Tafuta

Wataalam wanakadiria kwamba karibu watu milioni 4.8 Sahel ya Kati watakuwa katika hatari ya kutokuwa na uhakika wa chakula hasa katika msimu wa Juni hadi Agosti 2020 ikiwa hatua  hazitachukuliwa haraka Wataalam wanakadiria kwamba karibu watu milioni 4.8 Sahel ya Kati watakuwa katika hatari ya kutokuwa na uhakika wa chakula hasa katika msimu wa Juni hadi Agosti 2020 ikiwa hatua hazitachukuliwa haraka  

Milioni 1 ya watu wanateseka kwa njaa na kipeo cha kibinadamu ukanda wa Sahel!

Tarehe 3 Februari 2020 imetolewa Taarifa ya pamoja ya mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa (FAO/UNICEF/WFP) kuonesha hali halisi ya watu wanaoteseka kwa njaa na kipeo cha kibinadamu hasa changamoto za usalama katika ukanda wa Sahel unaounganisha nchi za Burkina Faso,Mali na Niger.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Taarifa ya pamoja iliyotolewa tarehe 3 Februari 2020  na mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa (FAO/UNICEF/WFP) imeonya kwamba idadi ya watu wanaokabiliwa na upungufu wa chakula na fursa muhimu za maisha katikati mwa Sahel imeongezeka sana katika mwaka mmoja uliopita kutokana na changamoto za usalama na mabadiliko ya tabianchi.

Mashirika hayo la  Mpango wa Chakula Duniani (WFP), la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na la Chakula na Kilimo (FAO) yamesema kwamba hali huenda ikawa mbaya zaidi ikiwa  jumuiya ya kimataifa hazitachukua hatua sasa. Taarifa hiyo inasema, “Licha ya hali inayoridhisha katika uzalishaji wa kilimo kwa ujumla watu milioni 3.3 wanahitaji msaada wa haraka Sahel ya Kati kwa mujibu wa tathimini ya mfumo wa uhakika wa chakula.”  Wataalam wanakadiria kwamba karibu watu milioni 4.8 Sahel ya Kati watakuwa katika hatari ya kutokuwa na uhakika wa chakula hasa katika msimu utakaoanza Juni hadi Agosti 2020 endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa haraka kuzuia hali hiyo.

Naye Chris Nikoi mkurugenzi wa kanda ya Afrika Magharibi na Kati amesema “Tunashuhudia ongezeko kubwa la njaa Sahel ya Kati, idadi ya watu wasio na uhakika wa chakula imeongezeka mara mbili baada ya msimu wa mavuno badala ya kupungua. Tusipochukua hatua sasa kizazi chote kipo hatarini”  Kwa mujibu wa mashirika hayo maeneo yanayotia wasiwasi zaidi ni nchini Burkina Faso, Mali na Niger ambako vita athari zake katika jamii vimekuwa chanzo kikubwa cha kutokuwa na uhakika wa chakula.

Vita, mashambulizi kutoka kwa makundi yenye silaha pia vimewafanya maelfu ya watu kufunga virago katika nchi hizo. Mabadiliko ya tabianchi pia yameelezwa kuwa kichochezi cha hali hiyo na kusababisha mifugo kujikusanya katika eneo moja hali inayotishia kuzuka kwa machafuko baina ya wakulima na wafugaji. Na kwa mujibu mratibu wa Fao katika ukanda huo  Bwana Robert Guei amesema, “Tusiposhughulikia mizizi ya mgogoro huu mamilioni ya wafugaji na wakulima wataendelea kuhitaji msaada wa haraka kila mwaka kama ilivyokuwa mwaka 2019 na sasa 2020”.

Naye mkurugenzi wa kanda ya Afrika Magharibi na Kati wa UNICEF,  Bi Marie-Pierre Poirier amesema “Mgogoro Sahel ya Kati ni zahma inayoikumba kanda nzima na kukiweka kizazi chote cha watoto katika hatari. Maelfu ya watoto wanakosa elimu, wako katika hatari ya kunyonywa, na kupata utapiamlo na ndio wanaoendelea kulipa gharama kubwa ya mgogoro ambao hawakuuanzisha. Tunahitaji kuchukua hatua sasa kuepuka janga zaidi”

04 February 2020, 15:59