Tafuta

Ndiye Rais wa mpito nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Bwana Felix Tshisekedi, aliyetangazwa na Tume ya Uchaguzi kwa ushindi wa asilimia 38 ya kura zilizopigwa hadi sasa Ndiye Rais wa mpito nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Bwana Felix Tshisekedi, aliyetangazwa na Tume ya Uchaguzi kwa ushindi wa asilimia 38 ya kura zilizopigwa hadi sasa 

Congo DRC:Je ushindi wa Rais Tshisekedi utaleta mshikamano ndani ya nchi?

Tarehe 30 Desemba 2018 ulifanyika uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na kuibuka mshindi Felix Tshisekedi kuwa rais na ndiye mtoto wa kiongozi maarufu Etienne Tshisekedi katika masuala ya kiupinzani wa kisiasa nchini humo. Je Kiongozi huyo mpya ataweza kuunganisha nchi yenye kuwa tayari na changamoto nyingi?

Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Hali ya Kinshasa mji Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC inaelekea kuwa ya utulivu. Kumetokea  ndiyo ghasia lakini mji kwa sasa unaendelea na maisha ya kawaida, japokuwa tunatambua kuwa ajali za vifo zilizotokea katika baadhi ya miji. Hata hivyo walio wengi wanasema kuwa ushindi wa mpito wa Felix Tshisekedi unaficha uongo uliofanyika katika kuhesabu kura, lakini mwisho wake matokoe hayo yatakubaliwa na nchi itaendelea mbele. Ndiyo mtazamo kwa baadhi ya watu wa dini ambapo Shirika la habari za Kimisonari Fides wameweza kukusanya mara baada ya kutangaza matokeo ya kwanza ya uchaguzi wa Rais ambao ulifanyika tarehe 30 Desemba 2018 na kuibuka Kiongozi wa upinzani nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Congo Bwana Felix Tshisekedi.

Na kwa mujibu wa  Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (CENI) imesema kuwa Tshisekedi amepata asilimia 38.57 ambayo ni takriban 6.4 milion ya kura zote na kuwashinda wapinzani wake Martin Fayulu na  Emmanuel Ramazani Shadary;na hivyo ikamtangaza kuwa rais mpya wa mpito nchini DRC. Bwana Felix Tshisekedi, mwenye umri wa 55  ni mtoto wa  kiongozi mkongwe na maarufu  wa upinzani  wa kihistoria katika Utawala wa Mobutu Sese Seko na Laurent Desire Joseph Kabila. Baba yake amekuwa akikamatwa na kuwekwa gerezani na kutolewa na kutumikia serikali, katika kipindi takriban cha miaka 60 ya harakati zake za siasa mpaka alipofariki mwaka 2017.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili nchi ya DRC

Hata hivyo Tarehe 11 Januari 2019, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa  limefanya kikao chake ccha kawaida kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambapo wajumbe wamepata taarifa kuhusu kinachoendelea hivi sasa nchini humo kufuatia kutangazwa kwa Felix Tshisekedi kuwa rais mteule wa  nchi hiyo. Naye Bi Leila Zerrougui, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC akihutubia kwa njia ya video kutoka mjini Kinshasa amesema tangazo hilo la matokeo lilipokelewa kwa mtazamo tofauti ambapo mshindi alisema atakuwa rais wa wote wakati  upande wa upinzani unaendelea kupinga matokeo hayo na kuchochea ukosefu wa utulivu. Hata hivyo ametaja maeneo kama jimbo la Kwilu na kwamba ghasia zilisababisha watu wapatao 12 kuuawa wakiwemo polisi na raia huku mali zikiharibiwa.

Tathimini za Monusco katika hali halisi za kuzuia ghasia

Pamoja na hayo amesema kuwa hivi sasa wanajiandaa kupeleka watu wao huko Kikwit kutathmini hali halisi na kuzuia ghasia kwa kuwa eneo hilo hakuna walinda amani wa ujumbe wa  Umoja wa Mataifa (MONUSCO). Na huko Kisangani na maeneo ya jimbo la Kasai matukio pia ya ghasia yaliripotiwa na wanachunguza taarifa za vifo. Bi. Zerrougui ambaye pia ni mkuu wa MONUSCO hata hivyo  amelaani ghasia hizo na kutoa rai kwa wananchi kuepuka vitendo vya ghasia na kujizuia wakati huu. Amewaambia wajumbe kuwa wiki zijazo zinaweza kughubikwa na michakato ya kupinga matokeo na mahakama ya kikatiba kutathmini matokeo. Kwa mantiki hiyo  ofisi  yake itaendelea kushirikiana na wadau wote nchini DRC ili kuhakikisha kuwa mchakato wa kihistoria unamalizika kwa amani. Kadhalika amesihi mshikamano kwa watoto wa Congo DRC wakati nchi hiyo inajiandaa kubadilisha mamlaka ya ngazi ya juu kwa amani na kwamba:” “Tushikamane na DRC ili mchakato wa uchaguzi umalizike kwa amani.

