Ubelgiji:Masikitiko ya Mfalme wa Ubelgiji kuhusu ukoloni dhidi ya Congo DRC!
Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican
Mfalme Philip wa Ubelgiji ameelezea maskitiko yake kwa madhara yaliyosababishwa na ukoloni wa nchi yake dhidi ya nchi ya Congo DRC ikiwa ni mara ya kwanza katika utawala wa Ubelgiji kutamka kauli kama hiyo. Katika barua yake aliyompelekea Rais Felix Tshisekedi, tarehe 30 Juni 2020 katika siku ambayo Congo inaadhimisha miaka 60 tangu kumalizika kwa ukoloni wa Ubelgiji, nchini mwao Mfalme Phillip amesema anajutia majeraha ya kale ambayo maumivu yake yapo hadi leo kutokana na ubaguzi unaoendelea kwenye jamii.
Hata hivyo wanahistoria wanasema mamilioni ya Wakongo waliuawa, kukatwa viungo vyao ama kufa kwa maradhi wakati wakifanyishwa kazi za suruba kwenye mashamba ya mipira yaliyokuwa yakimilikiwa na Mfalme Leopold II wa Ubelgiji. Bila ya kumtaja babu yake huyo mkuu kwa jina, Mfalme Philip ameandika kwenye barua hiyo kwamba matendo ya ukatili na unyama yaliyofanywa wakati huo ni sehemu kubwa ya kumbukumbu za pamoja kati ya Congo na Ubelgiji.
Vile vile sanamu kadhaa za Leopold II, aliyetawala kati ya mwaka 1865 na 1909, zimechafuliwa kwa rangi au kuvunjwa na waandamanaji nchini Ubelgiji katika siku za hivi karibuni, hasa katika wimbi la hasira kubwa iliyochochewa na mauaji ya George Floyd mmarekani mweusi mwezi uliopita katika mikononi mwa polisi wa Minneapolis, Marekani. Suala ambalo bado linaendelea kuleta vurugu na machfuko nchini humo na kwingineko.