Tafuta

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasema kwamba, hali ni tete sana nchini Libya kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe sanjari na janga la ugonjwa wa Corona, COVID-19. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasema kwamba, hali ni tete sana nchini Libya kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe sanjari na janga la ugonjwa wa Corona, COVID-19. 

Tamko la Mashirika ya Umoja wa Mataifa Kuhusu Libya! Hali ni tete

Kwa sasa hali ni tete sana kiasi kwamba, tangu mwanzo mwa Mwaka 2020, watu zaidi ya 3, 200 wameokolewa Baharini wakiwa wanajaribu kuikimbia Libya. Kwa bahati mbaya sana, wengi wao wanafia baharini au kuwekwa kizuini, kiasi hata cha kushindwa kuhudumiwa na Jumuiya ya Kimataifa. Kimsingi kumekuwepo na uvunjwaji mkubwa wa haki msingi, utu na heshima ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa yanasema, janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 sanjari na vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea nchini Libya ni tishio kubwa kwa afya na usalama wa wananchi wa Libya. Mashirika haya ni pamoja na: Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, Shirika la Afya Duniani, WHO, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF. Mengine ni Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, OCHA, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu, UNFPA. Kuna zaidi ya watu 400, 000 wasiokuwa na makazi maalum nchini Libya kutokana na vita ambayo imedumu takribani miaka tisa sasa.

Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa kusitisha mapigano haraka sehemu mbali mbali za dunia ili nguvu zote zielekezwe kupambana na janga kubwa la Virusi vya Corona, COVID-19, hadi sasa mwaliko huu umegonga mwamba na mapambano ya silaha yanaendelea kama kawaida nchini Libya. Wafanyakazi wa mashirika ya misaada ya kiutu wameshindwa kuwafikia walengwa kutokana na vizuizi vilivyowekwa. Kwa sasa hali ni tete sana kiasi kwamba, tangu mwanzo mwa Mwaka 2020, watu zaidi ya 3, 200 wameokolewa Baharini wakiwa wanajaribu kuikimbia Libya. Kwa bahati mbaya sana, wengi wao wanafia baharini au kuwekwa kizuini, kiasi hata cha kushindwa kuhudumiwa na Jumuiya ya Kimataifa. Kimsingi kumekuwepo na uvunjwaji mkubwa wa haki msingi, utu na heshima ya binadamu.

Shule na hospitali nyingi zimeshambuliwa kiasi cha kuwakosesha watoto fursa ya kuendelea na masomo pamoja na kupata huduma msingi za afya. Ukiukwaji wa haki msingi za binadamu unaendelea kujidhihirisha hata katika kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kuna hatari kwamba, maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 yakazidi maradufu na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Hadi wakati huu, kuna watu wengi wanaokabiliwa na baa la njaa nchini Libya. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanazitaka pande mbili zinazosigana nchini Libya kusitisha mapigano haraka iwezekanvyo, ili kuanza kuwahudumia wagonjwa Virusi vya Corona, COVID-19. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kutowapatia wananchi wa Libya kisogo, wakati huu wanapoendelea kuchakarika usiku na mchana kutafuta amani ya kudumu.

Libya
15 May 2020, 13:30