Tafuta

Vatican News
Serikali ya Tanzania inalipongeza Kanisa la TAG kwa kusherehekea Miaka 80 tangu kuanzishwa kwake na Miaka 10 ya Mpango Mkakati wa Mavuno. Serikali ya Tanzania inalipongeza Kanisa la TAG kwa kusherehekea Miaka 80 tangu kuanzishwa kwake na Miaka 10 ya Mpango Mkakati wa Mavuno. 

Serikali ya Tanzania yalipongeza Kanisa la TAG: Miaka 80 ya huduma kwa watanzania!

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amelipongeza Kanisa la "Tanzania Assemblies of God, TAG" kwa kuadhimisha Miaka 80 tangu kuanzishwa kwake na Miaka 10 ya Mpango Mkakati wa Mavuno, kama sehemu ya mchakato wa huduma makini kwa familia ya Mungu nchini Tanzania. Kanisa la TAG linaipongeza pia serikali ya awamu ya tano kwa kujizatiti katika maendeleo makini.


Na Mwandishi Maalum, Ofisi ya Waziri Mkuu, - Arusha.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amelipongeza Kanisa la “Tanzania Assemblies of God” kwa kuthamini na kutambua kazi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano. “Baba Askofu Mtokambali umenifurahisha kwa takwimu ulizozitaja hapa za miradi mikubwa ambayo inatekelezwa na Serikali hii. Kuna wengine hawapendi kusikia mambo kama haya, hongera sana,” amesema. Ametoa pongezi hizo Jumapili, Julai 21, 2019 wakati akizungumza na maelfu ya waamini wa Kanisa hilo katika maadhimisho ya miaka 80 ya TAG nchini Tanzania yaliyofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha. Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli, amesema ameguswa na jinsi kanisa hilo linavyomtambua Mheshimiwa Rais na wasaidizi wake na kuthamini juhudi za Serikali. 

“Serikali hii imedhamiria kuwatumikia Watanzania wote bila kujali dini zenu, rangi wala itikadi za kisiasa. Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya awamu ya tano itaendelea kumtegemea Mungu pasipo shaka yoyote.” Pia amewapongeza viongozi wa kanisa hilo kwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chote cha miaka 80. "Pia nikupongeze Baba Askofu kwa kuchangia mifuko 1,000 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari hapa Arusha. Natambua kwamba ulishachangia mifuko mingine 500, asante sana." Alilishukuru Kanisa hilo kwa kuendesha maombi maalum kwa ajili ya Taifa yaliyoongozwa na Mchungaji Titus Mkama. "Niliguswa sana wakati maombi ya Taifa yalipokuwa yakiendelea. Mchungaji aligusia masuala ya muhimu kwa Taifa hili."

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na maelfu ya washirika waliohudhuria maadhimisho hayo, Askofu Mkuu wa TAG, Dk. Barnabas Mtokambali alisema anamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa kulipenda na kulijali Kanisa hilo. Alimpongeza Rais Magufuli kwa miradi mikubwa ya maendeleo anayoisimamia kama vile: Umeme wa Stiegler's Gorge, Reli ya SGR, ununuzi wa ndege, ujenzi wa hospitali mpya 67 za wilaya, ujenzi wa vituo vya afya 370 na ununuzi wa dawa za hospitali. "Nina umri wa kutosha lakini katika miaka yangu yote hii, sijawahi kuona hospitali 67 zikijengwa kwa pamoja. Tena, mwaka huu wa fedha mmetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali nyingine 27. Hongera sana kwa ujasiri huo," alisema Dkt. Mtokambali.  Maadhimisho ya miaka 80 ya TAG yameenda sambamba na hitimisho la miaka 10 ya Mpango Mkakati wa mavuno.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watoto wa kike wasikubali kudanganywa na wanaume na badala yake wakazanie masomo hadi wahitimu elimu ya juu. “Wasichana wote mliopo hapa, mwanaume yeyote akikufuatafuata mwambie usinusumbue; mwambie niache nisome. Kamwe msikubali kudanganyika, someni hadi mmalize Chuo Kikuu,” alisema.  Ametoa wito huo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wakazi wa wilaya za Same na Mwanga akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo mkoani Kilimanjaro.  Waziri Mkuu ambaye alikuwa na ziara ya siku nne mkoani humo, amewaonya vijana na wazee ambao wana tabia ya kuweka mahusiano ya kimapenzi na watoto wa kike kwamba waache mara moja la sivyo wataishia jela. 

