Tafuta

Vatican News
Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa na wapenda amani sehemu mbali mbali za dunia wameitaka Serikali ya Tanzania kufanya uchunguzi wa kina kuhusu shambulio la Mbowe, ili ukweli ujulikane! Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa na wapenda amani sehemu mbali mbali za dunia wameitaka Serikali ya Tanzania kufanya uchunguzi wa kina kuhusu shambulio la Mbowe, ili ukweli ujulikane!  (AFP or licensors)

Mashambulizi dhidi ya Freeman Mbowe, Uchunguzi wa kina ufanyike, ukweli ubainike!

Usiku wa kuamkia tarehe 9 Juni 2020, Bwana Freeman Aikaeli Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema, Taifa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania alishambuliwa na watu wasiojulikana wakati akirejea usiku nyumbani kwake jijini Dodoma. Rais John Pombe Magufuli, Waziri mkuu Kassim Majaliwa na Spika wa Bunge ni kati ya viongozi waliomtembelea Mbowe!

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, Dodoma na Pd. Richard Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa tarehe 9 Juni 2020 amemtembelea na kumjulia hali Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Aikaeli Mbowe ambaye amelazwa katika hospitali ya Ntyuka jijini Dodoma kwa matibabu. Waziri Mkuu amemwombea kiongozi huyo uponyaji wa haraka wa majeraha aliyoyapata baada ya kuvamiwa na watu ambao bado hawajajulikana wakati akiingia nyumbani kwake jijini Dodoma usiku wa kuamkia tarehe 9 Juni 2020. “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za tukio la kuvamiwa kwa Mheshimiwa Mbowe na watu ambao bado hawajajulikana, namuomba Mwenyezi Mungu amjalie apone haraka ili aweze kurejea katika majukumu yake.” Baadhi ya wabunge wa Upinzani waliokuwepo hospitalini hapo na ambao walimpokea Waziri Mkuu ni Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, Mbunge Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema.

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya, EU Marekani na Uingereza zimeshutumu shambulio dhidi ya kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Freeman Mbowe siku ya Jumanne tarehe 9 Juni 2020. Katika taarifa tofauti zilizowekwa katika tovuti zao, jamii hiyo ya kimataifa imetoa wito kwa serikali ya Tanzania kuanzisha uchunguzi na hatimaye kukamatwa kwa wale wote waliohusika na shambulio la Bwana Freeman Mbowe aliyevamiwa na kushambuliwa na watu wasiojulikana wakati akirejea nyumbani kwake jijini Dodoma huku viongozi wa chama chake wakidai kwamba shambulio hilo lilishinikizwa kisiasa na kwamba, hili ni shambulio dhidi ya demokrasia. Jumuiya ya Umoja wa Ulaya imetaka mchakato wa demokrasia usonge mbele ili kuunda mazingira ya usawa ili uchaguzi uweze kuwa wa wazi, haki na usawa. ''Ubalozi wa Marekani umeshtushwa na kuhuzunishwa na tukio la kikatili la kushambuliwa kwa mbunge na mwenyekiti wa Chadema Freeman Aikaeli Mbowe tarehe 9 Juni, tunatoa pole kwa mbunge huyo na familia yake'', ilisema taarifa hiyo.

10 June 2020, 10:39