Tafuta

Tarehe 2-3 Mei 2019 linafanyika Jukwaa la Muungano wa Ustaarabu Jijini Baku nchini Azerbaijan kwa lengo la kuhamasisha kuishi kwa amani kwa maana inawezekana! Tarehe 2-3 Mei 2019 linafanyika Jukwaa la Muungano wa Ustaarabu Jijini Baku nchini Azerbaijan kwa lengo la kuhamasisha kuishi kwa amani kwa maana inawezekana! 

Jukwaa la Muungano wa Ustaarabu:Inawezekana kuishi pamoja kwa amani duniani!

Jukwaa la muungano wa ustaarabu limefunguliwa jijini Baku,Azerbaijan tarehe 2-3 Mei 2019. Ni muhimu kufikisha ujumbe mzito kwa jumuiya ya kimataifa kuwa “inawezekana kuishi pamoja kwa amani na kuelewa tofauti za tamaduni na dini” kwa mujibu wa Miguel Angel Moratinos mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kwa ajili Muungano wa ustaarabu UNOAC.

Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Kuishi pamoja kwa amani ni jambo linalowezekana, lakini kurejea kwa kile kinachoitwa chuki, kunatia hofu kubwa ya utangamano. Kauli hiyo imetolewa na Miguel Angel Moratinos ambaye ni mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kwa ajili Muungano wa ustaarabu UNOAC  mjini Baku Azerbaijan ambako tarehe 2 Mei 2019 wamefungua  jukwaa la Umoja wa Mataifa kuhusu “majadiliano ya hatua dhidi ya ubaguzi, kutokuwepo kwa usawa na migogoro.” Bwana Moratinos amesema jukwaa hilo la tano la kimataifa limekuja katika wakati mwafaka kwani ”Chuki ni neno linalochagiza jamii nyingi kusambaratishwa, inawafanya watu kufikia hatua ya kutoweza kuishi pamoja katika mwelekeo wa kuwatokomeza wapinzani wao na hii ni hatari kubwa.” Hata hivyo amesisitiza kuwa jukwaa hilo la muungano wa ustaarabu ni muhimu kufikisha ujumbe mzito kwa jumuiya ya kimataifa kuwa “inawezekana kuishi pamoja na kwamba tunaweza kuheshimiana na tunapaswa kuelewa vyema tofauti za tamaduni na dini.”

Dunia inazidi kuingia katika hali ya sintofahamu na hivyo mkakati wa kimataifa kwa ajili ya majadiliano ya tamaduni mbalimbali

Aidha Moratinos amesema dunia inazidi kuingia katika hali ya sintofahamu na hivyo mkakati wa kimataifa kwa ajili ya majadiliano ya tamaduni mbalimbali ni ya muhimu sasa kuliko wakati mwingine wowote. Ameongeza kuwa suluhu kupitia fedha, njia za kijeshi na njia za kisiasa inachukuwa mtazamo rahisi, lakini suluhisho la kudumu na endelevu “ linahitaji mtazamo wa kijamii na kitamaduni na ambao utachimba mizizi ya jamii mbalimbali ili kuweka hali halisi bayana. Hadi pale utakapoelewa mtazamo wa jirani yako, historia ya suala la chuki, jinsi gani umeingia katika mazingira hayo, yana athari gani na uhusiano uliopo, itakuwa vigumu sana kupata suluhu endelevu.” Jukwaa hilo la kimataifa la siku mbili litakalokunja jamvi tarehe 3 Mei 2019  linatathimini kwa kina jukumu muhimu la majadiliano ya tamaduni tofauti kama mkakati wa hatua kwa ajili ya ujenzi wa mshikamano na kuzisaidia jamii kukabiliana na machafuko na ubaguzi katika jamii mchanganyiko. Kongamano hilo limewaleta pamoja washiriki zaidi ya 450 kutoka mashirika ya kimataifa, Umoja wa Mataifa, wawakilishi wa nchi, taasisi za kidini na asasi za kiraia.

Kongamano kwa ajili ya kukabiliana na hotuba za chuki ili kulinda vikundi vidogo vya kidini, wakimbizi na wahamiaji 29 Aprili-Mei Mosi

Sambamba na Jukwaa hili hata  Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uzuiaji wa mauaji ya kimbari, Adama Dieng ameonya dhidi ya zama za nyakati ngumu na za hatari za leo. Bwana Dieng akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, Mei Mosi 2019 kwenye kongamano kwa ajili ya kukabiliana na hotuba za chuki ili kulinda vikundi vidogo vya kidini, wakimbizi na wahamiaji, ametoa wito wa kukabiliana na kutovumiliana akitoa mfano wa mashambulizi ya hivi karibuni katika sehemu za ibada ikiwemo mauaji katika msikiti wa Christchurch New Zealand, mashambulizi ya makanisa Sri Lanka na mashambulizi ya hivi karibuni katika hekalu Marekani.

Mjumbe maalum huyo amesema, “kile ambacho kimefanyika hivi majuzi kimesababisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kusisitiza umuhimu wa kukabiliana na hotuba za chuki.” Bwana Dieng ameongeza kuwa, wakimbizi na wahamiaji leo ni miongoni mwa walengwa, sababu tu ya utambulisho wao, akiongeza kuwa  “tunahitaji kuangalia vichocheo vya hali hii inayoshuhudiwa, ambayo kwa bahati mbaya inatukumbusha miaka ya 1930 wakati bara Ulaya, wayahudi waliochukuliwa kama wanayama na kulaumiwa kwa majanga mengi ikiwemo, mwelekeo wa kiuchumi wa wanyonge.” Halikadhalika amesema dunia iko katika wakati muhimu katika vita dhidi ya chuki na misimamo mikali ambapo amesema, “hotuba za aina hii tunzozisikia leo hii katika miji mingi barani Ulaya ni hatari.”

Hotuba za kueneza chuki na mitizamo hasi dhidi ya wageni ni ishara ya hatari

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, hotuba za aina hiyo na mitizamo hasi dhidi ya wageni ni ishara kwamba dunia iko katika wakati muhimu kukabiliana na chuki na misimamo mikali wakati huu kukishuhudiwa mwamko wa makundi yanayounga mkono misimamo na uhusiano na manazi wa kisasa. Ni katika muktadha huu ambapo kongamano hilo la dini, amani na usalma limefanyika likimulika wakimbizi na wahamiaji, kwani, “kwa sababu leo, kundi la watu hawa wanatishiwa, ameonya bwana Dieng. Bwana Dieng amekumbusha kwamba hotuba za aina yoyote ambazo zinazua ubaguzi au chuki kwa misingi ya kidini zinapaswa kupingwa, “na kama alivyosema Katibu Mkuu, Antonio Guterres, tunahitaji kuhakikisha kwamba mitandao ya kijamii sio kivuli cha hatuba za aina hiyo.”

02 May 2019, 16:14