Tafuta

Mtazamo wetu katika nchi ya Libia,Ethiopia na Somalia barani Afrika. Mtazamo wetu katika nchi ya Libia,Ethiopia na Somalia barani Afrika. 

AFRIKA:Mtazamo katika nchi ya Ethiopia,Somalia&Libya!

Ethiopia imeanza tena kampeni ya kupanda miche ya miti bilioni 5 ambapo 2019 iliweza kupanda miche bilioni 4.Somalia imekumbwa na majanga ya COVID-19,mafuriko na uvamizi wa nzige.Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Libya imetangaza kufanikiwa kuudhibiti kikamilifu mji mkuu wa nchi hiyo,Tripoli na kuwafukuza mabaki ya wapiganaji wa jenerali Khalifa Haftar.

Na Sr. Angela Rwezaula-Vatican

Katika harakati za kuondoa majanga mengi ya mazingira, nchini Ethiopia imeanza Kampeni ya kupanda miche ya miti bilioni 5, ambapo mwaka jana kampeni  iliyozinduliwa mwezi Mei  ilipanda miti  bilioni 4 kufikia mwezi Oktoba kwa utashi wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed  ili kuacha urithi wa mazingira ya kijani. Ongezeko la kasi sana la idadi ya watu linaloendana na mahitaji makubwa ya ardhi ya kilimo, matumizi yasiyo endelevu ya misitu na mabadiliko ya tabianchi, yanatajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayosababisha kutoweka misitu kwa kasi nchini Ethiopia.

Somalia imekumbwa na majanga ya COVID-19, mafuriko na uvamizi wa nzige

Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya Kibinadamu (OCHA) limetangaza kuwa Somalia inakabiliwa na majanga yaliyosababshwa na mafuriko, uvamizi wa nzige wa jangwani na ugonjwa wa COVID-19. OCHA imesema Somalia ambayo imegubikwa na miongo mitatu ya vita imeweza kupiga hatua kubwa kisiasa na kiusalama lakini mafanikio hayo yako hatarini kutokana na majanga hayo matatu yaliyoikumba nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Kwa mujibu wa OCHA takribani watu 500,000 wamefurushwa kwenye maeneo yao kutokana na mafuriko hayo ambayo yameathiri jumla ya watu zaidi ya milioni moja na kusambaratisha biashara, mazao, masoko, na kuwaacha wengi wakipoteza kila kitu, kushindwa kumudu gharama za chakula na kukosa kipato.

Msaada wa dola milioni 57 unahitajika kwa ajili ya operesheni

Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya Kibindamu (OCHA)limesema kana kwamba vita na mafuriko havitoshi kwani hata uvamizi wa nzige wa jangwani nayo inawasonga watu wa Somalia ambapo wakulima wengi wamepoteza mazao yao yote. Na sasa janga la COVID-19 limezusha taharuki nyingine mpya huku mkuu wa OCHA nchini Somalia Justin Brady akionya kwamba mfumo wa Somalia ni dhaifu kuweza kukabiliana na majanga yote haya kwa pamoja ukilinganisha na mataifa jirani, hali ambayo inatia wasiwasi mkubwa wa kurudisha nyuma hatua zote zilizopigwa kisiasa na kiusalama kwa miongo kadhaa iliyopita na kuiweka tena jamii njia panda. Kwa sasa Shirika la Afya Duniani (WHO) linafanyakazi kwa karibu sana  na OCHA na serikali ya Somalia kudhibiti maambukizi ya COVID-19. Somalia ina wagonjwa zaidi ya 2,080 wa corona na vifo karibu 80. Umoja wa Mataifa na serikali ya Mogadishu wanahitaji dola milioni 57 kwa ajili ya operesheni za kibinadamu na kukabilana na majanga hayo matatu nchini Somalia, lakini hadi sasa fedha zilizopatikana ni asilimia 20 pekee.

Serikali ya Libya imetangaza kufanikiwa kuthibiti wapiganaji 

Baada ya mapambano kwa mwaka mzima, serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imetangaza kufanikiwa katika operesheni la eneo lote la Tripoli ikiwa na kiongozi wake Fayez al-Sarraj ambaye amesema kuikomboa Nchi yote na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Tripoli uliokuwa umeshikiliwa na wapiganaji wa jenerali muasi, Khalifa Haftar. Kufuatia na hiyo, Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Libya imetangaza rasmi kwamba imefanikiwa kuudhibiti kikamilifu mji mkuu wa nchi hiyo, na kuwafukuza mabaki ya wapiganaji wa jenerali muasi, huyo. Taarifa iliyotolewa imesema kuwa, sasa maeneo yote ya mji wa Tripoli yanadhibitiwa na jeshi la taifa na yamekombolewa kutoka mikononi mwa wapiganaji wa Haftar. Ripoti zinasema wapigajani wa jenerali Haftar Jumatano 3 Juni 2020 walilazimika kurudi nyuma na kuondoka katika maeneo ya Wadi Rabie na Ain Zara baada ya kupoteza udhibiti wa Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Tripoli. Ushindi huo wa jeshi la serikali ya sasa ya Libya inayotambuliwa na raia una maana ya kuwafukuza kikamilifu wapiganaji wa Khalifa Haftar kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo.

05 June 2020, 11:49