Cerca

Vatican News
CENI: Imemtangaza Bwana Felix Tshisekedi toka chama cha upinzani cha UDPS kuwa "mshindi wa uchaguzi mkuu nchini DRC" CENI: Imemtangaza Bwana Felix Tshisekedi toka chama cha upinzani cha UDPS kuwa "mshindi wa uchaguzi mkuu nchini DRC".  (ANSA)

CENI: Felix Tshisekedi, toka UDP, Rais wa mpito DRC!

CENI, Alhamisi, tarehe 10 Januari 2019 imemtangaza Bwana Felix Tshisekedi kutoka Chama cha upinzani cha UDPS kuwa ni “mshindi wa mpito” wa Uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo hapo tarehe 30 Desemba 2018 kwa kupata asilimia 38% katika matokeo ya uchaguzi uliopita, sawa na kura milioni 7. Tshisekedi anasema, kipaumbele chake cha kwanza ni kupambana na umaskini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tume ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, CENI, Alhamisi, tarehe 10 Januari 2019 imemtangaza Bwana Felix Tshisekedi kutoka Chama cha upinzani cha UDPS kuwa ni “mshindi wa mpito” wa Uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo hapo tarehe 30 Desemba 2018 kwa kupata asilimia 38% katika matokeo ya uchaguzi uliopita, sawa na kura milioni 7. Bwana Felix Tshisekedi anasema, kipaumbele chake cha kwanza ni kupambana na baa la umaskini nchini humo!

Bwana Corneille Nangaa, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo amefafanua kwamba, washiriki wengine katika uchaguzi huu wamepata kura kama ifuatavyo:  Bwana Martin Fayulu amepata kura milioni 6.4 na Emmanuel Ramazani Shadary kutoka katika Chama tawala nchini humo amepata kura milioni 4.4. Hili ni tukio la kihistoria nchini DRC kufanya mabadiliko ya uongozi kwa njia ya kidemokrasia hata kama wachunguzi wa mambo wanasema, kulikuwepo na kasoro kubwa zilizojitokeza wakati wa mchakato mzima wa kupiga kura nchini DRC.

Wakati wote wa mchakato wa uchaguzi mkuu, Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO limeitaka familia ya Mungu nchini DRC kuhakikisha kwamba, inalinda na kudumisha amani na utulivu wakati na baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu na kwamba, matokeo yanayoweza kukubalika ni yale tu yaliyohesabiwa kutoka kwenye vituo vya kupigia kura. Viongozi waliokuwa wanashiriki katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu nchini DRC, wakiongozwa na Bwana Martin Fayulu walisikika wakisema, matokeo ya uchaguzi mkuu nchini humo hayana mjadala!

Rais Joseph Kabila anayemaliza muda wake wa uongozi kwa njia ya kidemokrasia, aliingia madarakani kunako mwaka 2001 baada ya baba yake Rais Laurent Kabila, aliyemwangusha Rais Mobutu Sese Seko madarakani kunako mwaka 1997 kuuwawa. DRC, tangu mwaka 1960 imekuwa ikiandika historia ya uongozi kwa damu ya viongozi waliouwawa kuanzia kwa Waziri mkuu wa kwanza Bwana Patrice Lumumba, aliyeuwawa miezi minne tu, baada ya DRC kujipatia uhuru wake kutoka kwa Ubelgiji.

Wachunguzi wa mambo wanasema, rasilimali na utajiri mkubwa wa madini yaliko nchini DRC, uchu wa mali, madaraka na sifa ni kati ya mambo ambayo yameendelea kusababisha vita, kinzani na migawanyiko nchini humo. Matokeo yake ni baa la umaskini kuendelea kuongezeka kila kukicha, milipuko ya magonjwa kama Ebola, imekuwa ni wimbo usiokuwa na kiitikio, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha ni mambo ya kawaida nchini DRC, licha ya madini yake kutumika kutengenezea simu za viganjani sehemu mbali mbali za dunia! Wananchi wa DRC wanasema kwa sasa wanataka amani na utulivu, ili kufurahia matokeo ya kidemokrasia nchini mwao kwani wamechoka kulia na kuomboleza! Kwa miaka mingi wametokwa machozi, lakini machozi yao yameishia majini kama kilio cha samaki!

Matokeo Uchaguzi Mkuu DRC 2019
10 January 2019, 08:43