Tafuta

Vatican News
WFP limekaribisha mchango wa dola milioni 3.39 kutoka mfuko wa Marekani wa maendeleo ya kimataifa USAID kusaidia kutatua hitaji la haraka la chakula kwa watu walioathirika na ukame nchini Zambia. WFP limekaribisha mchango wa dola milioni 3.39 kutoka mfuko wa Marekani wa maendeleo ya kimataifa USAID kusaidia kutatua hitaji la haraka la chakula kwa watu walioathirika na ukame nchini Zambia.   (ANSA)

Mchango wa dola milioni 3.39 kusaidia dharura nchini Zambia!

Shirika la Mpango na Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP)limekaribisha mchango wa dola milioni 3.39 kutoka mfuko wa Marekani wa maendeleo ya kimataifa USAID kusaidia kutatua hitaji la haraka la chakula kwa watu walioathirika na ukame nchini Zambia.Ongezeko la uhitaji ni baada ya ukame na kipindi kirefu cha kukosekana kwa mvua ambacho kimewaacha watu milioni 2.3 wakiwa hawana chakula.

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP, tarehe 6 Januari  limekaribisha mchango wa dola milioni 3.39 kutoka mfuko wa Marekani wa maendeleo ya kimataifa USAID kusaidia kutatua hitaji la haraka la chakula kwa watu walioathirika na ukame nchini Zambia.  Msaada huo wa Marekani ambao ulithibitishwa mwezi uliopita wa Desemba, umekuja katika wakati wa ongezeko la uhitaji baada ya ukame na kipindi kirefu cha kukosekana kwa mvua ambacho kimewaacha watu milioni 2.3 wakiwa hawana chakula na wakiwa katika uhitaji mkubwa wa msaada. Kupitia ufadhili huu, WFP itasambaza tani 2,380 za mahindi, na kuwapatia chakula na lishe  kwa watu 255,000 walioathirika nchini kote.

Akizungumzia mchango huo, Mwakilishi wa WFP nchini Zambia, Jenniffer Bitonde amesema, “WFP inahitaji dola milioni 36 za kimarekani ili kuweza kuisaidia serikali ya Zambia katika kukabiliana na janga. Mchango wa USAID unawakilisha asilimia 10 ya jumla ya hitaji lote na utairuhusu WFP  kuhakikisha watu waliothirika na ukame hawataenda kulala wakiwa na njaa katika kipindi hiki cha mwaka.” Takribani watu milioni 1.1 wanategemewa kupokea msaada wa WFP wakati watu wengine milioni 1.2 watasaidiwa na serikali na wadau wengine ambao WFP inashirikiana nao. Serikali ya Marekani ni moja ya wachangiaji wakubwa wa shughuli za WFP katika kuwasaidia wakimbizi kuanzia kule katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC. Kwa mwaka jana wa 2019, WFP imewasaidia takribani wakimbizi 14,000.

Na mwanzoni mwa Januari 2020, Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP limeainisha maeneo 15 ambayo yatahitaji msaada wa dharura na uwekezaji kwa mwaka huu wa 2020.  Kwa mujibu wa ripoti ya WFP, “Maeneo yaliyo hatarini duniani kwa 2020” , ni kuwa Haiti inashikilia nafasi ya kwanza ikielezewa iko katika hatari kubwa ya kutumbukia zaidi katika mgogoro endapo hatua za haraka, msaada na uwekezaji havitopatikana kwa mwaka 2020. Mmoja wa wakulima wa mbogamboga nchini humo Osena Previlon amenukuliwa na WFP akisema “Hatuishi vuzuri, hatuli vizuri na hatuwezi hata kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa sababu ya zahma iliyoikumba nchi yetu”

Kwa mujibu wa WFP machafuko ya kisiasa na kijamii yameitumbukiza nchi hiyo katika mtafaruku mkubwa huku bei za chakula Haiti zikipanda kwa asilimia 40 na mtu mmoja kati ya watatu nchini humo sawa na watu milioni 3.7 wanahitaji msaada wa haraka wa chakula vijijini na mijini na miongoni mwao milioni 1 wanakabiliwa na janga la njaa. WFP inaitaka dunia kuwekeza mabilioni ya dola 2020 ili kukomesha hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula inayoongezeka kote duniani. Ripoti hiyo imesema: Zimbabwe ni nchi nyingine iliyo katika hatari ambayo imeshuhudia ukame mbaya zaidi mwaka 2019 na utakapowadia msimu wa muambo Februari WFP inasema chakula chote kitakuwa kimeisha na watu milioni 7.7 wanakabiliwa na njaa na kuhitaji msaada wa chakula.

Aidha Sudan Kusini kwa mujibu wa ripoti hiyo bado kunatokota kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe watu milioni 3.8 wametawanywa na mafuriko ya 2019 yamewaathiri takriban watu milioni 1 na kuathiri tani Zaidi ya 73,000 za nafaka hali ambayo imewafanya baadhi ya wakulima nchini humo kujiuliza “endapo Mungu amewasahau” Maeneo mengine yaliyotajwa na ripoti hiyo ni Ukanda wa Sahel, Mali, Burkina Fasso na Magharibi mwa Niger ambako ni kutokana na mchanganyiko wa sababu ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, vita, na mamilioni ya watu kutawanywa. WFP inakadiria kuwa itahitahiji zaidi ya dola bilioni 10 mwaka huu 2020 ili kufadhili operesheni zake katika zaidi ya nchi 80 duniani kote na bila fedha hizo mipango yote ya uzaidizi itakuwa njiapanda. WFP imeongeza kuwa “Dunia ni sehemu isiyosameheka na tunapofungua ukurasa mpya 2020, WFP inakabiliwa na changamoto mpya na kubwa zinazohitaji kushughulikiwa kwa haraka ili kuokoa maisha.”

 

07 January 2020, 16:31