Tafuta

Vatican News
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Panama inasema, maandalizi yote yamekamilika, sasa ni sherehe ya vijana kwenda mbele! Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Panama inasema, maandalizi yote yamekamilika, sasa ni sherehe ya vijana kwenda mbele! 

PANAMA iko tayari kumpokea na kumkaribisha Papa Francisko!

Ni heshima kubwa kwa Panama, nchi ndogo kabisa huko Amerika ya Kati kupewa dhamana na wajibu wa kuandaa tukio hili la kimataifa. Lakini, ikumbukwe kwamba, tangu mwaka 2009 imekuwa ikijiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Uinjilishaji nchini Panama. Hii ni changamoto ya kusimama kidete pia kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jamhuri ya Watu wa Panama inayoheshima kubwa kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko pamoja na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaoshiriki katika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019. Kauli mbiu ni “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Katika hija hii, vijana wanasindikizwa kwa mfano, tunza na maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Bikira Maria anaendelea kufanya hija pamoja na waamini kwa kuwaongoza vijana wa kizazi kipya, ili waweze kukita maisha yao katika imani, udugu na mapendo.

Rais Juan Carlos Varela Rodríguez pamoja na familia yake  katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, yeye pamoja na familia yake, wanashiriki kikamilifu tangu mwanzo hadi mwisho, kwa kutambua na kuheshimu maadhimisho haya katika maisha na utume wa vijana ndani na nje ya Kanisa. Wamekuwa wakifuatilia hatua kwa hatua maandalizi ya maadhimisho haya na sasa wako tayari kusherehekea imani, matumaini na mapendo miongoni mwa vijana. Ni heshima kubwa kwa Panama, nchi ndogo kabisa huko Amerika ya Kati kupewa dhamana na wajibu wa kuandaa tukio hili la kimataifa. Lakini, ikumbukwe kwamba, tangu mwaka 2009 imekuwa ikijiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Uinjilishaji nchini Panama. Hii ni changamoto ya kusimama kidete pia kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu sanjari na kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii kwa wale wasiokuwa na sauti!

Ni wakati wa kuwajengea vijana Injili ya matumaini, imani na mapendo. Kanisa nchini Panama katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 linataka kushuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake, kama sehemu ya mwendelezo wa Jubilei ya miaka 500 ya Uinjilishaji nchini Panama. Katika hija hii, Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kukutana na ndugu zake katika Kristo, lakini kubwa zaidi kuwakutanisha vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kujenga na kudumisha madaraja kati ya mataifa na tamaduni zao; kwa kuwakutanisha vijana, tayari kuwa ni mashuhuda na watangazaji wa Injili ya matumaini kwa vijana sehemu mbali mbali za dunia!

Katika kipindi chote cha miaka miwili, familia ya Mungu nchini Panama imeshiriki kikamilifu kwa hali na mali na matumaini yao makubwa ni kuona ulimwengu ulioboreka zaidi katika umoja, upendo na mshikamano wa dhati! Kuandaa maadhimisho makubwa kiasi hiki, ni changamoto pevu, lakini pia imekuwa ni fursa kwa Panama kuboresha uwezo wake, na hatimaye kuonesha kwa walimwengu kwamba, kukiwepo na utashi wa kisiasa, umoja na mshikamano katika kutekeleza maamuzi yaliyofikiwa inawezekana kufanikisha mradi mkubwa kama huu, wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Hii ni kazi ya ushirikiano ambayo imetekelezwa na Serikali pamoja na Kanisa nchini Panama. Mambo makuu yaliyozingatiwa ni pamoja na: Ulinzi na usalama; dharura na usafirishaji, ili vijana waweze kwenda na kurejea katika makazi yao kwa muda uliopangwa!

Rais Juan Carlos Varela Rodríguez anasema kwa unyenyekevu mkubwa kwamba, katika kipindi cha Juma zima, Panama, macho na masikio ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, yatakuwa yanaelekezwa nchini humo! Panama inataka kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini, umoja na mshikamano, huduma na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Panama iko tayari sasa kumpokea Baba Mtakatifu Francisko pamoja na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia! Yaani, hadi rahaa anasema, Rais Juan Carlos Varela Rodríguez.

Rais: Panama: Vijana
22 January 2019, 10:31