Maisha ya Rais wa Mpito Bwana Felix Tshisekedi

Sehemu kubwa ya maisha yake, Felix Tshisekedi  mwenye umri wa miaka 55 yalikuwa yanafunikwa na kivuli cha baba yake Etienne, kiongozi mkongwe na maarufu sana wa upinzani aliyepta uzoefu wa kukamatwa na kuingizwa gerezana na baadaye kutolewa na kutumikia serikali, katika kipindi takriban cha miaka 60 ya harakati zake za siasa mpaka alipofariki mwaka 2017. Baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Alhamisi asubuhi, Tshisekedi mdogo anaonekana alisema, “Mimi ni rais wa wananchi wote wa Congo,” Tshisekedi aliwaambia maelfu ya wafuasi wake walio kuwa na furaha, wengi wao walikuwa wameparamia ukuta wa jengo la makao makuu ya chama chake na miti iliyoko nje ya jengo hilo ili waweze kumuona kiongozi huyo aliyekuwa jukwaani.

Uchaguzi huo utawezesha kwa mara ya kwanza kwa Congo kukabidhiana madaraka kupitia upigaji kura tangu nchi hiyo ipate uhuru wake kutoka Ubelgiji 1960, baada ya miongo kadhaa ya mapinduzi, udikteta, mauaji na vita vya wenyewe kwa wenyewe, lakini na iwapo atakuwa na amri ya kutekeleza ahadi zake za kampeni za kupambana na ufisadi. Lakini bado kuna mashaka juu ya ushindi wa Tshisekedi na wasiwasi iwapo ataweza kuzuia machafuko mapya, kwa maana vifo tayari vimeonekana kutokana  na maandamano yaliyo fanywa na wafuasi wa Fayulu huko upande wa magharibi Alhamisi 10 Januari 2019.

Chama cha UDPS, na mwendelezo wake 

Rais wa mpito ni moja kati ya watoto watano, Tshisekedi, 55, alikulia katika mji mkuu Kinshasa katika miaka ya awali ya utawala wa Mobutu Sese Seko ambaye aliipa nchi hiyo jina la Zaire. Baba yake Tshisekedi alitumikia katika serikali ya Mobutu kabla ya kutofautiana na kuanzisha chama chake cha UDPS, ambacho ndio upinzani wa kwanza kuundwa Zaire, mwaka 1982. UDPS ilivumilia ukandamizaji wa kinyama, na baba yake Tshisekedi alifungwa jela mara nyingi. Felix aliondoka na mama yake na ndugu zake kwenda Ubelgiji 1985, ambapo alifanya kazi za kawaida. Felix alikuwa mwanachama wa UDPS lakini alikuwa anajituma katika hali ya kujificha mpaka 2011, aliposhinda nafasi ya ubunge wa taifa katika uchaguzi uliofanya baba yake kuwa wapili katika uchaguzi ambao kabila alishinda. Lakini chama kilisema kuwa matokeo ya uchaguzi yalikuwa yamechakachuliwa.

Akiwa katika utu uzima afya ya Tshisekedi ilitetereka katika miaka kadhaa iliofuatia na alitumia muda wake mwingi huko Ulaya akifanya matibabu, Felix alijiongeza katika wasifu wake, na kutembelea maeneo kadhaa ya ndani ya Congo 2014. Alikabiliwa na upinzani ndani ya chama, wanachama ambao walikuwa wanamkosoa Kabila kwa kurithi urais kutoka kwa baba yake, Laurent Kabila, aliye uwawa 2001. Baadhi yao walimtuhumu Felix na mama yake kwa kukifanya chama hicho kama ni himaya ya familia yao. Baadhi ya viongozi wa chama walikuwa hususan na wasiwasi mwaka 2015 wakati Felix alipokubali kufanya mazungumzo na wawakilishi wa Kabila ambao walikuwa na lengo la kuzungumzia kipindi cha mpito kitakacho mwezesha Kabila kubakia madarakani wakati muda wake wa kuwepo madarakani utakapo malizika 2016. 

Kifo cha Etienne baba yake

Kifo cha baba yake Etienne  kilitokea mwezi Februari 2017, mara baada ya chama kukubali Kabila aendelee kushikilia madaraka kwa mwaka moja zaidi baada ya maandamano yakutisha, ambayo yalimsukuma Felix katika nafasi ya juu katika upinzani. Tabia yake ya upole na kufanana kwake na baba yake  Etienne  tangu maumbile mpaka kofia yake maarufu ambayo hakuacha kuivaa, ilimsaidia kukonga nyoyo za wengi, viongozi na wanachama wa kawaida katika chama hicho. Lakini, bado baadhi ya viongozi wa muda mrefu wa chama hicho walikuwa wakinung’unika kisiri kwamba Felix hana uwezo wa baba yake Etienne, ambaye mwili wake uko katika nyumba ya kuhifadhia maiti mjini Brussels kwa miaka miwili kwa sababu serikali ilichelea kuwa kurudishwa kwake nchini Congo kutaleta maandamano.

Felix kuungana na Fayulu

Mnamo Novemba 2018, alikubali kumuunga mkono Fayulu katika uchaguzi wa urais ili kuupa upinzani fursa bora zaidi ya kumshinda mgombea ambaye alichaguliwa na Kabila amrithi. Lakini saa 24 baadae, alijitoa kutoka katika mkataba huo, akidai kuwa wafuasi wake walimtaka agombee yeye mwenyewe. Iwapo ushindi wake utapitishwa na ataapishwa kuchukua madaraka baadaye mwezi huu Januari, atakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo mahitaji ya wananchi wa Congo DRC ambao kwa milioni 13 wanaohitaji chakula cha msaada, manung’uniko juu ya uhalali wa ushindi wake ambao unaweza kuhamasisha wapiganaji upande wa mashariki.

12 January 2019, 14:38