Tafuta

Vatican News
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ameibuka kidedea katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 23 Februari 2019 Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ameibuka kidedea katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 23 Februari 2019  (ANSA)

Rais Buhari aibuka kidedea, upinzani wapinga matokeo Nigeria!

Rais Muhammadu Buhari ameshinda uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Nigeria, kwa kupata asilimia 56% ya kura halali zilizopigwa na wananchi wa Nigeria. Rais Buhari ameongoza walau kwa asilimia 25 katika majimbo 24 kati ya majimbo 36 yaliyoko nchini Nigeria. Ushindi wa Rais Buhari umepingwa na Bwana Atiku Abubakar ambaye amejinyakulia asilimia 41% ya kura zote halali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini Nigeria, Bwana Mahmood Yakub imemtangaza Rais Muhammadu Buhari kuwa mshindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Nigeria, Jumamosi tarehe 23 Februari 2019 kwa kupata asilimia 56% ya kura halali zilizopigwa na wananchi wa Nigeria. Rais Buhari ameongoza walau kwa asilimia 25 katika majimbo 24 kati ya majimbo 36 yaliyoko nchini Nigeria. Ushindi wa Rais Buhari umepingwa na Bwana Atiku Abubakar ambaye amejinyakulia asilimia 41% ya kura zote halali zilizopigwa na kwamba, anatarajia kwenda Mahakamani kupinga ushindi huu kisheria!

Rais Buhari amekanusha madai haya kwa kusema: uchaguzi ulikuwa: huru na wa haki. Lakini angekuwa ameshinda kiongozi wa upinzani, ndiyo ungehesabika kuwa huru na haki! Hii ni dhana potofu katika ukuaji wa demokrasia Barani Afrika! Maoni yaliyotolewa na waangalizi wa uchaguzi kitaifa na kimataifa wanasema wameridhishwa na mwenendo mzima wa uchaguzi, hata kama kulikuwepo na kasoro ndogo ndogo! Uchaguzi umepita, sasa ni wakati wa kujenga Nigeria kwa ari na kasi kubwa zaidi!

Rais Muhammadu Buhari katika hotuba yake kwa wapambe wa Chama chake, amesikika akisema, huu ushindi wa demokrasia nchini Nigeria. Vipaumbele kwa awamu ya pili ya uongozi wake ni kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama pamoja mageuzi makubwa ya uchumi nchini Nigeria, bila kusahau mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, saratani inayosigina maisha ya wananchi wengi nchini Nigeria. Pamoja na mambo mengine, Rais Buhari amepania kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa, ili kisiwepo Chama au mwananchi wa Nigeria, anadhani kwamba, amegeuziwa kisogo nchini mwake!

Uchaguzi Mkuu Nigeria
01 March 2019, 12:33