Tafuta

Vatican News
Tarehe 3 Oktoba 2019: Siku Maalum ya Kuwakumbuka na Kuwaombea Wahanga wa Uhamiaji wanaopoteza maisha yao wakiwa njiani kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi! Tarehe 3 Oktoba 2019: Siku Maalum ya Kuwakumbuka na Kuwaombea Wahanga wa Uhamiaji wanaopoteza maisha yao wakiwa njiani kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi! 

Wakimbizi & Wahamiaji: Bahari ya Mediterrania imegeuka kuwa kaburi

Takwimu za mwaka 2018 zilizotolewa na UNHCR., zinaonesha kwamba, waliofariki dunia au kupotea katika mazingira ya kutatanisha walikuwa ni wakimbizi na wahamiaji 2277, kati yao wakimbizi na wahamiaji 1279 walizama na kufamaji kwenye Bahari ya Mediterrania ambako makaburi yao hayana alama na wala ndugu na jamaa zao hawana mahali pa kwenda kuwaombolezea. HATARI YA KIFO.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Serikali ya Italia kila mwaka ifikapo tarehe 3 Oktoba inaadhimisha Siku Maalum ya Kuwakumbuka Wahanga wa Uhamiaji wanaopoteza maisha yao katika harakati za kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi ugenini. Siku hii ilianzishwa kunako mwaka 2016 kama kumbu kumbu ya kuwaenzi wahamiaji na wakimbizi 368 waliozama na hatimaye, kufa maji huko Lampedusa, Kusini mwa Italia, kunako tarehe 3 Oktoba 2013. Boti hii ilikuwa imebeba abiria 368, ilishika moto na hatimaye, kuzama baharini. Katika maadhimisho ya Mwaka huu, maelfu ya watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za Ulaya wameshiriki, ili kuushinikiza Umoja wa Ulaya kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuokoa maisha ya watu wanaoendelea kufamaji kwenye Bahari ya Mediterrania.

Idadi ya wakimbizi na wahamiaji wanaopoteza maisha wakiwa njiani kwenda Ulaya kwa mwaka 2019 inazidi kuongeza maradufu. Takwimu za mwaka 2018 zinaonesha kwamba, waliofariki dunia au kupotea katika mazingira ya kutatanisha walikuwa ni wakimbizi na wahamiaji 2277, kati yao wakimbizi na wahamiaji 1279 walizama na kufamaji kwenye Bahari ya Mediterrania ambako makaburi yao hayana alama na wala ndugu na jamaa zao hawana mahali pa kwenda kuwaombolezea. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR., limeutaka Umoja wa Ulaya kurejesha tena huduma ya kuwatafuta na kuwaokoa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha yao; changamoto inayohitaji kupewa kipaumbele cha pekee pamoja na kujenga umoja na mshikamano Barani Ulaya, ili kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji!

Lampedusa
04 October 2019, 17:31