Tafuta

Vatican News
Miaka 100 ya Shirika la Kazi Duniani, ILO: Changamoto kubwa ya maendeleo ya teknolojia na hofu ya kukosekana kwa fursa za ajira duniani! Miaka 100 ya Shirika la Kazi Duniani, ILO: Changamoto kubwa ya maendeleo ya teknolojia na hofu ya kukosekana kwa fursa za ajira duniani!  (AFP or licensors)

Miaka 100 ya Shirika la Kazi Duniani, ILO na changamoto zake!

Umoja wa Mataifa: Sekta ya kazi haina budi kujikita katika ubunifu ili kuimarisha uchumi fungamani na kusonga mbele katika mchakato wa malengo endelevu ya binadamu! Mabadiliko katika mfumo wa kazi, mahusiano katika maeneo ya kazi pamoja na umuhimu wa mapumziko kwa wafanyakazi ni mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa, ili kuongeza tija na ufanisi kazini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani, maarufu kama Mei Mosi, huku kukiwa na changamoto kubwa kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yanayotishia fursa za ajira kwa mamilioni ya watu duniani. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Kazi Duniani, ILO, Katibu  mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alikazia umuhimu wa sekta ya kazi duniani kujikita katika ubunifu ili kuimarisha uchumi na kupiga hatua katika mchakato wa malengo endelevu na fungamani ya binadamu!Mabadiliko katika mfumo wa kazi, mahusiano na mafungamano katika maeneo ya kazi pamoja na umuhimu wa mapumziko kwa wafanyakazi ni mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa, ili kuongeza tija na ufanisi kazini.

Mabadiliko makubwa yanayoendelea kujitokeza katika maeneno ya kazi, ni tishio kwa wafanyakazi wengi duniani, kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu itakayowaandaa vijana wa kizazi kipya kukabiliana kikamilifu na changamoto za fursa za kazi na ajira kwa sasa na kwa siku za usoni! Sera na mikakati makini ya kiuchumi ni muhimu, ili kuwahakikishia usalama, ustawi na maisha bora wale wanaoweza kuathirika kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia maeneo ya kazi! Hii ni changamoto pevu, inayopaswa kuvaliwa njuga na Serikali pamoja na wadau mbali mbali katika sekta ya uchumi, uzalishaji na huduma.

Dunia inaendelea kujiimarisha katika mfumo wa kidigitali, hali ambayo inatishia kwa kiasi kikubwa fursa za kazi na ajira kwa watu wengi. Kumbe, hapa wafanyakazi wanapaswa kujiongeza, ili kukabiliana na changamoto hii, vinginevyo, maandamano ya wafanyakazi kudai fursa za kazi yataendelea kila kukicha pamoja na kuwaacha vijana wengi wakiwa wamesimama “vijiweni.” Kwa upande wake Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Maria Fernanda Espinosa, amekumbusha kwamba zaidi ya watu milioni 40 wameathiriwa na mifumo ya utumwa mamboleo na kwamba watu milioni 190 hawana ajira ikiwemo theluthi tatu ambao ni vijana.  "Watu milioni 300 walioajiriwa ni maskini kote ulimwenguni na nusu yao ni vijana. Aidha watu bilioni 2 wanafanya kazi katika sekta isiyo rasmi kwa kawaida bila ulinzi wa jamii," amesema Bi. Espinosa.

Ni katika muktadha huu, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, inafikia lengo namba 8 la Malengo ya Maendeleo Endelevu, kwa kutoa ajira bora zaidi, ili kupambana na baa la umaskini duniani sanjari na ukosefu wa haki. Katika mchakato wa maboresho ya teknolojia na fursa za kazi na ajira, pasiwepo hata mtu mmoja anayeachwa nyuma ya maendeleo haya. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inawajengea uwezo: wanawake, vijana, makundi ya watu asilia pamoja na walemavu, ili kupambana kikamilifu na changamoto za maisha kwa sasa na kwa siku za mbeleni!

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kazi Duniani, ILO, Guy Ryder anasema maadhimisho ya Jubilei ya Miaka mia moja ni fursa makini sana kwa Shirika la Kazi Duniani kutathmini mustakabali wake. Hii inatokana na ukweli kwamba, mazingira ya kazi yanapitia katika mabadiliko makubwa sana, kiasi cha kuibua hisia za hofu na wasi wasi kwa sasa na kwa siku za usoni. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia hayana budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu! Rasilimali watu ni muhimu katika maendeleo ya uchumi fungamani katika maisha ya binadamu!

Mei Mosi: Wafanyakazi
01 May 2019, 14:26