Tafuta

Serikali ya Tanzania imeandaa Mpango wa Kupunguza Ukatili wa Jinsia kwa asilimia 50% ifikapo mwaka 2022 Serikali ya Tanzania imeandaa Mpango wa Kupunguza Ukatili wa Jinsia kwa asilimia 50% ifikapo mwaka 2022 

Tanzania imeandaa mpango wa kupunguza ukatili wa kijinsia!

Serikali imeandaa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto kwa lengo la kupunguza kiwango cha ukatili kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022. Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000); Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Jinsia (2005); Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008); Sheria ya Makosa ya Kujamiiana -(1998).

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, Dodoma, & Padre Richard Mjigwa, C.PP. S  - Vatican.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, hivi karibuni amezindua kampeni ya Siku kumi na sita za Kupinga Ukatili wa Kijinsia na kusema kwamba, Serikali imeandaa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto kwa lengo la kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii ya kitanzania kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022. Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000); Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Jinsia (2005); Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008); Sheria ya Makosa ya Kujamiiana – SOSPA (1998).

Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa mpango huo utachangia katika utekelezaji wa mipango na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa kuhusu usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake na wasichana pamoja na haki na ustawi wa mtoto. Kadhalika Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaagiza Wakuu wa Mikoa wote wahakikishe wanasimamia uanzishwaji wa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto kama inavyoelekezwa katika Mwongozo wa uratibu wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto sanjari na kutenga bajeti maalum. Pia Waziri Mkuu amesema watu wenye ulemavu wana mahitaji maalumu na ni wahanga wa ukatili wa kijinsia ameelekeza Jeshi la Polisi kuboresha Dawati lake la jinsia ili liweze kushughulikia kikamilifu masuala ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watu wenye ulemavu. Na kuanzia sasa linaitwa Dawati la Polisi la Jinsia, Watoto na Watu wenye Ulemavu.

Akizungumzia kuhusu maana ya ukatili wa kijinsia amesema ni hali ya kutenda vitendo viovu, vinavyodhalilisha, vinavyotesa, vinavyonyanyasa, vinavyokandamiza, visivyojali haki za kuishi kwa binadamu anaweza kuwa wa kiume au kike. Ukatili wa kijinsia huja katika taswira nyingi. “Aidha, kwa uchache tunapozungumzia ukatili wa kijinsia tunamaanisha vitendo kama vile, vipigo, ubakaji, ukeketaji, ulawiti, matusi,  lugha na vitendo vya udhalilishaji pamoja na kunyimwa fursa za kushiriki katika shughuli za kiuchumi.” “Hivyo, ukatili wa kijinsia ni unyanyasaji wowote unaofanywa na mtu dhidi ya mtu mwingine bila kujali umri, maumbile, kabila, rangi, dini au mtazamo wa kisiasa. Unyanyasaji huu unahusisha mambo mengi kama kumpiga mwanamke au mwanamme, kumnyima mtoto elimu, kumlawiti mtoto wa kike au kiume, kumbagua mtu katika mahitaji ya msingi au kuwanyima urithi warithi wanaohusika.

Aidha, taarifa kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF) za mwaka 2017 zinaonesha kuwa wanawake na wasichana wapatao milioni 750 Duniani waliolewa wakiwa chini ya miaka 18. Halikadhalika, taarifa hiyo inakadiria kuwa wasichana milioni 120 (yaani mmoja kati ya wasichana 10) Duniani wamekumbana na vitendo vya kulazimishwa kufanya ngono bila ridhaa yao.  Waziri Mkuu amesema kama zilivyo nchi nyingine Duniani, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinakabiliwa na tatizo la ukatili wa kijinsia na kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu mwaka 2015/2016 kupitia inakadiriwa kuwa asilimia 40 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 - 49 wamefanyiwa ukatili wa kupigwa au kingono katika kipindi cha maisha yao.

Na Habari kutoka Sudan ya Kusini zinabainisha kwamba, Shirika la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka MSF limeelezea visa vya wanawake wengi kubakwa na kunyanyaswa Sudan ya Kusini, wanawake hao walipokuwa anakwenda kuhemea chakula cha msaada kilichotolewa na Mashirika ya Misaada ya Kimataifa yanayoendelea kuwasaidia waathirika wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan ya Kusini.

Dr. Tuth Okello anasema, hivi karibuni wanawake na wasichana wengi wametibiwa kwenye Kituo chao cha Afya kilichoko mjini Bentiu baada ya kubakwa na kunyanyaswa kijinsia na kwamba, wahusika bado hawajatambuliwa na kutiwa mbaroni. Vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan iliyoibuka tangu mwaka 2013 imekuwa ni chanzo cha mpasuko wa kitaifa kwa misingi ya ukabila na kwamba, ubakaji umekuwa ukitumiwa kama silaha ya kivita na madhara yake ni makubwa nchini Sudan ya Kusini. Vita ya wenyewe kwa wenyewe imekwisha kusababisha watu zaidi 380, 000 kupoteza maisha pamoja na watu zaidi ya milioni nne wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

Wanawake

 

04 December 2018, 13:48