Tafuta

Vatican News
Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania amemwapisha CAG Charles Edward Kichere, Majaji 12 wa Mahakama kuu pamoja na viongozi mbali mbali walioteuliwa 3 Novemba 2019. Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania amemwapisha CAG Charles Edward Kichere, Majaji 12 wa Mahakama kuu pamoja na viongozi mbali mbali walioteuliwa 3 Novemba 2019.  (AFP or licensors)

Rais Magufuli amwapisha CAG Kichere na Majaji 12 wa Mahakama Kuu

Rais Magufuli amemtaka Bwana Charles Kichere kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa uhuru kabisa pamoja na kuzingatia mipaka ya kazi yake akitambua kwamba, anapaswa kushirikiana na mihimili mingine yaani: Serikali, Bunge na Mahakama. Rais Magufuli amemtaka CAG kushughulikia kasoro ambazo zimejitokeza katika ofisi ya CAG na hivyo kuichafua kimaadili! Hapa kazi tu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania, Jumatatu tarehe 4 Novemba 2019 amemwapisha Charles Edward Kichere mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali, Majaji 12 wa Mahakama Kuu, Kamishna wa Kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Balozi wa Tanzania Nchini Kuwait pamoja na Viongozi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Viongozi wote hawa wamekula kiapo cha maadili ya viongozi wa umma. Kwa namna ya pekee kabisa, Rais Magufuli amemtaka Bwana Charles Kichere kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa uhuru kabisa pamoja na kuzingatia mipaka ya kazi yake akitambua kwamba, anapaswa kushirikiana na mihimili mingine yaani: Serikali, Bunge na Mahakama. Rais Magufuli amemtaka CAG Kichere kushughulikia kasoro ambazo zimejitokeza katika ofisi ya CAG na hivyo kuichafua kimaadili, ikiwemo baadhi ya watumishi kulipwa posho kinyume cha taratibu, kanuni na sheria.

Rais Magufuli amempongeza kwa uvumilivu wa kisiasa aliouonesha alipotengua uteuzi wake kama Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania na baadaye akamteua tena kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Jombe, tarehe 8 Juni 2019. Katika muktadha huu, kweli yataka moyo! CAG Kichere ameyashuhudia yote haya sasa ni wakati wa kuchapa kazi kwa ari na moyo mkuu, kwani Tanzania kumenoga! Bwana Charles Kichere anachukua nafasi ya Profesa Mussa Assad ambaye kipindi chake cha uongozi cha miaka mitano kimefikia ukomo, tarehe 4 Novemba 2019. Profesa Assad anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kuwatumikia watanzania katika kipindi hiki na kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye anayetoa riziki, atampatia kazi nyingine kwa wakati wake! Anashukuru na kusamehe yote, ili kuanza upya mchakato wa maisha!

 

04 November 2019, 16:23