Tafuta

Mkutano wa Umoja wa Nchi za Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia 9 Februari 2020 Mkutano wa Umoja wa Nchi za Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia 9 Februari 2020 

Viongozi wa Afrika wanataka washughulikie masuala yanayowahusu wao!

Wakuu wa mataifa ya Afrika wamekutana Jumapili 9 Februari 2020 mjini Addis Ababa Ethiopia kwa ajili ya mkutano wa kila mwaka wa kilele,huku wakitoa wito kusuluhisha mizozo ya ndani na kuzuia uingiliaji kutoka nje.

Na Sr Angela Rwezaula –Vatican

Wakuu wa mataifa ya Afrika wamekutana mwishoni mwa wiki iliyopita  mjini Addis Ababa, Ethiopia kwa mkotano wao  wa kila mwaka   uliokuwa unaongozwa na mada “kunyamazisha milio ya risasi: Imarisha uwezo wa Afrika kuelekea maendeleo”, na wakihitimisha kwa kukazia wito wa kuchukua hatua katika kusuluhisha mizozo ya ndani ili kuzuia uingiliaji kutoka nje.  Afrika kusini imechukua uenyekiti wa Umoja huo kwa mwaka huu wa 2020, kutoka Misri.

Rais Cyiril Ramaphosa akizungumzia juu ya mkutano anasema Afrika Kusini itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa mwezi Mei utakaojadili pamoja na masuala mengine changamoto dhidi ya amani na usalama wa bara la Afrika.  Bwana  Ramaphosa amesema “Mkutano tutakaouandaa utatakiwa kufikiria hatua madhubuti ambazo sisi kama waafrika tunatakiwa kuzichukua ili kumaliza mizozo na vitendo vya ugaidi vinavyojitokeza kwenye mataifa na kanda mbali mbali kama za Sahel, ambavyo kwa sasa vinasambaa kwenye maeneo mengine ya Kusini mwa Afrika pia.”

Mizozo ya Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, mali na ukanda wa Sahel ni miongoni mwa ile iliyopewa kipaumbele kwenye majadiliano ya mkutano huo wa kilele wa Umoja huo wa Afrika. Rais Ramaphosa alisisitiza kwamba Afrika inatakiwa kuchukua nafasi yake katika kusuluhisha mizozo yake ya ndani ili kuzuia uingiliaji wa nje.

Naye Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye pia ameshiriki katika mkutano huo pamoja na masuala mengine amewaeleza wakuu hao kwamba bara la Afrika linatakiwa kujiimarisha katika kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa ambazo tayari ziko dhahiri. “Joto linaongezeka mara mbili ya wastani wa kidunia. Mwaka jana hali ilikuwa mbaya sana. Pamoja na athari za vimbunga Idai na Kenedy, taarifa zinasema kwamba vilitokana na mabadiliko ya tabianchi, kuanzia Sahel hadi Zambia, Kenya hadi Madagascar”

Viongozi hao pia wamejipa changamoto ya kujikita zaidi katika kuwawezesha wanawake na wasichana. Katika kutekeleza hilo, tayari Umoja huo pamoja na tume ya kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika wamezindua wakfu wa kuwasaidia wanawake kupata mikopo kwa ajili ya biashara.

10 February 2020, 17:19