Tafuta

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na UNICEF ni matarajio ya kuzaliwa watoto milioni 116 ulimwenguni kufikia mwezi Desemba tangu kutangazwa virusi vya  corona kama janga la kimataifa tarehe 11 Machi 2020 Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na UNICEF ni matarajio ya kuzaliwa watoto milioni 116 ulimwenguni kufikia mwezi Desemba tangu kutangazwa virusi vya corona kama janga la kimataifa tarehe 11 Machi 2020 

DUNIA#coronavirus,UNICEF:watoto milioni 116 watazaliwa kipindi cha janga!

Katika matarajio ya siku ya Mama duniani,ifanyakapo kila mwezi wa Mei,tripoti ya Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF linakadiria kuwa katika kipindi cha janga la covid-19,watazaliwa watoto milioni 116 ulimwenguni kote kati ya Machi hadi Desemba mwaka huu.

Na Sr. Angela Rwezaula- Vatican

Katika kuelekea siku ya mama duniani, iliyotambuliwa kufanyika kila mwezi Mei ya ya kila mwaka na kuungwa mkono na  zaidi ya Mataifa 128, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linakadiria kuwa watoto milioni 116 watakuwa wamezaliwa kwa wiki 40 tangu ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19 utangazwe kuwa janga la kimataifa tarehe 11 mwezi Machi mwaka huu. Taarifa ya UNICEF iliyotolewa tarehe 7 Mei 2020  jijini New York, Marekani inasema kuwa, wanawake waliojifungua na watoto wachanga watakumbana na machungu mapya ikiwemo hatua za kuzuia kuchangamana, vituo vya afya kuzidiwa uwezo wa kutoa huduma, ukosefu wa vifaa vya matibabu, uhaba wa wahudumu wa afya wenye stadi za kutosha kwa kuwa wengi wanahudumia wagonjwa wa Corona sambamba na amri za kutotembea hovyo.

Gonjwa linaathiri hata mfumo wa kawaida kwa wazazi walio wengi

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore amenukuliwa katika taarifa hiyo akisema kuwa mamilioni ya wazazi duniani kote wanaanza safari ya uzazi na ambapo, wanalazimika kujiandaa kuleta kiumbe duniani katika dunia ambayo kwayo, wajawazito wanahofia kwenda vituo vya afya kwa hofu ya maambukizi, au wanakosa huduma ya dharura kutokana na vituo vya afya kuzidiwa uwezo au kutokana na amri ya kutotembea hovyo. Bi. Fore amesema ni vigumu sana kufikiria ni kwa jinsi gani gonjwa la Corona limeathiri uzazi na hivyo UNICEF inaonya kuwa, hatua za kuzuia watu kutoka majumbani mwao zinaweza kuvuruga huduma za afya za kuokoa maisha kama vile huduma za kujifungua na hivyo kuwaweka mamilioni ya wajawazito na watoto wao hatarini.

Nchi zitakazo kuwa na watoto wengi kwa miezi 9 baada ya janga la covid-19

Kwa mujibu wa UNICEF inasema kuwa nchi zinazotarajiwa kuwa na idadi kubwa ya watoto miezi 9 baada ya COVID-19 kutambuliwa kuwa ni janga ni pamoja na India watoto milioni 20.1, China, watoto milioni 13.5, Nigeria watoto milioni 6.4 huku Pakistan ikitarajia watoto milioni 5 na Indonesia watoto milioni 4. Kadhalika Shirika la UNICEF linasema kuwa idadi kubwa ya mataifa hayo tayari yana viwango vya juu vya vifo vya watoto wachanga, hata kabla ya janga la COVID-19 na hivyo viwango hivyo vinaweza kuongezeka wakati huu wa Corona. Marekani nayo ambayo imeathiriwa na janga la Corona inatarajia zaidi ya watoto milioni 3.3 kuzaliwa kati ya Machi 11 hadi Desemba ambapo mamlaka za jimbo la New York, zinaangalia mbinu ya kuweka vituo vya kujifungulia kwa kuwa wajawazito wengi wanahofia kwenda kujifungulia hospitalini.

