Tafuta

Vatican News
Mfalme Mohammed VI wa Morocco asema, dini zina wajibu wa kukuza na kudumisha: haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa! Mfalme Mohammed VI wa Morocco asema, dini zina wajibu wa kukuza na kudumisha: haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa!  (ANSA)

Hija ya Papa Francisko Morocco: Hotuba ya Mfalme Mohammed VI

Mfalme Mohammed VI anasema, katika amana na urithi wake wa maisha ya kiroho, Morocco imeendelea kutangaza na kushuhudia udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika majadiliano ya kidini na uhuru wa kuabudu. Majadiliano ya kidini yanapaswa kusimikwa katika mchakato wa maridhiano kati ya watu wa Mataifa, ili kufahamiana na kusaidiana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya 28 ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa nchini Morocco kuanzia tarehe 30-31 Machi 2019 imeongozwa na kauli mbiu“Papa Francisko mhudumu wa matumaini Morocco 2019”. Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Morocco, Jumamosi, tarehe 30 Machi 2019 amekumbushia kuhusu uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Morocco, ulioboreshwa zaidi kwa hija ya kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1985, wakati wa maadhimisho ya Mwaka wa Vijana Kimataifa. Uhusiano huu umeimarishwa zaidi kwa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Morocco, kama mhudumu wa matumaini.

Morocco ni daraja la mawasiliano ya maisha ya kiroho na kitamaduni; mambo msingi yanayojikita katika majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini ya Kiislam na Wakristo. Ni daraja la mawasiliano kati ya Bara la Afrika na Ulaya; changamoto na mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali kuheshimiana, kuthaminiana na kuishi kwa umoja, amani na utulivu kama ndugu. Katika amana na urithi wake wa maisha ya kiroho, Morocco imeendelea kutangaza na kushuhudia udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika majadiliano ya kidini na uhuru wa kuabudu. Majadiliano ya kidini yanapaswa kusimikwa katika mchakato wa maridhiano kati ya watu wa Mataifa, ili kufahamiana na kusaidiana.

Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco anaendelea kufafanua kwamba, Dini mbali mbali duniani zinapaswa kukuza na kudumisha amani, kwa kutambua kwamba, binadamu wote ni ndugu wamoja kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Elimu ya dini, maadili na utu wema ni mambo msingi ambayo viongozi wa dini wanapaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya, ili kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, inayohatarisha umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii. Taasisi ya Mohammed V ilijengwa kwa ajili ya kuwalea na kuwafunda viongozi na wahubiri wa dini ya Kiislam nchini Morocco.

Mfalme Mohammed VI wa Morocco anasema, anaunga mkono tasaufi ya Baba Mtakatifu Francisko katika kusimamia, kulinda na kudumisha mafao ya wengi; kwa kujikita katika huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, daima yuko tayari kusamehe. Morocco kwa kusukumwa na tasaufi juu ya Mungu ambaye ni upendo,  katika kipindi cha miaka 14 iliyopita, ilianzisha mchakato wa maboresho ya maisha ya wananchi maskini, kwa kuwawezesha kujenga makazi bora zaidi pamoja na kuendelea kudumisha mshikamano na wakimbizi pamoja na wahamiaji.

Morocco imeridhia Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018 “Global Compact 2018”, uliotiwa mkwaju tarehe 10 Desemba 2018 huko Marrakesh, Morocco. Mkataba huu unapania kuhakikisha kwamba mchakato wa uhamiaji unajikita katika: usalama, uratibu pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Jumuiya ya Kimataifa. Hii ni hatua kubwa kwani kwa mara ya kwanza katika historia, Jumuiya ya Kimataifa. Dini zinazomwabudu Mungu mmoja zinayo nafasi ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, maridhiano pamoja na maboresho msingi, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Mfalme Mohammed VI wa Morocco amempongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Injili ya amani, majadiliano ya kidini na kiekumene, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na mapambano dhidi ya umaskini, rushwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, yanayoendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao! Waamini wa dini mbali mbali duniani wanahimizwa kukita maisha yao katika tunu msingi za maisha ya kiroho; kwa kujenga madaraja ya kukutana na watu hata katika tofauti zao msingi!

Mfalme Mohammed VI
03 April 2019, 15:16