Tafuta

Vatican News
Jumuiya ya Kimataifa inaomboleza vifo vya watu 157 waliopoteza maisha katika ajali ya Shirika la Ndege la Ethiopian Airlines, yumo Padre George Mukua, CMM. Jumuiya ya Kimataifa inaomboleza vifo vya watu 157 waliopoteza maisha katika ajali ya Shirika la Ndege la Ethiopian Airlines, yumo Padre George Mukua, CMM. 

Ajali ya Ndege ya Ethiopia: Yumo Sr. Wangari & Padre G. K. Mukua!

Wahanga wa ajali hii, wengi wao ni wale walioamini kwamba, hawawezi kubadili dunia, lakini wanaweza kuchangia katika mchakato wa maboresho ya maisha ya watu Barani Afrika! Hawa ni watu ambao ndani mwao, walisukumwa kwa namna ya pekee kabisa kushiriki kikamilifu kama mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wahitaji zaidi Barani Afrika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.- Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anaungana na viongozi wengine wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kutoa salam za rambi rambi kutokana na ajali ya ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopian Airlines iliyoanguka Jumapili tarehe 10 Machi 2019 na kusababisha watu 157 kupoteza maisha yao! Rais Sergio Mattarella wa Italia katika salam zake za rambi rambi anawakumbuka wote waliofariki dunia, wengi wao wakiwa ni wale waliokuwa wanasafiri kikazi kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa Kimataifa mjini Nairobi; baadhi ni watu waliojisadaka kwa ajili ya huduma ya maendeleo endelevu na fungamani pamoja na ushirikiano wa kimataifa.

Katika orodha hii, Kanisa linawakumbuka wote waliofariki dunia, lakini kwa namna ya pekee, Padre George Kagecha Mukua, CMM, wa Shirika la Wamisionari wa Mariannhill. Marehemu Padre Mukua alizaliwa tarehe Mosi, Januari 1979, huko nchini Kenya. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, kunako tarehe 2 Februari 2004 akafunga nadhiri za mwanzo na hatimate, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 30 Novemba 2017. Tarehe 10 Machi 2019, akakutana na Fumbo la kifo machoni pake! Watu wanakumbushwa kwamba, binadamu ni marehemu taraji! Katika ajali hii pia, Sr.  Florence Wangari wa Shirika la Wamisionari wa Bikira Maria Malkia wa Malaika kutoka Jimbo Katoliki la Nakuru, Kenya amefariki dunia. Sr. Wangari aliweka nadhiri zake za kawanza mwaka 2017 na alikuwa anarejea Kenya kubadilisha Pasipoti yake. Ujumbe, jiwekeni tayari kwani hamjui siku wala saa atakapokuja Mwana wa Adamu!

Wahanga wa ajali hii, wengi wao ni wale walioamini kwamba, hawawezi kubadili dunia, lakini wanaweza kuchangia katika mchakato wa maboresho ya maisha ya watu Barani Afrika! Hawa ni watu ambao ndani mwao, walisukumwa kwa namna ya pekee kabisa kushiriki kikamilifu kama mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ni akina Carlo Spin na mke wake Gabriela Vigian pamoja na Matteo Ravasio waliokuwa wanakwenda Sudan ya Kusini kupitia Nairobi, ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa Zahanati kubwa mjini Juba! Ndoto na matamanio ya maisha bora kwa wananchi wa Sudan ya Kusini, imezimika kwenye ajali hii!

Wakati huo huo,  Umoja wa Mataifa unasikitika kupoteza wafanyakazi wake 35 kwenye ajali hii. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP linaomboleza vifo vya wafanyakazi wake saba, waliokuwa wanakwenda kufanya kazi nje ya nchi na familia zao, ili kusaidia kuboresha hali ya chakula, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Katika orodha hii ya wafanyakazi kutoka katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa alikuwepo pia Bwana Victor Tsang, mtaalamu kutoka katika Mradi wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Mazingira, UNEP ambao uko chini ya ECOSOC, yaani Baraza la Kiuchumi na Jamii. Baraza hili linalo jukumu la kuhifadhi na kuboresha mazingira ya binadamu kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho! Itakumbukwa kwamba, Makao makuu ya UNEP yako Jijini Nairobi, nchini Kenya.

Nalo Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, linamwombolezea kwa namna ya pekee kabisa, Profesa Sebastiano Tusa kutoka Italia, bingwa na mtaalam aliyejisadaka sana kwa ajili ya kuhifadhi urithi wa kitamaduni uliohifadhiwa chini ya Bahari. UNESCO inasema, ni mtaalam aliyebahatika kushirikisha ujuzi wake kuhusiana na mambo ya kale na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Profesa Tusa alikuwa anaenda Malindi nchini Kenya, ili kushiriki mkutano kuhusu Maendeleo ya Utalii Afrika ya Mashariki, uliofunguliwa hapo tarehe 11 Machi 2019 kwa kuwakumbuka wale wote waliopoteza maisha kwenye ajali ya ndege ya Ethiopian Airlines!

Maombolezi Kimataifa
12 March 2019, 11:27