Tafuta

Vatican News
Balozi Dr. Augustine Philip Mahiga, 74, amefariki dunia Jijini Dodoma, tarehe 1 Mei 2020 baada ya kuugua ghafla nyumbani kwake! Balozi Dr. Augustine Philip Mahiga, 74, amefariki dunia Jijini Dodoma, tarehe 1 Mei 2020 baada ya kuugua ghafla nyumbani kwake! 

Tanzia: Dr. Augustine Philip Mahiga amefariki dunia nchini Tanzania!

Rais Magufuli amemwelezea Marehemu Balozi Mahiga kuwa alikuwa ni mchapakazi, mwadilifu, mzalendo na Mwanadiplomasia mahiri aliyeiwakilisha na kuipigania Tanzania katika nyanja za Kimataifa kwa miaka mingi. Balozi Mahiga alikuwa mnyenyekevu na mtiifu kwa kila jukumu alilompatia. Rais Magufuli anamwombea kwa Mwenyezi Mungu ili apumzishe roho yake peponi. Amina.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania anasikitika kutangaza kifo cha Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dr. Augustine Philip Mahiga, Mbunge, kilichotokea alfajiri tarehe 1 Mei 2020 Jijini Dodoma. Taarifa rasmi kutoka kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa inaonesha kwamba, Balozi Mahiga ameugua ghafla akiwa nyumbani kwake Jijini Dodoma na amefikishwa hospitalini akiwa tayari ameshafariki dunia. Rais Magufuli ametoa sala za pole kwa familia ya Marehemu, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Job Yustino Ndugai, Wabunge, Wafanyakazi wa Wizara ya Katiba na Sheria na wananchi wa Mkoa wa Iringa kwa kuondokewa na mpendwa wao, na amesema anaungana nao katika kipindi kigumu cha majonzi.

Rais Magufuli amemwelezea Marehemu Balozi Mahiga kuwa alikuwa ni mchapakazi, mwadilifu, mzalendo na Mwanadiplomasia mahiri aliyeiwakilisha na kuipigania Tanzania katika nyanja za Kimataifa kwa miaka mingi. Pamoja na umri wake mkubwa na uzoefu wa kushika madaraka katika nyadhifa mbali mbali za Kitaifa na Kimataifa, Marehemu Balozi Mahiga alikuwa mnyenyekevu na mtiifu kwa kila jukumu alilompatia. Rais Magufuli anamwombea kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuipumzisha roho yake mahali pema peponi, Amina.

Itakumbukwa kwamba, Dr. Augustine Philip Mahiga alizaliwa tarehe 28 Agosti 1945 huko Iringa na amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 74. Katika maisha yake, amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kati ya Mwaka 2015 hadi Mwaka 2019. Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2010. Aliteuliwa na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon kuwa Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2013. Kunako mwezi Desemba 2015 akateuliwa na Rais John Pombe Magufuli kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Takwimu zinaonesha kwamba, nchini Tanzania katika kipindi cha siku 10 zilizopita hadi kufikia Mei Mosi, 2020 imewapoteza viongozi kadhaa akiwemo: Jaji mkuu mstaafu, Majaji wawili wastaafu, Wabunge wawili wastaafu, Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Uhamiaji Mkoa, wabunge watatu na kati yao ni Balozi Dr. Augustine Philip Mahiga. Kana kwamba, hii haitoshi, Mheshimiwa Haroon Mulla Mbunge wa Mbararli naye ameaga dunia, tarehe 01 Mei 2020. 

 

 

01 May 2020, 08:08