Cerca

Vatican News
Tanzania na Misri ni nchi ambazo zinapania kwa sasa kudumisha ushirikiano katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wao! Tanzania na Misri ni nchi ambazo zinapania kwa sasa kudumisha ushirikiano katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wao!  (AFP or licensors)

Tanzania na Misri kuendelea kuimarisha ushirikiano kati yao!

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Misri Abdel Fattah Al- Sisi, ambapo wametumia fursa hiyo kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi za Tanzania na Misri. Pia Waziri Mkuu amemfikishia Rais wa Misri salamu kutoka kwa Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Na Mwandishi Maalum kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Cairo, Misri.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Misri Abdel Fattah Al- Sisi, ambapo wametumia fursa hiyo kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi za Tanzania na Misri. Mbali na kuzungumzia masuala hayo ya kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kisiasa, kiuchumi na kijamii, pia Waziri Mkuu amemfikishia Rais wa Misri salamu kutoka kwa Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli. Mazungumzo baina ya Waziri Mkuu na Rais wa Misri yamefanyika Jumatano, Julai 10, 2019 Ikulu jiji Cairo, ikiwa ni katika siku ya tatu na ya mwisho ya ziara yake ya kikazi nchini Misri.

Katika ziara hiyo ameambatana na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga. Waziri Mkuu amemaliza ziara yake ya kikazi nchini Misri ambapo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Cairo ameagwa na Waziri wa Kilimo na Uhaulishaji wa Ardhi wa Misri, Dkt. Ezz Eldien Abo Setit. Akiwa ziarani nchini Misri, Waziri Mkuu alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Misri, Dkt. Mostafa Madbouly katika siku yake ya kwanza ya ziara yake, ambapo aliwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Misri waje kuwekeza nchini. Pia, Waziri Mkuu alitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo nchini humo ambayo ni pamoja na mradi wa ujenzi wa makao makuu mapya ya nchi hiyo, mradi wa awamu ya pili ya upanuzi wa mfereji wa Suez Canal na kiwanda kikubwa cha ngozi.

Wakari huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali kutoka Misri ikiwemo kampuni ya “Cairo for Investment and Development” inayoshughulika na usimamizi wa kiwanda cha ngozi waje kuwekeza nchini Tanzania. Ametoa kauli hiyo Jumanne, Julai 9, 2019 alipotembelea kiwanda kikubwa cha ngozi cha Robbiki kilichoko katika mkoa wa Sharkia nchini Misri, ambapo alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji hao waje wawekeze nchini kwani kuna malighafi za kutosha. Waziri Mkuu akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi nchini Misri alisema Tanzania ina mifugo mingi hivyo inahitaji wawekezaji watakaojenga viwanda vya kuchakata bidhaa mbalimbali zitokanazo na mifugo hiyo ikiwemo ngozi.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imeboresha mazingira ya biashara na ya uwekezaji pamoja na kusimamia uwajibikaji kwa watumishi wa umma, hivyo Tanzania ni mahali bora na salama kwa wawekezaji na wafanyabiashara. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kampuni ya “Cairo for Investment and Development” ya nchini Misri, ambayo inasimamia kiwanda cha ngozi cha Robbiki, Yasser Mohamed Ahmed Al Maghraby alisema kiwanda hicho kinauhitaji mkubwa wa ngozi kutoka Tanzania. Awali, Waziri Mkuu alitembelea mradi mkubwa wa mabwawa ya kufugia samaki, mradi wa upanuzi wa awamu ya pili ya mfereji wa suez canal, ambapo aliipongeza Serikali ya Misri kwa ujenzi wa mradi huo mkubwa kwa kutumia fedha za ndani (Dola bilioni 8.2).

11 July 2019, 10:18