“Wanaume msisahau kwamba mtoto wa mwenzio ni wako. Nataka niwakumbushe kuwa ukimwona mtoto wa kike, muache. Huyo ni moto wa kuotea mbali. Ukimchumbia, ukimuoa, au kumpa mimba mtoto wa kike, ujue kuwa miaka 30 jela ni yako.” “Serikali ya awamu ya tano, imeamua kuwekeza kwa mtoto wa kike, kwa hiyo tunataka watoto wa kike wakianza shule ya awali, wasome shule ya msingi, waende sekondari hadi wamalize Chuo Kikuu,” alisisitiza.  Katika ziara hii, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Bashay, wilayani Karatu watumie fursa zinazojitokeza kwenye sekta ya utalii kuboresha maisha yao. “Tumieni fursa ya uwepo wa eneo hili.

Halmashauri wakishajenga vizimba vya biashara, leteni bidhaa zenu kama vile picha za tingatinga, mapambo, vinyago na vyakula vya asili ili watalii wakija hapa wapate huduma kutoka kwenu,” alisema.  Ametoa wito huo Jumapili, Julai 21, 2019 wakati akizindua mradi wa ujenzi wa vituo vya polisi vya kupunguza changamoto kwa magari ya utalii barabarani na kukabidhi gari la polisi kwa ajili ya patrol ya watalii katika eneo la Bashay, wilayani Karatu, mkoani Arusha. Waziri Mkuu alizindua kituo cha kutolea huduma za usalama kwa watalii wilayani Karatu ikiwa ni ishara ya kuwakilisha vituo vingine vitatu vinavyoendelea kujengwa mkoani Arusha katika maeneo ya Kikatiti (Arumeru), Makuyuni (Monduli) na Engikaret (Longido).

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasihi wakazi hao wawalinde watalii ili waitangaze vema nchi ya Tanzania pindi wakirudi makwao. “Ili kukuza na kutangaza utalii, tunapaswa tuwe na mapenzi mema kwa watalii lakini kikubwa zaidi ni usalama wao.” Aliwataka wakazi hao waendelee kuiamini Serikali ya awamu ya tano na waendelee kumuombea Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili apate nguvu ya kuleta maendeleo zaidi. Pia aliwashukuru viongozi wa Tanzania Association of Tour Operators (TATO) kwa kuchangia ujenzi wa vituo hivyo na kutoa gari jipya la polisi kwa ajili kituo hicho cha Karatu. Gari hilo aina ya Toyota Landcruiser lililogharimu dola za Marekani 45,000, limepewa namba za usajili za PT 4190.

 Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wakazi wa Bashay waliohudhuria hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo alisema ujenzi wa vituo hivyo umetokana na malalamiko aliyopokea kwamba watalii wakitoka Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) hadi kufika Karatu wanakuwa wamesimamishwa njiani zaidi ya mara 20. “Tulijiuliza hawa watalii wamekuja kutalii, wanataka kupumzika, sasa ni kwa nini wasumbuliwe kiasi hicho? Tuliamua kuanzisha vituo vya aina hii, ili watalii wafanyiwe ukaguzi kwenye check-points maalum,” alisema. Aliomba Jeshi la Polisi liwapange barabarani askari ambao ni weledi na wana uelewa wa masuala ya utalii na kutolea mfano wa wiki iliyopita ambapo alikuwa akitokea mjini kwenda Karatu na kukuta magari ya watalii zaidi ya 10 yamesimamishwa njiani.

