguzi nchini Malawi kujiuzuru kwa kushindwa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao kwa umma. Katika kesi yao ya msingi Chakwera na Chilima walipinga matokeo ya uchaguzi huo wakisema makosa yaliofanyika yaliathiri zaidi ya kura milioni 1.4 kati ya kura milioni 5.1 zilizopigwa.

Malawi
30 June 2020, 08:12