Serikali zinapaswa kuhakikisha huduma kabla ya kujifungua wajawazito

Lakini pia UNICEF inaonya kuwa ingawa ushahidi unaonesha kuwa wajawazito hawaathiriwi zaidi na COVID-19 kama ilivyokuwa kwa watu wengine, serikali zinapaswa kuhakikisha kuwa bado wanapata huduma za kabla ya kujifungua, za kujifungua na baada ya kujifungua. “Vivyo hivyo watoto wachanga wanahitaji huduma za dharura. Familia mpya zinahitaji msaada kuanza kunyonyesha watoto na kupata dawa, chanjo na lishe ili watoto wao wawe na afya,” imesema UNICEF. Naye Mwenyekiti wa UNICEF Italia Bwana Franesco Samengo amesema”: Italia inatazamiwa idadi ya watoto watakaozaliwa karibu 365.000 na kati ya watoto hawa watazaliwa mahospitali yanayo tambuliwa na Shirika la Watoto (UNICEF) na Shirika la Afya Duniani (WHO) na taarifa ni kwamba ni mwaka 2018 tu walizaliwa watoto katika Hospitali zaidi ya watoto 31.500 ambao walikuwa ni asilimia 7% ya ujumla watoto 449.000.

Wito kwa serikali na wahudumu wa afya kuokoa maisha

Ni kwa mantiki hiyo, UNICEF inatoa wito kwa serikali na wahudumu wa afya kuokoa maisha katika miezi ijayo kwa kuchukua hatua ikiwemo, kusaidia wajawazito kupata huduma za uchunguzi kabla, wakati na baada ya kujifungua na huduma zitolewe na wahudumu wenye ujuzi. Pili, “kuhakikisha wahudumu wa afya wana vifaa vya kujikinga na wanapatiwa kipaumbele katika kupima iwapo wana virusi vya Corona au la na pia iwapo chanjo dhidi ya Corona ikipatikana, wawe wa kwanza kupatiwa ili waweze kutoa huduma bora.” UNICEF inataka pia kuwepo kwa hakikisho la mbinu za kukinga na kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona kwenye vituo vya afya wakati wa kujifungua na baada ya hapo na pia kuwezesha wahudumu wa afya kutembelea wajawazito na wazazi majumbani mwao bila kusahau kutumia teknolojia kama vile simu kufikia wazazi walio maeneo ya ndani zaidi. Ijapokuwa bado haijafahamika iwapo virusi vya Corona vinaweza kuambukizwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujautizo, UNICEF inasihi wajawazito wachukue hatua kujikinga na kufuatilia dalili za virusi hivyo.

“Sikukuu hii ya Mama kwa namna ya pekee inagusa kwa sababu familia nyingi zimelazimika kutengena wakati wa janga la virusi vya corona, lakini ni wakati wa kuungana wote pamoja. Tunaweza kuchangia kuokoa maisha ya binadamu kwa kufanya kwamba kila mama mjazito anapokea msaada ambao anauhitaji ili ajifungue salama katika miezi ijayo” amesihi sana Bi Fore.

Italia kuhamasisha mpango uitwao:‘Kwa pamoja kunyonyesha- Hospitalini & Jumuiya ya Marafiki wa watoto'

UNICEF kwa upande wa Italia, wanahamasisha mpango uitwao “ kwa pamoja kunyonyesha- Hospitalini & Jumuiya ya Marafiki wa watoto” kwa lengo la kuhakikisha watoto wote wanapata lishe ya kutosha na mwanzo wa ubora wa maisha. Hadi leo hii, mpango huo unaunganisha Mtandao wa UNICEF nchini Italia katika mahospitali 30 , kati yao  kuna “Alto Vicentino” ya  Santorso, iliyotajwa kunako mwezi Juni 2018 na Jumuiya 7 zilizotambuliwa na UNICEF kama Marafiki wa watoto, kwa kutoa Kozi 4 za  shahada inayotambuliwa ya Marafiki wa kunyonyesha na zaidi ya  nafasi 900 ziitwazo ‘Baby Pit Stop’ yaani sehemu zinazohusika  kwa ajili ya familia zote ambazo wanaweza kutunza watoto wao kwa serikali na wahudumu wa afya ili katika miezi ijayo waweze kuokoa maisha.

07 May 2020, 10:08