Tafuta

Vatican News
Nzige wanavyovamia kila sehemu na kuangamiza kila kitu Nzige wanavyovamia kila sehemu na kuangamiza kila kitu 

FAO:Shukrani kubwa kwa msaada kutoka taasisi ya Bill & Melinda Gates!

Shirika la chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO linapongeza taasisi ya Bill na Melinda Gates kwa kutoa msaada wa dola milioni 10 katika kusaidia harakati za kukabiliana na nzige waliovamia Afrika ya Mashariki.Hata hivyo bado wanazidi kukaribishwa wahisani wengine ili kukabiliana na janga hili ambalo hadi sasa nzige wamevamia Djibouti,Eritrea,kusini,Sudan Kusini,Uganda kenya hadi magharibi mwa Iran.

Na Sr.Angela Rwezaula – Vatican

Wito wa Umoja wa Mataifa wa kutaka wahisani kusaidia harakati za kukabiliana na nzige wavamizi wa jangwani huko Afrika Mashariki umeanza kupata mwitikio ambapo msaada umetolewa hivi karibuni wa dola milioni 10 kutoka taasisi ya Bill na Melinda Gates. Msaada huo umewakilishwa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO ambapo Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo lenye  makao  yake mjini Roma, Italia, Bwana QU Dongyu amekaribisha na kutoa shukrani kwa taasisi hiyo.

Taarifa ya FAO iliyotolewa mjini Roma, Italia imesema kuwa fedha hizo, zitasaidia serikali za Ethiopia, Kenya na Somalia katika kukabiliana na kuzaliana kwa nzige ambao wanatishia uzalishaji wa chakula na harakati za kujipatia kipato kwa wakazi wa ukanda huo.  Bwana Qu ameshukuru taasisi hiyo na kusema kuwa, “nasihi wahisani wengine nao wafuate mfano wao ili tuweze kulinda njia za kipato za wakazi wa vijijini, kusaidia wakulima pia na familia zao.” Baa la sasa la nzige ni baya zaidi kuwahi kukumba Ethiopia na Somalia katika kipindi cha miaka 25 na ni kiwango cha kuzaliana kwa nzige nchini Kenya ni kibaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 70. Kwa mujibu wa jarida la FAO, Desert Locust Watch, Djibouti na Eritrea nazo pia zimeathirika na wimbi la nzige limeenea maeneo ya kusini mashariki mwa Sudan Kusini na Uganda hadi kusini magharibi mwa Iran.

Kwa sasa FAO imeongeza ombi lake la fedha hadi dola milioni 138 kutoka ombi la awali la dola milioni 76 lililotolewa mwezi mmoja uliopita kwa lengo la kusaidia nchi zilizoathirika. Hadi sasa ni dola milioni 33 tu zilizokwishaahidiwa au kupatikana. Mkurugenzi Mkuu Qu  wa FAO akizungumza hali ya sasa ya wadudu hao hatari amesema kuwa inatia wasiwasi mkubwa na kwamba wiki chache zijazo zitakuwa muhimu katika kuanzisha operesheni fanisi ya kudhibiti nzige hao wa jangwani. “Ongezeko la wadudu hao linatishia vipato vya watu na usalama wa chakula kwenye eneo hilo ambalo tayari linakabiliwa na uhaba wa chakula.  Hakuna muda wa kupoteza,”  amesema Bwana Qu.

Nzige wa jangwani anatambuliwa kuwa mdudu wa kuhamahama hatari zaidi duniani na kundi dogo la wadudu hao lililopo kwenye usawa wa kilometa 1 ya mraba, linaweza kula chakula kinachotosheleza watu 35,000 kwa siku moja. Wakiwa katika mazingira mazuri ya kuzaliana, wanataga mayai haraka na kuzaliana na idadi yao inaweza kuongezeka mara 500 katika kipindi cha miezi 6.

 

25 February 2020, 15:13