“Niliona baadhi yao wakiwa wamelala kwenye magari kwa uchovu, nilipowauliza wamekalishwa kwa muda gani, walisema ni kwa zaidi ya dakika 45. Nilipomuuliza askari aliyewasimamisha ni kwa nini anafanya hivyo, akanijibu kwamba dereva amemjibu vibaya. Hivi ni kwa nini watalii wateseke juani wakati mwenye makosa ni dreva?” Naye, Makamu Mwenyekiti wa TATO, Bw. Henry Kimaro aliishukuru Serikali kwa jitihada inazofanya za kupambana na ujangili na kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini. “Tumeona hivi karibuni watalii wengine kutoka Israel, China na sasa ndege yetu imeanza kwenda India kuwafuata hukohuko,” alisema. Alisema wameanza na vituo hivyo vinne mkoani Arusha lakini tatizo hilo liko maeneo mengi nchini na wao hawawezi kufika nchi nzima kutoa huduma kama hiyo. Hivyo, alimuomba Waziri Mkuu awahimize Wakuu wa Wilaya ambao wilaya zao zinajihusisha na sekta ya utalii, waige mfano wa wilaya ya Karatu ili kuhakikisha usalama wa watalii wawapo nchini.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe ulioko Kirya, wilayani Mwanga, na kukagua hatua mbalimbali za ujenzi wa mradi huo. Waziri Mkuu amekagua ujenzi huo Jumamosi, Julai 20, 2019 na kutoa maelekezo kadhaa ili kuharakisha ujenzi wa mradi ambao umekuwa ukiendelea kwa muda mrefu sasa. Akizungumza na wakazi wa Kirya, Nyumba ya Mungu na vijiji vilivyo jirani na eneo la mradi, Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kutoa fedha hatua kwa hatua ili kukamilisha mradi huo. Waziri Mkuu amewataka wakazi hao waache kutumia uvuvi haramu na badala yake, wavue samaki kwa kutumia njia halali. “Bwawa la Nyumba ya Mungu linagusa wilaya tatu za Mwanga, Simanjiro na Moshi Vijijini. Ninataka Serikali za wilaya husika zisimamie jambo hilo,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwagiza Afisa Elimu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bibi Pauline Nkwama amsimamie Afisa Elimu wa Wilaya hiyo anayeshughulikia elimu ya msingi, Bibi Mariana Mgonja na kuhakikisha kuwa anawahamishia walimu kwenye shule mbili za Kirya ambazo zilikuwa na walimu wawili wakati zina wanafunzi zaidi ya 400 kila moja. “Afisa Elimu Mkoa hakikisha Afisa Elimu ya msingi katika wilaya hii anahamisha walimu kutoka pale mjini na kuwaleta huku ili huku vijijini kuwe na walimu sita katika kila shule.  Waziri Mkuu alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mwanga, Bw. Zephrin Lubuva awatafutie gari walimu watakaohamishiwa huko ili wafike mapema. Amechukua hatua hiyo, baada ya kuelelezwa na mbunge wa jimbo hilo, Profesa Jumanne Maghembe kwamba katika eneo hilo kuna shule mbili ambazo zina walimu wawili wakati kuna madarasa nane, yaani la awali moja na ya msingi saba, na wanafunzi zaidi ya 400. Alizitaja shule hizo kuwa ni Kiti cha Mungu na Emangulai.

Mapema, akitoa taarifa kuhusu mradi huo, msimamizi wa mradi huo Mhandisi Richard Magwizi alimweleza Waziri Mkuu kwamba Serikali inatekeleza mradi huo ili kuondoa kero ya maji inayowakabili wakazi wa miji ya Same na Mwanga na vijiji 38 vilivyo katika eneo la mradi. Alisema mradi huo utakapokamilika, unatarajiwa kunufaisha wananchi 438,931 katika Wilaya za Same (246,793), Mwanga (177,085) na Korogwe (15,053). Alisema mradi huo umegawanywa katika awamu mbili za utekelezaji na unakadiriwa kugharimu dola za Marekani milioni 300. “Awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa miundombinu ya uzalishaji wa maji safi na kusambaza maji kwa wakazi wa Mji wa Same na Mji wa Mwanga na vijiji 9 vilivyo kandokando ya chanzo cha maji. Awamu ya pili itahusisha ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa maji katika vijiji 29,” alisema. Akielezea changamoto zinazowakabili, Mhandisi huyo alisema wana changamoto ya kuchelewa kwa malipo ya mkandarasi kutokana na uwiano wa uchangiaji ambapo Serikali inagharimia asilimia 50.18. “Malipo yanapochelewa, yanaathiri kasi ya utekelezaji,” alisema.

22 July 2019, 11:41