Tafuta

Vatican News
Umoja wa Mataifa unawataka wananchi wa Msumbiji baada ya uchaguzi mkuu kuanza kujikita katika ujenzi wa demokrasia, haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa. Umoja wa Mataifa unawataka wananchi wa Msumbiji baada ya uchaguzi mkuu kuanza kujikita katika ujenzi wa demokrasia, haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.  (AFP or licensors)

UN: Uchaguzi Mkuu Msumbiji 2019: Amani na Umoja wa Kitaifa!

Takwimu zilizotolewa na Tume ya Uchaguzi Nchini Msumbiji zinaonesha kwamba, Rais Nyusi alipata kura asilimia 73% ya kura zote halali zilizopigwa na mpinzani wake Bwana Ossufo Momade wa RENAMO akajinyakulia kura asilimia 22% za kura zote. Upinzani walikataa kukubaliana na matokeo haya kwa misingi kwamba, uchaguzi umefanyika katika hali ya vitisho pamoja na “wizi wa kura”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres amesema, baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Msumbiji tarehe 15 Oktoba 2019 na Rais Filipe Jacinto Nyusi wa Chama cha FRELIMO kuibuka kidedea katika uchaguzi mkuu, kuna haja sasa kwa Msumbiji kuendelea kujikita katika ujenzi wa misingi ya haki, amani, demokrasia na umoja wa kitaifa. Hivi karibuni, Chama cha FRELIMO kimewekeana tena saini Mkataba wa Amani na Chama cha RENAMO ambacho kwa sasa kinaongozwa na Bwana Ossufo Momade. Lengo ni kusitisha vita na mashambulizi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia; pamoja na kuhakikisha kwamba, ulinzi na usalama wa Msumbiji unaendelea kuimarishwa. Hakuna tena sababu msingi za vikosi vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Msumbiji kushambuliana na majeshi ya RENAMO.

Mkataba huu, unaweka matumaini makubwa katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Mchakato wa uchaguzi na hatimaye matokeo kutangazwa na kukubalika katika hali ya amani na utulivu ni hatua kubwa katika ujenzi wa demokrasia shirikishi nchini Msumbiji. Umefika wakati kwa wananchi wa Msumbiji kujenga na kuimarisha umoja wa Kitaifa, ili hatimaye, kuanza mchakato wa umoja na upatanisho wa kitaifa; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini humo! Takwimu zilizotolewa na Tume ya Uchaguzi Nchini Msumbiji zinaonesha kwamba, Rais Nyusi alipata kura asilimia 73% ya kura zote halali zilizopigwa nchini Msumbiji na mpinzani wake Bwana Ossufo Momade wa RENAMO akajinyakulia kura asilimia 22% za kura zote. Upinzani walikataa kukubaliana na matokeo haya kwa misingi kwamba, uchaguzi umefanyika katika hali ya vitisho pamoja na “wizi wa kura”.

Msumbiji: Uchaguzi
02 November 2019, 13:43