Tafuta

Umoja wa Mataifa unawaomba viongozi wa dini mbali mbali kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kupambana dhidi ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Umoja wa Mataifa unawaomba viongozi wa dini mbali mbali kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kupambana dhidi ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. 

UN: Dhamana ya Viongozi wa Kidini Dhidi ya Corona, COVID-19!

Umoja wa Mataifa unawahimiza viongozi wa dini mbali mbali duniani kuunga mkono jitihada za Umoja wa Mataifa za kupambana na ugonjwa wa Corona-COVID-19. Sherehe na matukio ya kidini licha ya kugusa maisha ya kiroho, lakini pia ni matukio yenye mashiko katika maisha ya kijamii. Hizi ni nyakati ambazo wanafamilia hukutana na kujumuika pamoja, kusherehekea matukio haya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Pasaka ya Kiyahudi “Pèsach”, “Pesah”, “Passover”, ni kati ya Sherehe muhimu sana za dini ya Kiyahudi. Sherehe hii inawakumbusha Waisraeli jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu alivyowaokoa kutoka utumwani Misri kwa mkono wa nguvu na maajabu makubwa! Sherehe hizi kwa mwaka 2020 zilianza tangu tarehe 8 Aprili na kuhitimishwa tarehe 16 Aprili 2020. Kwa Wakristo Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 12 Aprili 2020, ameadhimisha Sherehe ya Pasaka ya Bwana, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Makanisa ya Mashariki nayo yameadhimisha Pasaka ya Bwana hivi karibuni, kama kielelezo cha umoja na mshikamano wa Makanisa ya Mashariki. Kwa upande wa waamini wa Dini ya Kiislamu, Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni muhimu sana katika maisha ya waamini wa dini ya Kiislam.

Matukio yote haya ya kidini sehemu mbali mbali za dunia, yanaadhimishwa katika kipindi hiki ambacho Jumuiya ya Kimataifa inakabiliwa na changamoto kubwa ya Janga la maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Ni katika muktadha huu, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres anawahimiza viongozi wa dini mbali mbali duniani kuhakikisha kwamba, wanasaidia kuunga mkono jitihada za Umoja wa Mataifa za kupambana na ugonjwa wa unaosababishwa na Virusi vya Corona-COVID-19. Sherehe na matukio yote haya licha ya kugusa maisha ya kiroho, lakini pia ni sherehe na matukio yenye mvuto na mashiko katika maisha ya kijamii. Hizi ni nyakati ambazo wanafamilia kutoka sehemu mbali mbali za dunia, hukutana na kujumuika pamoja, kusherehekea matukio haya! Mambo yamebadilika kutokana na athari kubwa za maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Watu wanazuiliwa kwenda nchini na majumbani mwao, kwa hofu kubwa ya maambukizi!

Kumbe, matukio yote haya yanapaswa kuadhimishwa kwa watu kubaki majumbani mwao, huku wakichukua tahadhari ya kuepukana Virusi vya Corona; wajitahidi kuokoa maisha yao na ya jirani zao! Na jambo la muhimu pia ni kuepuka na habari za kizushi zinazoweza kuwachanga kama “Karanga”. Matukio yote haya yawe ni fursa ya kuzama zaidi katika tunu msingi za maisha ya kiroho kwa kuyakumbuka yaliyopita kwa hamasa na kuyaambana ya mbeleni kwa moyo wa matumaini! Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anawataka waamini wa dini mbali mbali duniani kujikita zaidi katika sala na ibada kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya ambao wanaendelea kusadaka maisha yao kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu walioathirika na ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Ni fursa ya kuwakumbuka na kuwasaidia, watu walioathirika kwa vita, wakimbizi na wahamiaji; watu wasiokuwa na makazi maalum; wazee na maskini, bila kuwasahau watu wanaopoteza maisha kutokana na uhaba wa vifaa tiba, huduma duni na uhaba wa miundo mbinu ya huduma bora ya afya!

Huu ni wakati wa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati katika huduma kwa ndugu na jirani; kwa kukuza na kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene, yanayofumbatwa katika huduma! Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres anasema, mapambano dhidi ya Janga kubwa la Virusi vya Corona, COVID-19 yataweza kufanikiwa, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itazidisha umoja na ushirikiano wa dhati; kwa kujenga na kudumisha mshikamano katika imani, utu na udugu wa kibinadamu!

Viongozi wa Kidini 2020

 

 

27 April 2020, 13:04