Tafuta

Vatican News
Tarehe 11 Juni Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani umezindua mkakati jumuishi wa watu walemavu katika Mkutano wa 12 wa nchi wanachama wa mkataba wa watu wenye ulemavu,CRPD Tarehe 11 Juni Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani umezindua mkakati jumuishi wa watu walemavu katika Mkutano wa 12 wa nchi wanachama wa mkataba wa watu wenye ulemavu,CRPD   (AFP or licensors)

Kisarawe na Kibaha,Tanzania ni mfano wa mafanikio ya sera jumuishi kwa wenye ulemavu katika nyanja ya elimu!

Tarehe 11 Juni Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani umezindua mkakati jumuishi wa watu walemavu katika Mkutano wa 12 wa nchi wanachama wa mkataba wa watu wenye ulemavu,CRPD.Na Wilaya za Kisarawe na Kibaha nchini Tanzania zimetajwa kuwa mfano wa mafanikio ya sera jumuishi kwa wenye ulemavu katika nyanja ya elimu kwa mujibu wa Bwana Jimmy Innes,Afisa Mtendaji Mkuu wa shirika la kiraia,ADD linalosaidia kujenga uwezo wa mashirika ya watu wenye ulemavu.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Ikiwa ni siku ya Pili ya Mkutano wa 12 wa nchi wanachama wa mkataba wa watu wenye ulemavu, (CRPD) kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani,wilaya za Kisarawe na Kibaha mkoani Pwani nchini Tanzania zimetajwa kuwa mfano wa mafanikio ya sera za ujumuishi wa watu wenye ulemavu katika nyanja ya elimu. Bwana Jimmy Innes, Afisa Mtendaji Mkuu wa shirika la kiraia, ADD linalosaidia kujenga uwezo wa mashirika ya watu wenye ulemavu, ametaja mafanikio hayo akihojiwa na  waandishi wa habari wa Umoja wa Mataifa, kandoni mwa mkutano huo ambapo Bwana Innes amesema katika wilaya hizo za Kibaha na Kisarawe,  wamefanya kazi kwa zaidi ya miaka mitatu, na taratibu wanapiga hatua ndogo ndogo moja kwa moja mpaka wamefika hatua ambayo viongozi wa halmashauri wameelewa kitu kinachoitwa elimu jumuishi. Pia amesema kuwa  kwa sasa wamefikia wakati viongozi wa halmashauri wenyewe wanaanza kuahidi na kutekeleza bajeti ya elimu jumuishi inaongezeka kutoka katika mfuko wa halmashauri. Na kwa maana hiyo Bwana Innes amethibitishwa kwamba hiyo ni hatua kubwa sana!

Shirika la Kimataifa la kiraia linataka kusema nini katika mkutano?

Kuhusu ujumbe  wa shirika la Kimataifa la kiraia (ADDI) katika mkutano wa wiki mbili, Bwana Innes amesema, “tunasema kwamba haki za watu wenye  ulemavu, ni lazima tujenge uwezo wa watu wenye ulemavu ili kudai haki zao wenyewe. Si kwamba haki ni kitu cha kupewa, hapana! Haki ni kitu cha kudai wewe mwenyewe upate haki yako. Kwa  hiyo ujumbe wetu katika mkutano huu na mapambano ya haki kwa jumla ni lazima tuwape watu nafasi waweze kudai haki zao wenyewe.” Aidha alipoulizwa amelipokea kwa namna gani  hatua ya Umoja wa Mataifa kutangaza mkakati wake wa ujumuishaji watu wenye ulemavu kuanzia kwenye ofisi zake za makao makuu hadi mahalia, Bwana Innes amesema: “kwa upande mmoja najisikia vizuri kuwa Umoja wa Mataifa umechukua hatua hiyo, lakini tunajiuliza mwaka huu wa 2019 mpaka leo ndio umezindua mkakati huo? Hapana si kwamba umechelewa lakini tunatakiwa kufanyia kazi kwa dhati.”

Usinduzi wa mkakati wake wa kujumuisha watu wenye ulemavu katika nyanja zote

Hata hivyo kuhusiana na mkutano huo, tarehe 11 Juni 2019, Umoja wa Mataifa  umezindua mkakati wake wa ujumuishi wa watu wenye ulemavu katika nyanja mbalimbali, kama mojawapo ya hatua za kutekeleza kwa vitendo kwa mfano ahadi yake ya kutomwacha nyuma mtu yeyote kwenye utekelezaji wa ajenda 2030. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametangaza uzinduzi huo  kwenye makao makuu ya umoja huo jijini New York, Marekani wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 12 wa nchi wanachama wa mkataba wa haki za watu wenye ulemavu, CRPD unaotarajiwa kufanyika kwa wiki mbili. Bwana Guterres amethibitisha juu ya  msingi wa kuanzisha mkakati huo kwamba  ni baada ya ripoti iliyodhihirisha kuwa hali ya ujumuishi wa watu wenye ulemavu ndani ya chombo hicho inatisha, kuanzia makao makuu hadi katika ofisi za uwakilishi wa chombo hicho akisema kuwa kuna kutokuelewa ni jinsi gani Umoja huo unapaswa kutekeleza majukumu yake kuhusiana na ujumuishi. Amegusia pia mantiki ya uamuzi wa kuanzisha mkakati huo kwamba  ni maneno ya msichana mkimbizi mwenye mtindio wa ubongo kutoka Syria Nujeen Mustapha ambaye alipohutubia Baraza la Usalama wiki chache zilizopita alitaka kauli ya Umoja wa Mataifa ya hakuna mtu kuachwa nyuma itekelezwe kwa vitendo na si maneno tu, akisisitiza kuwa katu hawawezi kusubiri zaidi.

Huu si mkakati wa maneno ni mkakati wa vitendo

Ni kwa kuzingatia hayo Katibu Mkuu amesema,“huu si mkakati wa maneno, ni mkakati wa vitendo, hatua za kuongeza viwango vya utendaji vya Umoja wa Mataifa kuhusu ujumuishaji wa watu wenye  ulemavu katika ngazi zote na hatua za kuleta mabadiliko ya pamoja na ya dhati tunayohitaji.” Amesema mkakati unataka ufuatiliaji na uwajibikaji na ukiangazia maeneo muhimu ikiwemo uongozi, mipango, upatikanaji wa huduma na kutoa wito kwa watu wenye ulemavu kufanya kazi na Umoja wa Mataifana wapatiwe usaidizi zaidi. Bwana Guterres amesema: “nataka Umoja wa Mataifa uwe ni mwajiri anayechaguliwa na watu wenye ulemavu. Nataka operesheni zetu za kibinadamu, maendeleo na amani zitambue na zihamasishe haki za watu wenye ulemavu. Ni lazima Umoja wa  Mataifa uwe wa kila mtu kwa maana ni jambo rahisi sana. Hatuwezi kuwa jukwaa la mabadiliko wakati  watu wenye ulemavu hawawezi kupata fursa ya jukwaa la kuzungumza. Nategemea kuungwa mkono thabiti  kutoka kwa nchi wanachama ili kuhamasisha mkakati huu”.

12 June 2019, 12:22