Tafuta

Vatican News
Kila ifikapo tarehe 19 Agosti ni Siku ya Kimataifa ya Huduma ya Kibinadamu! Kila ifikapo tarehe 19 Agosti ni Siku ya Kimataifa ya Huduma ya Kibinadamu! 

tarehe 19 Agosti ni Siku ya Kimataifa ya Huduma za kibinadamu!

Tarehe 19 Agosti ni siku ya Kimataifa ya huduma za kibinadamu na ofisi ya Caritas Ulaya inasema siku hii haipaswi kukumbukwa kwa siku moja tu kwa ajili ya huduma ya kibinadamu,bali iwe ni mwendelezo wa utoaji huduma kwa dharura nyingi.Kwa upande wa Umoja wa Mataifa katika kilele hiki umeangazia wanawake waliojitolea kusaidia wengine katika nchi zenye kipeo cha mizozo.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Ofisi ya Caritas Ulaya imekumbusha katika kilele cha Siku ya Kimataifa ya Huduma za kibinadamu, (World Humanitarian Day) inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 19 Agosti ya kila mwaka kwamba: “Siku hii haipaswi kukumbukwa kwa siku moja tu kwa ajili ya huduma ya kibinadamu. Mara nyingi dharura na waathirika wake hawaonekani au kusahuliwa kwa yote. Matukio haya ni ya kuleta wasiwasi, hasa kwa sababu ya kipeo cha kibinadamu ambacho kinazidi kuongezeka na kuwa daima kigumu kukikabiliana nacho".  Siku hii ilitangazwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2008 kama kwamna ni  kutoa jibu la shambulizi la kigaidi lililokuwa limetokea miaka mitano kabla katika Mtaa wa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa huko Baghdad Iraq na kusababisha vifo vya watu 22. Aidha Ofisi ya Caritas Ulaya inasema “kila mtu anahusika katika matendo ya dhati ya kutoa huduma ya kibinadamu, iwe katika nchi mahalia au nje ya nchi. Caritas ni kituo kikubwa cha jumuiya, kwa ngazi ya kwanza, ya kati au baada ya dharura kwa ajili ya kusaidia watu wenye kuhitaji".

Caritas ya Ulaya iko hai katika kushirikishana na kusaidia dharura

Na kwa ajili ya kuhamasisha zaidi juu ya dharura katika matendo madogo madogo  na kati kwa ngazi ya Ulaya, na mahali ambapo Caritas ni hai na kwa ajili ya kushirikishana taarifa juu ya ulinzi wa kibinadamu, wamezindua chombo maalumukinacho husika na matendo ya kibanadamu. Lengo lake ni kuwakilisha jibu lao la utoaji msaada wa dharura na ambapo kila wakati watasasisha taarifa za matendo hayo katika mtandao na kuhakiki. Na kwa taarifa zaidi bonyeza kupitia tovuti hii: https://www.caritas.eu/humanitarian-action/

Umoja wa Mataifa unaangazia wanawake katika utoaji huduma

Na kwa upande wa wa Umoja wa Mataifa katika kilele cha kuadhimisha Siku ya huduma za kibinadamu kwa mwaka huu imemlika wanawake waliojikita katika kutoa huduma za kibinadamu kote ulimwenguni. Katika ujumbe wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres amesema wanawake wanamulikwa kutokana na tofauti kubwa wanayoleta pale wanaposhiriki kutoa huduma za kibinadamu kwa mamilioni ya wanawake, wanaume na watoto. “Kuanzia kuwasaidia raia waliokumbwa na migogoro hadi kushughulikia milipuko ya magonjwa, wanawake wahudumu wa kibinadamu wako mstari wa mbele. Uwepo wao unafanya operesheni za misaada kuwa nzuri zaidi kwa kuongeza ufikiaji wao. Pia unaboresha hatua zinazochukuliwa dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, ambao huongezeka wakati wa dharura,”

Lazima kuthibitisha ahadi ya kuimarisha jukumu la wanawake

Aidha Katibu Mkuu ametaka kila mtu kushiri katika simulizi za wanawake hao, simulizi ambazo zina nguvu na hivyo amsema:“kuthibitisha ahadi yetu  ya kuimarisha jukumu la wanawake katika operesheni za kibinadamu.” Kupitia ujumbe huo Katibu Mkuu Bwana Guterres amewageukia pia viongozi wa dunia na pande katika mizozo na kusema kuwa wanapaswa kuhakikisha kwamba wahudumu wa kibinadamu wanalindwa dhidi ya madhara, kama inavyotakiwa chini ya sheria za kimataifa. “Ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu unaendelea duniani kote. Ni lazima uchunguzwe na kuchukuliwa hatua,” amesema Bwana Guterres, huku akitamatisha ujumbe wake akisema kuwa “katika siku ya huduma za Kibinadamu na kila siku, tunasimama pamoja na wahudumu wa kibinadamu kote duniani.”

Ikumbukwe kwamba Siku ya huduma za kibinadamu duniani huadhimishwa kila ifikapo tarehe 19 Agosti ya kila mwaka tangu mwaka 2008 kwa kukumbuka shambulizi dhidi ya jengo la makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Baghdad nchini Iraq tarehe 19 Agosti mwaka 2003. Shambulio hilo lilisababisha vifo vya watu 22 akiwemo mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Iraq Sergio Vieira de Mello. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kuadhimisha siku hii mwaka 2008 kupigia chepuo ulinzi na usalama wa wafanyakazi wanaotoa huduma za kibinadamu sambamba na utu wao kwenye maeneo yenye mizozo.

Umoja wa Mataifa waadhimisha tukio hili maalum

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani, Naibu Katibu Mkuu Amina J. Mohammed ameongoza tukio la kukumbuka wale waliopoteza maisha mjini Baghdad, Iraq tarehe 19 mwezi Agosti mwaka 2003 sambamba na kutambua mchango wa maelfu ya wanawake wanaofanya kazi za kujitolea kusaidia binadamu walio hatarini. Katika shambulio hilo mjini Baghdad watu 22 waliuawa akiwemo Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq Sergio Vieira de Mello. Akizungumza kwenye tukio hilo, Bi. Mohammed amesema, “wale wanaoshambulia Umoja wa Mataifa wanataka tuwe na uoga, tujione dhaifu na turudi nyuma. Mchango wa wale waliopoteza maisha ndio bado upo na ndio maana tunaahidi kuokoa watu kutoka kwenye shida na vifo na azma yetu ya kujenga mustakabali bora kwa wote.” Katika tukio hilo, washiriki walinyamaza kimya kwa dakika moja kukumbuka waliopoteza maisha wakihudumia binadamu.

Wanawake wahudumu wa kibinadamu ni 250,000 ambayo ni zaidi ya asilimia 40 ya nguvu kazi

Duniani kote kuna wanawake wahudumu wa kibinadamu 250,000 idadi ambayo ni zaidi ya asilimia 40 ya nguvukazi katika sekta ya huduma za kibinadamu. Licha ya umuhimu wa kazi hiyo, bado ni kazi hatari zaidi duniani. Tangu mwezi Agosti mwaka 2003, zaidi ya wafanyakazi 4,500 wa huduma za kibinadamu wameuawa, au wamejeruhiwa au hata kushambuliwa na kushikiliwa kinyume cha sheria wakati wakiwa kazini. Umoja wa Mataifa unasema wahudumu wa kibinadamu wanawake wako hatarini zaidi kuporwa, kufanyiwa ukatili wa kingono na ghasia nyingine nyingi.

20 August 2019, 15:21